Watanzania Wanakataa Ubaguzi wa Kidini, Wanaonesha Umoja Mitandaoni
Dar es Salaam – Wamekataa kubaguana, ndiyo uhalisia wa kinachoonekana katika mitandao ya kijamii nchini, waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo wanaonyesha mshikamano na umoja, licha ya tofauti zao za kiimani.
Wimbi jipya la maudhui ya ucheshi kuhusu umoja wa kidini limeibuka kwenye mitandao ya kijamii nchini, likiwa kama ishara ya wazi kwamba Watanzania hawataki kuchezea misingi ya umoja na mshikamano wao. Wengi wanasisitiza kuwa hawataki kuelekezwa nani wambague au ni yupi mbaya.
Hatua hiyo inakuja baada ya kuibuka kauli za baadhi ya viongozi wa taasisi za dini, wanaohusisha baadhi ya matukio yakiwemo la vurugu siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu na tofauti za kidini.
Kutokana na vurugu hizo, baadhi ya watu walipoteza maisha, biashara na mali za watu kuharibiwa na kuibiwa, huku baadhi ya miundombinu ya umma ikichomwa moto.
Kwa siku kadhaa, mitandao kama X, Instagram, Facebook na TikTok imefurika maudhui ya picha, memes na kauli mbalimbali zinazopinga mitazamo ya ubaguzi wa kidini.
Badala ya kushabikia mivutano, wananchi wamejitokeza kuonesha kuwa Tanzania bado ni ngome ya ustaarabu, kuheshimiana na kuishi pamoja bila kinyongo, hasa linapokuja suala la dini.
Kinachoendelea Mitandaoni
Video na picha zinazochapishwa na watu mbalimbali zinaonesha kuwa hawajali utenganisho wa dini, hata salamu za dini zimeanza kuchanganywa kati ya zile za Kiislamu na Kikristo.
Maudhui mengine yanachapishwa Wakristo wakiwa kanisani, huku waumini wakiwa wamevalia mavazi yanayotumiwa na Waislamu katika nyumba za ibada.
Moja ya chapisho katika mtandao wa X lilisema: "Ukinitafuta msikitini utanikuta, usiponikuta nipo kanisani. Tukikutana njiani basi tuende wote tukapate wali wa Sunday Special."
Katika picha jongefu moja iliyosambaa kwenye mtandao wa TikTok, vijana wawili, mmoja akiwa amevaa kanzu na mwingine shati lenye msalaba mdogo shingoni, wanasema, "Tumezoea kuchukua madeni pamoja, leo tena mtutenganishe kwa dini?"
Ndani ya mijadala hiyo ya mtandaoni, baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbusha misingi ya taifa. Mmoja aliandika kupitia X, "Huu ni mwaka 2025; bado mtu akamchukie mwenzake kwa sababu ya dini? Hapana bana, Tanzania ni yetu sote, kuanzia salamu za ‘Amani iwe juu yako (Asalam aleukum)’ hadi ‘Bwana asifiwe’ tunazipokea kwa mikono yote miwili."
Mwingine aliandika, "Kwenye harusi za ndugu zetu Waislamu tunacheza ngoma mpaka miguu inawaka, wao wakija Christmas wanakula pilau mpaka wanaomba second round. Ubaguzi unatoka wapi tena?"
Katika mjadala mmoja raia mmoja alisisitiza umoja wa kidini Tanzania haujawahi kusimama kwenye misingi ya maandiko tu, bali ni matendo.
Aliandika: "Tangu shule ya msingi tulikuwa tukila chakula kwenye sahani moja bila kuulizana ‘We dini gani?’ Sasa leo watu wanaanzisha mijadala ya kututenganisha? Tumekataa."
Kwa upande wa makundi ya vijana, hashtags kama #DiniZoteNdioSisi, #UmojaZaidiYaTofauti na #WatanzaniaTunakataaUbaguzi zimekuwa zikisambaa kwa kasi.
Mtazamo wa Kitaalamu
Wataalamu wa masuala ya jamii wamesema kinachoonekana sasa mitandaoni ni ishara kuwa vijana wanataka kudhibiti simulizi nyingi zinazojaribu kujenga mpasuko wa kidini.
Mwanaasosholojia, Dk Neema Mdoe, amesema ucheshi huo unaotembea mitandaoni ni njia ya jamii kushirikiana kulinda misingi ya amani.
"Watanzania wana uelewa mpana kuhusu thamani ya kuishi pamoja. Ucheshi huu unaoibua taswira ya kuunganisha dini ni sehemu ya juhudi za jamii dhidi ya propaganda na misimamo mikali. Kila taifa lina namna yake ya kupambana na kauli hatarishi, kwetu sisi Tanzania ni mzaha, utani na ujumbe mwepesi unaokataa mgawanyiko," amesema.
