Watuhumiwa wa Vurugu za Uchaguzi Waachiwa Huru Mahakamani
MIKOANI – Watuhumiwa wa makosa ya kuchoma moto, kuharibu mali za umma na unyang’anyi wa kutumia silaha wakati wa vurugu za maandamano siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, wameachiwa huru katika mahakama mbalimbali nchini.
Watuhumiwa hao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka wakihusishwa kwenye kushiriki kwenye maandamano yaliyotawaliwa na vurugu yaliyojitokeza katika baadhi ya mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe.
Wakati akilihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma, Novemba 14, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza msamaha kwa vijana waliokamatwa wakati wa maandamano hayo na kufunguliwa kesi za uhaini, akieleza kuwa wengi wao wanaonekana kufuata mkumbo.
Hivyo, alimweleza Mwendesha Mashtaka (DPP) kuwafutia kesi vijana wa aina hiyo, kwani hawajui walitendalo.
Arusha: Washtakiwa 24 Waachiwa Huru
Mkoani Arusha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini washtakiwa 24 waliokuwa wakishtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni kula njama ya kutenda kosa pamoja na uhaini.
Uamuzi huo umetolewa Jumatatu, Novemba 24, 2025, na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erasto Philly, baada ya mawakili wa Serikali kuieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao.
"Shauri linakuja kwa ajili ya kutajwa, lakini hata hivyo DPP, kwa niaba ya Jamhuri, hana nia ya kuendelea kuwashitaki washtakiwa chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya CPA. Tunaitaarifu Mahakama kwamba DPP hana nia ya kuendelea kuwashitaki washtakiwa wote katika shauri hili," amesema Wakili wa Serikali.
Katika kesi ya kwanza namba 26624/2025, washtakiwa 19 walioachiwa ni Hongson Kishe, Wili Mollel, Josia Talalai, Noel Sawe, Henry Paul, David Mollel, Evance Shirima, Elisha Shirima na Noel Dennis.
Wengine ni Calvin Mboya, Sifuni Pallangyo, Gilbert Tesha, Alex Zaghenea, Francis Kyehe, Jackson Lyimo, Obrey Mmbaga, James Mbise, Cornelio Mtui na Zahara Munna.
Katika kesi ya pili namba 26621/2025 kulikuwa na washtakiwa watano ambao ni John Mafie, Moris Matei, Christoph Joseph, Joshua Kaaya na Yohana Saimalye.
Washtakiwa wote 24 walikuwa wakiwakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Arusha, Khamisi Mkindi.
Wakili Mkindi alieleza Mahakama kuwa wamepokea taarifa hiyo kwa moyo mkunjufu na hawana pingamizi.
"Kama mleta mashtaka alivyoomba, hati ya nolle prosequi imepokelewa na utetezi umekubaliana. Mahakama inaondoa rasmi shauri na mnaachiliwa huru chini ya kifungu kilichotajwa," amesema Hakimu.
Mwanza: Watuhumiwa 139 Wafutiwa Mashtaka
Kwingineko mkoani Mwanza, jumla ya watuhumiwa 139 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini, kuchoma moto na kuharibu mali za umma siku ya uchaguzi mkuu, wameachiwa huru baada ya DPP kuondoa kesi zao mahakamani.
Waliofutiwa mashtaka ni 76 wenye makosa ya kutenda kosa (uhaini) kutoka Wilaya ya Ilemela na 63 wenye mashtaka ya kuharibu mali kwa makusudi, unyang’anyi wa kutumia silaha na kuchoma moto kutoka Wilaya ya Nyamagana.
Watu hao ni miongoni mwa takribani watuhumiwa 281 waliokuwa wameshtakiwa katika wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza kutokana na matukio ya vurugu na maandamano yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu na siku zilizofuata.
Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka katika Mahakama za Wilaya ya Ilemela na ile ya Nyamagana, katika mashauri manne tofauti yaliyotajwa kwa mara ya pili na ya tatu.
Uamuzi wa kufuta mashtaka yao umekuja baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya DPP ya kuonyesha nia ya kutotaka kuendelea na kuwashtaki, hivyo kuomba mashtaka hayo yaondolewe mahakamani kwa washtakiwa waliotajwa.
Kwa upande wa Ilemela, mashauri hayo ni kesi namba 26641/2025 na 26565/2025 ambazo zimesomwa kwa nyakati tofauti mbele ya Mahakimu Wakazi Wakuu wa Mahakama hiyo, Stella Kiama na Christian Mwalimu, kuanzia saa 7 hadi saa 8 mchana.
Katika kesi namba 26641/2025 inayowakabili watuhumiwa 61, ambayo imesomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama, upande wa mashtaka umeongezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Safi Amani, pamoja na Mwanahawa Changale na Clara Mhando.
Dar es Salaam: Washtakiwa 47 Waachiwa Huru
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, DPP amewafutia kesi na kuwaachia huru washtakiwa 47 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda kosa la uhaini.
Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, akishirikiana na Cathbert Mbiling’i, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26645 ya mwaka 2025 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mrema ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo kwa washtakiwa 47 kati ya 48 waliopo katika kesi hiyo.
Hata hivyo, washtakiwa hao wamefutiwa kesi chini ya kifungu namba 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.
"Kwa kuwa Jamhuri haina nia ya kuendelea na kesi hii isipokuwa mshtakiwa Nasrim, washtakiwa mnajulishwa kuwa kifungu hiki kilichotumika kuwafutia kesi ndicho kinachoweza kutumika kuwakamata tena iwapo Jamhuri itajiridhisha kuona ushahidi upo, watawarudisha mahakamani," amesema Hakimu Swallo na kuwaachia huru.