Tanzania Ni Salama, Watalii Wakaribisha Kutembelea Vivutio Mbalimbali
Arusha – Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, ametoa ujumbe wa kuwakaribisha watalii kutoka nchi mbalimbali kuja kutembelea vivutio vya utalii nchini na kudhibitisha kuwa Tanzania ni salama.
Dk Kijaji ambaye ameongozana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Hassan Abbas, wamekuwa wakitembelea hifadhi mbalimbali jijini Arusha kujiunza na kujionea shughuli za uhifadhi na utalii. Ziara hii inalenga pia kujitambulisha katika taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.
Akizungumza katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara Novemba 27, 2025, Waziri huyo alisisitiza kuwa Tanzania ni salama na kuwahamasisha Watanzania wajitokezwe kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
"Tanzania ni salama tunaendelea kupokea wageni wanaokuja kutembelea na kuona vivutio mbalimbali katika hifadhi zetu na sisi tunakwenda kutembelea hifadhi zote 21 na kukaribisha watalii zaidi waje kwani tuko tayari kuwapokea, tuachane na maneno mengine yanayosemwa wageni wetu karibuni sana," alisema Dk Kijaji.
Awali akiwa Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Waziri alikabidhi miundombinu muhimu ikiweamo magari mawili yatakayosaidia shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, hususan katika kazi za doria na kupambana na moto.
"Tunashukuru Serikali ya China kwa kutupatia vitendea kazi hivi na tutavitumia kama ambavyo dhamira ya kutolewa kwake ilikuwa. Niwasihi tuvitunze na vifanye kazi ili tufikie malengo ya kuhakikisha tunaendelea na kazi ya uhifadhi na kufikia idadi ya watalii milioni nane mwaka 2030," alisema Waziri.
Mmoja wa watalii, Caroline Johanes, alieleza uzoefu wake wa kutembelea Tanzania akisema kwamba amekuja pamoja na familia yake kwa muda wa siku saba kutembelea hifadhi mbalimbali.
"Tuko kwa siku saba hapa na tumeanza leo kwa kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara. Tumeona wanyama wengi na tunaamini tutaendelea kuona wengine zaidi na mandhari nzuri zaidi katika hifadhi zingine. Hali ya hewa ni nzuri sana," alisema.
Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya utalii kama mojawapo ya vyanzo vikuu vya kipato cha Taifa, ikiwa na lengo la kufikia watalii milioni nane kutembelea nchi mennamo mwaka 2030.