TLS Yatangaza Kuwatetea Bure Watuhumiwa wa Vurugu za Baada ya Uchaguzi
Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetangaza kuwatetea watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kushiriki maandamano yaliyoambatana na vurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, kikibainisha kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba wengi wao wana uwezo mdogo wa kifedha.
TLS imesema sababu nyingine ni kutekeleza wajibu wake wa huduma kwa jamii, pamoja na kubaini changamoto za uelewa wa kisheria kwa baadhi ya watuhumiwa.
Hatua ya chama hicho inakuja wakati tayari zaidi ya watuhumiwa 641 wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali, ikiwemo ya uhaini huku mamia wengine wakingali kwenye vituo mbalimbali vya polisi.
Watuhumiwa Zaidi Wanafikishwa Mahakamani
Kuanzia wiki iliyopita, Jeshi la Polisi limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuhusika na vurugu hizo.
Maandamano yaliyozaa vurugu yaliyofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songwe, Mwanza na Dodoma, Geita, Shinyanga na mingineyo, ambako watu kadhaa wamepoteza maisha, kujeruhiwa na mali za watu binafsi na Serikali kuharibiwa.
Hata hivyo, jeshi hilo halijaeleza lolote kuhusu idadi ya watu waliopoteza maisha katika matukio hayo.
Mbali na watuhumiwa hao, Jeshi la Polisi pia limewakamata viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kisha kuwaachia kwa dhamana.
Miongoni mwa viongozi hao waliokamatwa, yumo Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Aman Golugwa, mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Pwani, Boniface Jacob, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
Wengine ambao jeshi la polisi lilitangaza kuwasaka lakini hawakukamatwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho, Deogratius Mahinyila, Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Hilda Newton na kada Award Kalonga.
Pia, wengine waliotajwa wanatakiwa kukamatwa ni Askofu wa Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Naibu Katibu Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo na Uzima, Askofu Maximilian Machumu Kadutu maarufu Mwanamapinduzi.
TLS Yatoa Huduma za Kisheria Bure
Akizungumzia hilo leo Jumanne, Novemba 11, 2025 jijini Dar es Salaam, mmoja wa mawakili, William Maduhu amesema wameamua kuchukua jukumu hilo kama wajibu wao kutoa huduma kwa jamii, baada ya kubaini changamoto za uelewa na uwezo wa kifedha kwa watuhumiwa wengi.
Amesema mashauri hayo yaliyoanza kufunguliwa Novemba 7, 2025 katika mahakama mbalimbali nchini yanahusisha makosa mazito kama uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha, uchomaji na uharibifu wa mali.
"Watuhumiwa wengi ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25, baada ya tathmini, tulibaini kuwa uelewa wao wa kisheria ni mdogo na wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za mawakili wa utetezi, hivyo, TLS imeamua kuwatetea bure bila ubaguzi," ameema Maduhu.
Amesema baada ya kufuatilia vituo vya polisi na mahakamani, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa watuhumiwa zaidi ya 400, Mwanza zaidi ya 200, Kilimanjaro 312, Mbeya zaidi ya 300, Njombe 12 na Tabora watano.
Amesema hadi sasa watuhumiwa 641 wamefikishwa mahakamani katika mikoa mbalimbali nchini huku wengine wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
"Wapo watuhumiwa waliokamatwa kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Tumetembelea baadhi ya vituo vya polisi na mahakamani kupitia kesi zinazofunguliwa na kubaini idadi hiyo kubwa ya vijana wanashikiliwa wakisubiri taratibu za kisheria," ameongeza.
Usambazaji wa Watuhumiwa Katika Mikoa
Maduhu ameeleza kufikia sasa watuhumiwa 240 wa Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za uhaini, Mwanza watuhumiwa 172 kwa tuhuma za unyang’anyi na uharibifu wa mali, Dodoma 32 kwa uhaini, Kigoma 11, Iringa 89, Njombe 9, Arusha zaidi ya 60, Tabora 5, Bunda 29, Tarime 9 na Mafinga 45, hivyo jumla yao ni 641.
"Makosa haya kwa mujibu wa sheria zetu hayana dhamana, hivyo watuhumiwa wanashikiliwa gerezani wakati mashauri yao yakiendelea. Kwa mfano, wale wa Dar es Salaam wapo Gereza la Segerea," amesema Maduhu.
Ameongeza, mawakili wa TLS wataendelea kufuatilia na kutoa utetezi kwa vijana hao wakihakikisha kila hatua ya kisheria inafuatwa ipasavyo kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Wito wa Uwazi na Ushirikiano
Kwa upande wake, Paul Kisabo amesema TLS imepokea maombi kutoka kwa ndugu na familia mbalimbali kuhusu msaada wa kisheria kwa wapendwa wao, wakidai hawana uwezo wa kumudu gharama za mawakili.
"Tumewatembelea baadhi ya watuhumiwa na kuzungumza nao, wapo wenye changamoto za kiafya wanapaswa kupata huduma za afya, hivyo TLS itahakikisha wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria," amesema.
Aidha, ametoa wito kwa Jeshi la Polisi na Magereza kutoa taarifa na ushirikiano kwa jamii ili ndugu wa watuhumiwa wajue walipo wapendwa wao na kuwaona au kuwapatia mahitaji muhimu.
"Haki ya kuona ndugu yako anapokuwa chini ya uangalizi wa vyombo vya dola ni ya msingi, tunashauri mamlaka zitoe taarifa za wazi ili kuondoa mkanganyiko kwenye jamii watu wajue walipo ndugu zao," amesema Kisabo.
Wakili huyo ameongeza, taarifa sahihi na za uwazi kutoka Jeshi la Polisi kuhusu idadi ya watu wanaowashikilia na mahali walipo itasaidia kuondoa taharuki katika jamii kuhusu hali za ndugu zao hao ambao hawajui kama wapo hai au wameshafariki.
Kwa upande wake, Dickson Matata ametoa wito kwa vyombo vya habari kutimiza wajibu wake kwa kutafuta na kutoa taarifa sahihi ili kusaidia jamii kupata majibu ya maswali waliyonayo kwa kuzingatia kanuni za maadili.
Amesema TLS inafuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi zote na taarifa zinazohusu watuhumiwa, kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka kwa bila ubaguzi.
"Lengo letu si kupinga mamlaka, bali kusaidia kuhakikisha misingi ya haki inasimamiwa kwani hawa ni watuhumiwa, si wahalifu. Sheria inasema mtu huchukuliwa hana hatia hadi mahakama itakapothibitisha vinginevyo," amesema.
Aidha, mawakili hao wametoa wito kwa wadau na taasisi mbalimbali kutoa ushirikiano ili kuhakikisha vijana hao wanapata haki zao kwa mujibu wa kisheria bila ubaguzi.