Wafanyabiashara Watarajiwa Kufaidika na Mkataba wa Biashara ya Afrika Kufikia 2030
Morogoro – Wafanyabiashara nchini wametakiwa kujiandaa na ushindani wa kibiashara, kufuatia hatua ya Serikali kushiriki mazungumzo ya kikanda yatakayowezesha bidhaa za Tanzania kuingia kwenye masoko ya Afrika bila ushuru kufikia mwaka 2030.
Hatua hii inatarajiwa kufungua fursa kubwa za biashara, hususan kwa wanachama wa Chamba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya biashara ya Mkoa wa Morogoro, Novemba 24, 2025, katika Uwanja wa Jamhuri, Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA Taifa, Oscar Kisanga amesema wafanyabiashara wanapaswa kuongeza ubunifu na kuboresha ubora wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Vyeti vya Uasili Husaidia Kupunguza Kodi
Kisanga ameeleza kuwa TCCIA imekuwa ikitoa vyeti vya uasili kwa bidhaa zinazozalishwa nchini tangu mwaka 1999, ambavyo husaidia wafanyabiashara kupata punguzo la kodi wanaposafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi.
"Kuna wafanyabiashara wengi wanachama wa TCCIA ambao wanapeleka bidhaa nje ya Tanzania na hupata punguzo la kodi kupitia cheti cha uasili. Kwa mfano, mfanyabiashara anayepeleka bidhaa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kama angepaswa kulipa kodi ya Sh5 au Sh50 kwa bidhaa kama chupa moja ya maji, akitumia cheti hiki analipa Sh1 au Sh5 tu. Huu ni ushindani mkubwa na faida halisi ya kuwa mwanachama," amesema.
Fursa za Masoko ya Kikanda
Kisanga amesema mazungumzo ya kikanda yanayoendelea yatawezesha Tanzania kushiriki katika masoko manne makubwa ya Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na soko la Afrika lenye watu zaidi ya bilioni 1.4.
Amebainisha kuwa ifikapo mwaka 2030, bidhaa za Tanzania zinazokidhi vigezo hazitatozwa kodi kwenye masoko hayo, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara, ajira na uwekezaji nchini.
Morogoro Ghala la Taifa
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Morogoro, Mwadhini Myanza, amesema maonyesho hayo ni matokeo ya maazimio ya Baraza la Biashara la Mkoa wa Morogoro lililoongozwa na Mkuu wa Mkoa, Adam Malima.
Amesema Mkoa wa Morogoro ni muhimu katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara tangu mwaka 2017 na umeendelea kuwa ghala la taifa kutokana na uwezo wake wa kuzalisha mazao mbalimbali yanayopatikana nchini.
Myanza ameongeza kuwa baadhi ya washiriki kutoka Kenya wamehudhuria maonyesho hayo na kuonyesha bidhaa zao.
Amani Msingi wa Maendeleo
Akizindua rasmi maonyesho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amesema lengo lake kuu ni kuwaunganisha wajasiriamali, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi ili kubadilishana ujuzi, kukuza ubunifu na kuimarisha mitandao ya biashara.
Kilakala ameongeza kuwa maonesho ya biashara ni ishara ya kuwepo kwa amani nchini, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kudumisha umoja bila kujali tofauti za dini, kabila au rangi, akisema: "Bila amani, hakuna maendeleo yanayoweza kufanyika."