Madiwani 19 Waapiwa Halmashauri ya Ubungo, Mlaki Meya Mpya
Dar es Salaam. Madiwani 19 wakiwemo wa viti maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam leo Jumanne, Desemba 2, 2025 wamekula kiapo kuwatumikia wananchi huku wakiahidi kuwatafutia fursa za kiuchumi vijana na kina mama.
Sambamba na hilo, suala la maji, barabara, umeme na usimamizi wa miradi mipya pia ni ahadi zilizotolewa na madiwani hao katika ofisi za Manispaa ya Ubungo zilizopo Luguruni.
Wakiapa mbele ya wananchi waliohudhuria, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, kamati ya siasa Wilaya pamoja na wageni waalikwa, madiwani hao wamesema jukumu lililopo ni kuwatumikia wana Ubungo kwa bidii.
Laurence Mlaki Achaguliwa Meya wa Ubungo
Katika kikao hicho cha kiapo, Diwani wa Goba, Laurence Mlaki amechaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo ambapo amepata kura za ndiyo 19.
Meya Mlaki amesema watabuni vyanzo vya mapato na fursa kwa vijana na wanawake ili wakuwe imara kiuchumi. Amesema yuko tayari kuwatumikia wana Ubungo kwa moyo wake wote.
"Lengo letu Ubungo kukusanya Sh50 bilioni kwa mwaka. Tunataka pia kubuni vyanzo vingine vya mapato ili kufikia malengo yetu. Tutatengeneza fursa kwa vijana na wanawake waweze kujiajiri ili kuendesha maisha yao," amesema Meya Mlaki.
Ally Bakari Naibu Meya Mpya
Kwa upande wake, Naibu Meya ambaye ni Diwani wa Manzese, Ally Bakari aliyeshinda kwa kupata kura 19 pia amesema ataleta umoja na mshikamano kwa watu wote wakiwemo madiwani na watumishi.
Jana Jumatatu, wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao ni madiwani wa Manispaa ya Ubungo walimchagua Mlaki kugombea nafasi ya Mstahiki Meya.
Mlaki sasa anakuwa Meya, nafasi iliyokuwa ikitumikiwa na Jaffary Nyaigesha.
Katika uchaguzi huo uliofanyikia ofisi za wilaya za chama hicho, alichaguliwa kwa kura 17 huku akiwashinda Zaidi Muliro aliyepata kura moja na Ashura Sengondo aliyepata kura mbili.
Madiwani Waahidi Kutatua Changamoto
Diwani wa Mabibo, Ashura Sengodo amesema atashughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo vivuko na huduma za msingi kwa wananchi.
Naye, Diwani wa Kibamba, Otaigo Mwita amesema kazi iliyo mbele yake ni utatuzi wa changamoto za majina ya barabara pamoja na kuwasaidia wana Kibamba kiuchumi.
"Changamoto kubwa ni kuunganisha barabara za ndani pamoja na vivuko, maji safi na salama, na zahanati. Vyote hivi tutaenda kufanyia kazi," ameeleza Diwani Mwita.
Awali, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli ambaye ndiye Katibu wa kikao hicho, amesema kura zilizopigwa ni ndiyo au hapana kwa kuwa hakukuwa na mgombea kutoka chama kingine.