Mauaji ya Muuguzi KCMC: Mahakama Yatoa Hukumu Kwa Mganga wa Jadi
Moshi – Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imekamilisha kusikiliza kesi ya mauaji ya muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck ambayo ilifanywa na mganga wa jadi, Omary Mahmoud Rang’ambo.
Katika ushahidi wake ulioutolewa mbele ya Jaji Safina Simfukwe, mtoto wa marehemu, Wende Mrema, alieleza namna mganga huyo alivyomwambia kuwa mizimu ilikuwa imefanikiwa kumsafirisha Patricia. Aliambiwa aingie katika chumba cha mama yake na kufanya usafi, ndipo alihisi harufu ya ubani.
Madai ya Pesa Milioni 25
Wende alieleza Mahakamani kuwa Omary alimtaka ampe fedha nyingine kama gharama za kumtibu mama yake ili aweze kuondoka Moshi. Omary alihitaji kati ya Shilingi milioni 20 na 25, hivyo Wende akalazimika kuuza shamba lake.
Alifanikiwa kupata mnunuzi aliyempa Shilingi milioni 10, ambayo alimpa Omary aliyeondoka asubuhi. Wende aliendelea kumsumbua Omary akitaka kufahamu mama yake anaendeleaje, lakini Omary alimhakikishia kuwa mama yake yuko salama na aendelee kumtafutia pesa.
Uongo kwa Viongozi wa Kijiji
Machi 2021, viongozi wa kijiji walimfuata Wende na kumuuliza mama yake yuko wapi. Aliwaambia yuko India kwa matibabu na aliwadanganya kwa kuwa Omary alimpiga marufuku kuwaeleza kuwa amechukuliwa na mizimu.
Kwa mujibu wa Wende, Omary alimwambia endapo angetoa siri hiyo, angekufa. Pia alimpiga marufuku kwenda eneo lile walilompeleka mama yake kwa kuwa kuna mizimu inamlinda.
Desemba 2021, maofisa wa polisi walimfuata na kumtaka awaeleze mahali alipo mama yake. Aliamua kusema ukweli ili maofisa hao wamsaidie mama yake. Aliwaeleza kuwa mganga mwenzake aitwaye Waziri anajua alipo Omary, ndipo akawapeleka polisi hadi Korogwe ambapo Waziri alikamatwa.
Ushahidi wa Viongozi na Madaktari
Shahidi wa nane, Mussa Liali aliyekuwa mwenyekiti wa Kijiji cha Rau, alieleza namna Machi 2022 alivyopokea taarifa za kutoweka kwa Patricia na alivyoshiriki katika mchakato wa kufukua mabaki ya mwili wa Patricia.
Kichwa Kilitenganishwa na Kiwiliwili
Dk Alex Mremi kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC alieleza namna alivyoshiriki katika kazi ya kufukua mwili wa Patricia. Shimo lilikuwa na urefu wa kama meta moja na ndani yake walikuta jambia, shuka ya kulalia na blanketi.
Jambia lilikuwa na nywele, matone ya damu na mchanga. Walikuta mabaki ya mwili wa mwanamke, mashuka na blanketi vyote vilikuwa na damu. Fuvu lilikuwa na alama ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Dk Mremi alibaini kiini cha kifo kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na kuchinjwa. Kichwa kilitenganishwa na kiwiliwili. Kupinda kwa mkono wa marehemu kunaashiria alikuwa akijitetea.
Shahidi wa 12, Stesheni Issa mwenye namba E.8872 aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alieleza namna walivyopata taarifa za kutoweka kwa Patricia, kupeleleza na kukamata mtuhumiwa mkuu.
Mganga Alivyojitetea Kortini
Katika utetezi wake, Omary alikanusha kutenda kosa la mauaji ya Patricia. Alisema ni mashtaka ya kutungwa yaliyochangiwa na kutoelewana kati yake na Wende baada ya kumfuma Wende akiwa na mwanamume mwingine.
Alidai walivunja mahusiano na Wende alianza kumfuatilia ili kurejesha uhusiano. Alipokataa kurudiana naye, Wende alimtishia kuwa atamfanyia kitu ambacho hatakaa akisahau maishani mwake.
Wakati akiulizwa maswali ya dodoso na wakili wa Serikali, Edith Msenga, alikiri kuwa majina ya Omary Mahmoud Rang’ambo yalikuwa ni miongoni mwa mambo ambayo hayakubishaniwa wakati wa usikilizwaji wa awali.
Uchambuzi wa Mahakama
Jaji Simfukwe alisema hoja kuu inayohitaji kuamuliwa ni kama upande wa mashitaka ulikuwa umeweza kuthibitisha shitaka pasipo kuacha shaka. Katika kesi iliyopo, mganga wa jadi anahusishwa na mauaji hayo kwa kuegemea vitu vitatu: kanuni ya yeye kuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, ushahidi wa mazingira na maelezo yake ya onyo.
Jaji alisema hakuna ubishi kwamba Patricia alikufa na kifo chake hakikuwa cha kawaida.
Jaji alieleza: "Ushahidi wa Wende unaelezea namna mshitakiwa alivyompa Patricia dawa za kienyeji na alipopoteza fahamu, mshitakiwa alimtaka amletee jembe na shoka. Alimtaka Wende ashirikiane naye kumbeba mama yake na kumpeleka nje ya nyumba."
"Inasikitishwa kwamba Wende alikuwa anamwamini sana mshitakiwa kama mganga wao wa jadi. Aliamini kila kitu alichoambiwa. Mshitakiwa alikuwa anawajibika kueleza aliachanaje na marehemu," alisema Jaji.