Kanisa la Ufufuo na Uzima Ladai Uharibifu wa Mali Baada ya Ufunguzi
Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima ukidai kuwapo uharibifu na upotevu wa mali katika kipindi ambacho kanisa lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, Serikali imetaka wafanye tathmini na kuwapelekea taarifa.
Kanisa hilo lilifutiwa usajili Juni 2, 2025. Taarifa ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa, ilieleza kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337: "Kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi."
Tangu usiku wa siku hiyo hadi leo, Novemba 25, 2025, saa 7:30 mchana, kanisa hilo lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, kabla ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, kwenda kuruhusu huduma kuendelea.
Awali, Novemba 24, 2025, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alielekeza kanisa hilo lifunguliwe.
Madai ya Uharibifu wa Mali
Akizungumza muda mfupi baada ya kuruhusiwa kuendelea na huduma, Askofu Baraka Tegge, ambaye ni mchungaji kiongozi na mkuu wa utawala na fedha wa makanisa ya Ufufuo na Uzima, amedai kuwapo uharibifu wa mali na upotevu wa vitu ndani ya kanisa hilo.
"Tumezunguka kuangalia, kuna maeneo yamevunjwa, mali zimepotea. Kwa haraka haraka hatuwezi kusema ni kiasi gani cha uharibifu na upotevu umefanyika. Tunausubiri uongozi wa Serikali ya mtaa ili tukague kabla ya kufanya tathmini," amesema.
Wakiwa ndani ya kanisa hilo, Askofu Tegge, aliyefuatana na viongozi wengine na waumini wachache wa kanisa hilo, wamedai baadhi ya milango, ukiwamo unaofunguka kwa kutumia namba za siri umevunjwa.
Wamedai televisheni kwenye moja ya chumba ndani ya kanisa haipo na chumba cha kuhifadhia sadaka kimevunjwa.
Ndani ya kanisa hilo baadhi ya nguo, majalada na viti vilikuwa vimesambaa, huku kukiwa kumejaa vumbi.
Jibu la Serikali
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Msando, amesema wakati kanisa hilo linafungwa hakukuwa na makabidhiano na hata leo yeye na kamati ya amani ya wilaya hawakwenda kufanya makabidhiano wala ukaguzi.
"Hatujakagua, tumezunguka tu kuangalia kabla ya kuruhusu huduma kuendelea baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu. Hayo yanayosemwa ya uharibifu na upotevu, baba mchungaji (Askofu Tegge) na timu yake watafanya tathmini watuletee," amesema.
Katika hatua nyingine, Msando amezungumzia kauli zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wakidai kufunguliwa kwa kanisa hilo ni mtego ili kumkamata Askofu Gwajima.
Msando amesema kauli hizo si za kweli, kwani Serikali inafanya kazi kwa utaratibu.
Kurudi kwa Waumini
Waumini walianza kumiminika kanisani hapo kuanzia saa 3:00 asubuhi leo, Novemba 25, wakisubiri kukabidhiwa kanisa lao ambalo kwa zaidi ya miezi mitano lilikuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi likiwa limezungushiwa utepe wa rangi nyeusi na njano.
Wakiwa kwenye uwanja wa kanisa wakisubiri maelekezo ya viongozi wao, waumini hao, baadhi wakiwa wamebeba fagio na vifaa vya kupigia deki, walisalimiana kwa bashasha na furaha kwa salamu ya kanisa hilo ya ‘Majeshi Majeshi’ na ‘Utukufu’.
Baadhi walitumia muda huo kukumbushana yaliyotokea kabla na baada ya kufungwa kwa kanisa, walipotawanywa kwa mabomu ya machozi na wengine kukamatwa na polisi walipokusanyika kwa ibada.
Baada ya kanisa kufungwa, baadhi ya waumini walikusanyika kwa ibada nje ya kanisa hilo, eneo la Kibo, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Polisi walipowatawanya, walihamia katika Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) ambako nako waliondolewa na Jeshi la Polisi.
Kutokana na hilo, walihamia ukumbi wa Tanzanite na Kibo Park ambako nako waliondolewa na kuhamia maeneo mengine tofauti hadi leo waliporudi kanisani hapo.
Akizungumza na waumini baada ya kutoka ndani ya kanisa, Askofu Tegge amewataka waumini kufanya usafi wa kimwili kwanza kabla ya ule wa kanisa.
"Lazima tufanye usafi kwanza. Hii ni nyumba ya Bwana iliyokuwa imegeuzwa kuwa pango la wanyang’anyi," amesema huku akishangiliwa kwa nguvu na mamia ya waumini waliojitokeza kanisani hapo wakiongozwa na mitume na maaskofu wa kanisa hilo.