Mahakama Yaachia Huru Washtakiwa 105 wa Uhaini Arusha
Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini washtakiwa 105 kati ya 100 waliokuwa wakishtakiwa katika kesi tatu tofauti.
Miongoni mwa walioachiwa ni watoto saba waliokuwa na umri chini ya miaka 18 ambao kwa pamoja walikuwa wakishtakiwa kwa kesi za uhaini, pamoja na mwanamke mwenye ujauzito wa wiki 18.
Uamuzi huo umefikiwa Jumatano Disemba 3, 2025 na Hakimu Mkazi Regina Oyier, baada ya Wakili wa Serikali kuieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
TNC imebaini kuwa DPP alitumia kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Washtakiwa hao walikuwa wakishtakiwa katika kesi tatu tofauti ambao kwa pamoja wanawakilishwa na mawakili kadhaa wakiongozwa na Khamisi Mkindi, mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Arusha.
Mashtaka Waliyokuwa Wakikabiliwa
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa ya kula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kutenda kosa lenyewe.
Wanadaiwa kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29, 2025 walifanya njama mbalimbali za kutenda kosa la uhaini.
Kosa la pili ni kufanya uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mgawanyo wa Washtakiwa
Katika kesi ya kwanza washtakiwa 51 waliwachiwa huru, kesi ya pili wakiachiwa washtakiwa 33 na watano kubaki, huku kesi ya tatu wakiachiwa washtakiwa wote 21.
Baada ya maombi hayo, Hakimu Regina amefikia uamuzi wa kuwaachia huru watoto hao bila masharti ya kuripoti polisi.
Watoto hao wenye umri wa chini ya miaka 18 na mwanamke mwenye ulemavu wa kuzungumza na kusikia hawajapewa masharti ya kuripoti, huku mshtakiwa mmoja mwanamke mwenye ujauzito wa wiki 18 akitakiwa kuripoti miezi mitatu baada ya kujifungua.
Washtakiwa Watano Warejeshwa Gerezani
Washtakiwa watano wamerejeshwa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo ambapo upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi dhidi yao haujakamilika na Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, 2025 itakapotajwa tena.
Novemba 24, 2025, washtakiwa wengine 24 wa kesi za uhaini mkoani Arusha waliachiwa na mahakama hiyo na kuwa watakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja wakitakiwa kuripoti polisi mara moja kwa mwezi.