Vyama vya Kitaaluma Vyalalamika Kuhusu Usimamishaji wa Watumishi Tabora
Dar es Salaam. Vyama vya kitaaluma, likiwemo Baraza la Madaktari Tanzania (MAT), vimesema utaratibu haukufuatwa wakati wa kusimamishwa kazi watumishi watatu mkoani Tabora, akiwemo tabibu anayetuhumiwa kumbaka mgonjwa Novemba 24 mwaka huu.
Jana, Desemba Mosi, 2025, watumishi watatu wa kada ya afya, akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Urambo, walisimamishwa kazi, huku wengine wawili wakiendelea kuhojiwa, kufuatia tuhuma ya mgonjwa kubakwa na tabibu na matukio mengine ya uzembe kazini.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, wakati wa ziara maalumu ya kamati ya usalama ya mkoa wilayani Urambo, siku moja baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kutoa maelekezo ya kuchukuliwa hatua kwa mhusika wa kitendo hicho cha ubakaji.
Maelekezo ya Waziri Mkuu
Dk Mwigulu alitoa maelekezo hayo Novemba 30, 2025, alipozungumza katika mkutano wa hadhara viwanja vya Magufuli, Leganga, wilayani Arumeru, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, 2025.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya kitaaluma wamesema suala hilo ni la kimaadili na la kitaaluma pia. Wamesema kama mtumishi wa afya anatuhumiwa kufanya jambo kinyume na maadili, vipo vyombo vilivyowekwa kisheria kushughulikia kabla ya hatua zaidi.
Msimamo wa MAT
Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko, amesema kuna mabaraza ya kitaaluma yaliyotakiwa kupewa jukumu hilo kwanza, na endapo yakibaini kuna makosa, mhusika atavuliwa na kukabidhiwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
"Taarifa tulizozisikia kwa Waziri Mkuu ni za upande mmoja. Vyama vya kitaaluma tunasikia juu juu hili suala halijatufikia. Ushauli wetu, tungeacha vyombo vinavyohusika vichukue hatua zinazopaswa. Mtaaluma hufakuzwi hadharani kwa makusudi au kwa kuwa tu limetokea jambo," amesema Nkoronko.
Amesema mtaaluma ni lazima apewe haki ya kiasili kwanza, kwa kupewa nafasi baraza au chama chake cha kitaaluma wachunguze na kujua undani wake kwanza kwa kuhoji pande zote mbili.
"Wataaluma hawapendezwi kuishi kwa matamko. Tunadhani Waziri alitakiwa atoe maelekezo kimamlaka kwa vyombo vya usalama, na mabaraza ya kitaaluma yafanye uchunguzi na kuthibitisha kama ametuhumiwa, watamwacha kwenye jinai," amefafanua.
Onyo kwa Wataalamu
Hata hivyo, Dk Nkoronko amewaasa wataalamu wote wanaoshughulika na masuala ya afya wafuate kanuni, sheria, miongozo na maadili ya taaluma zao wakati wote, bila kujali ni mchana au usiku, kwa mtoto au mkubwa, iwe ni mwanamke au mwanaume.
"Huo ndiyo wajibu wetu, ila panapotokea changamoto, zishughulikiwe kupitia pande zote mbili na vyombo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria, tukiangalia suala hili halijatokea hivi karibuni," amesema.
Naye Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Alexander Baluhya, ameeleza kusikitishwa na suala hilo akisema hawezi kulifafanua kwa sasa: "Nimesikia kwenye vyombo vya habari, sijalifuatilia kwa kina, kwahiyo sina maelezo sahihi ya kusema kwa sasa."
Utaratibu Sahihi wa Kisheria
Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Dk Beatrice Mwilike, ameeleza utaratibu sahihi unaotakiwa kutumika iwapo mkunga amepata changamoto kazini.
"Ikitokea mkunga amepata changamoto kazini, katika suala la utendaji, taarifa ipelekwe Baraza la Uuguzi na Ukunga. Baraza huunda kamati kufuatilia, kujua uhalisia na ukweli wa tukio kwa kuhoji pande zote mbili, na wakishapata ukweli, hatua stahiki huchukuliwa kwa kushirikisha vyombo husika," amesema Dk Mwilike.
Maelezo ya Tukio
Akielezea tukio hilo, mwathirika ambaye jina lake limehifadhiwa, amesema Novemba 24, 2025, akiwa na mumewe walikwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo kwa ajili ya matibabu ya tatizo la uzazi, alipokabiliwa na tabibu huyo, ambaye alitumia chumba cha upasuaji kumuhudumia.
"Alinibaka kwenye chumba hicho," alidai mlalamikaji.
Amesema wakati tabibu amemuelekeza kwamba dawa hiyo atakuwa anaingiza sehemu za siri kila siku kidonge kimoja na asishiriki tendo la ndoa, alishangaa kuona tena akimuelekeza kuvua nguo ili amuingizie dawa, ambapo alitumia uume wake.