Serikali Yawaonya Madereva Wake Wanaokiuka Sheria za Usalama Barabarani
Dar es Salaam – Serikali imewaonya watumishi na wasimamizi wa sera wanaokiuka kanuni za usalama barabarani, huku baadhi ya madereva wa Serikali wakieleza chanzo cha changamoto ni shinikizo la kiutendaji kutoka kwa mabosi wao.
Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, Novemba 26, 2025 alitoa onyo kwa watumishi wa Serikali na wasimamizi wa sera wanaokiuka kanuni za usalama barabarani akisema mwenendo huo unachochea kutokuwa na usawa katika utekelezaji wa sheria baina yao na wananchi wa kawaida.
Alisema kanuni za usalama barabarani nchini Tanzania zinawahusu watu wote kwa usawa na hazipaswi kutekelezwa kwa upendeleo.
Madereva Waeleza Changamoto Zao
TNC imebaini kuwa baadhi ya madereva wa Serikali wamesema wamekuwa wakishinikizwa na mabosi wao kuwahi, hasa wanapokuwa na vikao.
"Ni shinikizo la kiutendaji, huwa tunalazimishwa kuwahi, sasa hii ina maana uendeshe kwa kasi au uharakishe safari," mmoja wa madereva aliye mkoani Dodoma ameeleza.
Dereva mwingine amesema: "Baadhi yetu tumekuwa tukilazimishwa kuendesha kwa mwendokasi au kusafiri haraka, hasa wakati wa kufanya safari za Serikali jambo ambalo mara nyingi linatuweka katika hatari ya ajali kwani huwa chanzo cha kutozingatia sheria za mwendo, alama au tahadhari."
Chama cha Madereva Chatoa Msimamo
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) Mkoa wa Dar es Salaam, Adam Lameck, amesema wameupokea ujumbe wa Waziri Mkuu na tayari wameanza kuufanyia kazi kwa kutoa ujumbe mahsusi wa kuzingatia sheria.
"Baadhi ya madereva wa Serikali wamekuwa wakivunja sheria za usalama barabarani hilo tunakiri, nimetoa rai kwa madereva wenzangu tuna haraka gani sehemu ya mwendokasi 50 tukaenda mpaka 100? Bahati mbaya likitokea jambo dereva mwenyewe upo hatarini zaidi," amesema.
Lameck, ambaye pia ni mjumbe Baraza Kuu Taifa la chama hicho, amesema wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara kwa madereva namna ya kuzingatia sheria, kujilinda wenyewe, vifaa vya magari ya Serikali na watumiaji wengine wa barabara.
Hata hivyo, amekiri kuwapo kwa changamoto zilizotajwa na madereva hao, akisema wengi hushurutishwa pale mabosi wao wanapotaka kuwahi vikao mahali fulani.
"Tunawaambia unapopewa maelekezo unatakiwa kuangalia uweke masilahi yako wewe na kiongozi kwanza, kwa sasa barabara zetu nchini ni nzuri na vyombo vya moto barabarani vimeongezeka, umakini ni muhimu," amesema.
"Pamoja na maelekezo tumia akili, barabara hii inaniruhusu? Ukiona barabara haikuruhusu ni suala la kumwelekeza kwamba haiwezekani, nitajitahidi kadri nitakavyoweza. Viongozi nao wanajua changamoto za barabara, ukimwelewesha naamini atakuelewa na mtaenda sawa."
Ametaja changamoto nyingine kuwa, utii wa sheria bila shuruti barabarani kwa wengi wao ni mdogo, hivyo wamekuwa wakishindwa kutii maelekezo ya askari wa usalama barabarani.
Mikakati ya Chama
Katibu Mkuu wa CMST Taifa, Castro Nyabange, ametaja mikakati ya chama hicho kuwa ni kutoa elimu, hasa kwenye makongamano ya kila mwaka wanapokutana.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha madereva wa Serikali wanakuwa kioo na kielelezo kwa kuheshimu na kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani.