Hata hivyo, ucheshi huo haujaibuka kwa bahati mbaya. Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikitajwa kama moja ya nchi zenye kiwango cha juu cha uvumilivu wa kidini barani Afrika.
Utafiti wa mwaka 2024 uliitaja Tanzania kuwa moja ya mataifa na wanafunzi wa dini tofauti hushirikiana zaidi katika maisha ya kila siku kuliko sehemu nyingi duniani.
Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 75 ya Watanzania wana marafiki wa karibu kutoka dini nyingine, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 54 katika nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Hali hiyo pia imejidhihirisha katika utafiti wa Tanzania Interfaith Forum wa mwaka 2023, unaoonesha asilimia 89 ya tofauti za kidini zinaibuliwa na wachache, lakini kiuhalisia hazipo.
Kama hiyo haitoshi, Ripoti ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2024 inaonesha hakuna ongezeko la migogoro inayohusiana na dini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, licha ya misuguano midogo inayojitokeza kwenye majukwaa ya kijamii.
"Tanzania imeendelea kuwa nchi salama ambayo dini hazijawahi kuwa chanzo kikubwa cha vurugu," ilieleza ripoti hiyo.
Sauti za Wananchi
Aneth Mollel (28), mfanyabiashara jijini Dar es Salaam, amesema mafanikio ya utani huo ni kuonesha kwamba Watanzania bado wanathamini utamaduni wa kuheshimiana.
"Hata kama kuna watu wachache wanaotaka kupandikiza chuki, mitandao imetuonesha kuwa wengi wetu tunathamini amani kuliko mabishano ya kidini," amesema.
Kwa upande wa Abdallah Mpache, anayeishi Dar es Salaam, amesema utani huo ni njia ya kukumbushana kuwa dini zinapaswa kuwa moja ya nguzo zinazojenga jamii, si kuibomoa.
"Binafsi naamini dini zililetwa kwa sababu hazikuanza kabla ya binadamu. Hatuwezi kukubali kitu kilichokuja kikatukuta kitumike kututenganisha, hili halitatokea," amesema.
Viongozi wa Dini Wanasemaje
Akizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema inavyoonekana ni kama vijana hawajaeleweka vema.
Ameeleza kizazi cha sasa hakitawaliwi na fikra za kibabe na nguvu yake ni kutoshikamana na dini yoyote, itikadi wala mila yoyote.
"Nguvu ya kizazi hiki ni kutoshikamana na dini yoyote, itikadi yoyote wala mila yoyote. Waliotaka kuwagawa vijana kwa kutumia dini ni sisi wazee. Wamekataa," amesema Askofu Bagonza.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka, amesema kila kinachoshuhudiwa msingi wake ni uhusiano wa muda mrefu uliokuwepo kati ya Uislamu na Ukristo.
Amesema Uislamu umeutambua Ukristo katika kitabu chake kitakatifu cha Quran. Ndani yake kuna sura ya Rumi inayozungumzia kuhusu vita kati ya Wakristo na Waajemi.
"Quran ina sura inayoitwa Rumi na inaeleza kuhusu vita vilivyokuwepo kati ya Warumi (ambao ni Wakristo) na Waajemi. Quran inaeleza kuwa Rumi imepigwa katika vita hivyo, lakini baada ya kipindi kifupi itashinda, na waumini wa dini zote watafurahi," amesema.
Uhusiano mwingine uliopo kati ya dini hizo, amesema, ni ukweli kwamba zote zinaamini katika Mungu mmoja na zinasisitiza kuhusu amani, undugu, upendo na kuishi pamoja.
Ameeleza uhusiano wa dini hizo ulianza kitambo, akirejea hadithi za Kiislamu zinazoeleza Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie) alipokuwa mdogo, wakati anapelekwa Sham nchini Syria ambako angeuawa, aliyemwokoa ni aliyekuwa Padri wa Kikatoliki.
"Padri huyo alisema Mtume Muhammad asipelekwe huko kwa sababu atauawa, pamoja na kwamba alijua huyo ni Muislamu na yeye ni Mkristo," amesema.
Sheikh Mataka ametahadharisha kuwa yanayoendelea yasibebwe zaidi na wasio na elimu wala umahiri wa dini hizi, kwani kuna hatari ya kuupotosha umma.
"Jambo la taaluma za kidini ni hatari kushikwa na watu wasio na taaluma za kidini. Ukiona makundi yanashughulika na masuala ya kidini bila taaluma wala umahiri, ni jambo tunalohitaji kuchukua hadhari kwa sababu linaweza kuibua tatizo baadaye," amesema.