Arusha. Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amezitaka taasisi za kitafiti kuendelea kuimarisha nafasi ya sayansi, teknolojia, na ubunifu katika sekta ya kilimo ili kufanikisha malengo ya Taifa ya kuongeza Pato la Taifa kupitia sekta hiyo.
Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kumshauri Rais katika masuala ya chakula na kilimo, ametoa kauli hiyo leo Desemba 4, 2025, jijini Arusha, wakati akifungua mkutano mkuu wa nne wa mwaka na semina ya Chama cha Wanasayansi wa Kilimo-Mazao Tanzania (CROSAT).
Mkutano huo ulio na kaulimbiu isemayo: ‘Kuendeleza Uzalishaji wa Mazao Yanayostahimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Usimamizi Endelevu wa Udongo na Rasilimali za Maji’, umeendana na jitihada za Serikali za kuibadili sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) na Agenda ya AMP 10/30.
Akizungumzia mchango wa sekta ya kilimo, Pinda amesema kuwa ilizalisha moja kwa moja Sh214.4 bilioni kama mapato ya kodi katika mwaka wa fedha 2023/24, hasa kupitia kodi za mauzo ya nje.
"Mapato hayo yanaweza kuimarika zaidi, hata kufikia mara mbili au tatu, endapo taasisi zetu za kitafiti zitaimarisha nafasi ya sayansi, teknolojia, na ubunifu katika sekta hii," amesema Pinda.
Pinda ameongeza kuwa maazimio na majadiliano ya siku mbili ya semina yatachangia pakubwa katika mjadala wa kitaifa kuhusu namna utafiti na ubunifu vinavyoweza kusaidia utekelezaji madhubuti wa ASDP II katika sekta zote ndogo za kilimo.
Amesisitiza kuwa usimamizi bora wa udongo na rasilimali za maji ndicho msingi wa kilimo endelevu, kwani bila udongo wenye afya na mifumo imara ya maji, uzalishaji na usalama wa chakula haviwezi kuimarika.
"Serikali inaendelea kuwekeza katika umwagiliaji, usimamizi wa rutuba ya udongo, na matumizi ya teknolojia rafiki kwa tabianchi ili kuongeza uzalishaji na ustahimilivu, hususan kwa wakulima wadogo hivyo nanyi imarisheni teknolojia na ubunifu kufanikisha haya yote."
"Kwa sasa, asilimia 65.6 ya Watanzania wanajihusisha moja kwa moja na shughuli za kilimo, ambapo uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2022/2023 ulifikia tani 20,402,014, ukilinganisha na tani 17,148,290 msimu wa 2021/2022, sawa na ongezeko la asilimia 19, hatua iliyoongeza uhakika wa chakula na kuboresha kipato cha kaya," amesema.
Pinda amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha utafiti, kwa kutenga Sh40.73 bilioni kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), ambazo ziliwezesha kuzalishwa teknolojia mpya 64 zinazoongeza ufanisi na ustahimilivu wa uzalishaji.
Ametoa wito kwa washiriki wa semina kuwekeza nguvu katika suluhu za kiutafiti zinazotekelezeka na zinazoweza kupanuliwa.
"Tambueni kuwa sayansi na ubunifu havipaswi kubaki kwenye maabara au makaratasi, bali lazima yafikishwe shambani ili kuongeza tija na maisha ya wananchi," ameshauri.
Akizungumza kabla ya ufunguzi, Profesa Kallunde Sibuga, Mwenyekiti wa CROSAT na Mhadhiri Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Mazao na Bustani, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), amesisitiza kuwa kilimo kimeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa kwa kuwa sekta hii inachangia asilimia 16.1 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa asilimia 65.6 ya Watanzania.
Ametumia nafasi hiyo kumuomba Waziri Pinda kuwa mlezi wa CROSAT ili kusaidia kufikisha mahitaji yao mbele.
Aidha, Profesa Joseph Ndunguru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Dawa za Wadudu (TPHPA), amesema shirika lake linafanya kazi kuhakikisha Tanzania inabaki mbele katika utafiti wa kilimo na ubunifu.
Amebainisha kuwa zaidi ya watu milioni 580 barani Afrika wanategemea kilimo, huku sekta hiyo ikichangia asilimia 25 tu ya Pato la Bara.