Amesema jukumu hilo pia limekuwa likifanywa na viongozi mbalimbali wa mikoa wa chama hicho, akieleza wameifanya kuwa ajenda ya kudumu ya kuhimizana.
Ametaja changamoto iliyopo ni madereva wengi kutumia mwamvuli wa Serikali kutofuata sheria, hivyo chama kimekuwa kikichukua hatua kadhaa kwa mujibu wa majukumu ya kitaaluma, zikiwamo kumsemea, kumtetea na kumkumbusha wajibu.
Nyabange amesema dereva anapofanya makosa humuonya na kumkanya ingawa nyakati zingine hatua huchukuliwa moja kwa moja bila kushirikishwa.
"Tumefanya kazi kubwa na mwaka huu angalau ajali zimepungua na watu walioathirika tangu mwaka unaanza hawajafiki 20, ikilinganishwa na mwaka 2023 au 2024. Kikubwa tunajitahidi kuzungumza nao, dereva unapokabidhiwa gari wewe ndiye kiongozi wa kile chombo," amesema.
"Ikitokea ajali awajibishwe bosi wako? Inabidi uchukue tahadhari kwa uharaka wako kuhakikisha unafuata sheria, kiongozi afike salama."
Onyo la Waziri Mkuu
Wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, Dk Mwigulu alisema: "Natoa maelekezo kwa Wizara ya Uchukuzi na wadau husika kupitia sheria zetu na kubaini kama kuna zilizopitwa na wakati au hazitoshelezi. Kama zinahitaji marekebisho, yafanyike. Lakini kama bado zinatosha, basi ni lazima kila mtu aziheshimu."
Aliwakosoa madereva wa Serikali wanaopuuza sheria za usalama barabarani, licha ya kuwa kanuni hizo zilipendekezwa na kuidhinishwa na taasisi za Serikali.
"Hakuna aliye juu ya sheria. Wizara husika, polisi na wadau wengine wa usafiri lazima wahakikishe kanuni zote za usalama barabarani zinatekelezwa kwa haki na bila upendeleo."
Alieleza kuwa inasikitisha kwamba, baadhi ya maofisa wa Serikali wamekuwa miongoni mwa wanaoongoza kwa makosa ya barabarani.
Tatizo la Ajali za Magari ya Serikali
Ajali zinazohusisha magari ya Serikali zinaonekana ni jambo la kawaida nchini zikiendelea kusababisha vifo na hasara, huku baadhi ya madereva wakijiona wako juu ya sheria, hivyo hawastahili kuchukuliwa hatua.
Kutokana na hali hiyo, askari wa usalama barabarani wameripoti changamoto katika kuwaadhibu madereva wa magari yenye namba za Serikali, hali inayowafanya kuwa miongoni mwa wanaokiuka sheria za usalama barabarani kwa kiwango kikubwa.
Aprili Mosi, mwaka huu, Baraka Ludohela (32), dereva wa Serikali alifungiwa leseni ya udereva kwa miezi mitatu, hatua iliyozua mjadala kuhusu madereva wa Serikali wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilimfungia leseni ya udereva kwa kutofuata taratibu za usalama barabarani baada ya kuyapita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa kisheria.
Oktoba 24, 2023, Waziri Mkuu wa wakati huo, Kassim Majaliwa, aliwataka madereva wa Serikali kuwa mfano kwa wengine akiwasisitiza kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Alisema kuendesha gari la Serikali haimaanishi umepewa rungu la kuvunja sheria au uko juu ya sheria.
Agosti 20, 2024, Majaliwa alieleza kushtushwa na madai ya madereva wa Serikali kulogana ili wapate magari ya kufanyia kazi, akiwataka wakuu wa taasisi kujali masilahi ya madereva hasa ya kupata mafunzo ya mara kwa mara ya mabadiliko ya teknolojia ya magari ya Serikali yanayoingia.