Mahakama ya Kahama Yawaachia Huru Watuhumiwa Sita
Shinyanga. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama leo Jumanne, Desemba 2, 2025 imewaachia huru na kuwafutia mashtaka yaliyokuwa yanawakabili watuhumiwa wengine sita kati ya tisa waliokuwa wameshikiliwa.
Walioachiwa ni Mohammed Mzungu, Ally Paulo, Peter Mhoja, Isaac Gerald, Dickson Mkoko na Godfrey Andrea.
Wote kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni unyang’anyi wa kutumia silaha, kuchoma mali na uharibifu wa mali.
Uamuzi huo umefikiwa leo Jumanne Desemba 2, 2025, na hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Christina Chovenye baada ya wakili wa Serikali, Salome Mbughuni kuieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao.
Akisoma shauri hilo nambari 26513 la 2025, Mbughuni amesema uamuzi huo wa DPP unafuatia kifungu namba 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Wakili wa utetezi, Evodius Rwamgobe amesema wao hawana kipingamizi na uamuzi wa DPP kuhusiana na kufutwa kwa shauri hilo, huku akiiomba mahakama kuharakisha upelelezi wa wateja wake waliosalia.
"DPP anayo mamlaka ya kushitaki na kufuta shauri lolote kisheria, leo hapa kwa wateja wangu sita ametumia kifungu namba 92 (1) ambapo amesema hana nia ya kuendelea na shauri hili," amesema Rwamgobe.
Akizungumza baada ya kuachiwa, mkazi wa Kahama, Godfrey Andrea ameishukuru Serikali kwa uamuzi huo.
"Walinikamata maeneo ya Lumambo stendi nikienda kuchukua mahitaji yangu, na leo wameona sina hatia wameamua kuniachilia, nashukuru sana Serikali yangu," amesema Andrea.
Mmoja wa wazazi ambao kijana wake mmoja kati ya wawili waliokamatwa ameachiwa, Regina Rutege ameishukuru na kuiomba Serikali kuona namna ya kuwasamehe na kuwaachia vijana wanaoshikiliwa ili waendelee na majukumu katika familia zao.
"Kukamatwa kwa watoto wangu kumeniathiri kwa sababu nilikuwa nawategemea, mimi ni mjane na namlea mama mkwe wangu mwaka wa sita anaugua kansa yupo kitandani, sina kazi yoyote ninayoifanya," amesema Rutege.