Watu 33,000 Wafariki Kwa Mwaka Kutokana na Moshi wa Kupikia Tanzania
Dar es Salaam. Kwa Tanzania watu takribani 33,000 hufariki dunia kwa mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua ambayo huchangiwa na uvutaji wa moshi unaotokana na matumizi ya nishati ya kupikia isiyosafi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba leo Ijumaa Septemba 12, 2025 wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Nishati Safi ya Kupikia 2025.
"Mama anaweza kuwa anapika na mtoto wake mgongoni au jirani yake anapika katika mazingira ya moshi kwa miaka mingi, ile athari ya moshi inaathiri miili yao taratibu. Kwa sababu ya athari hizo ndipo Serikali imekuja na mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa miaka kumi," amesema Mramba.
Kaulimbiu ya Mwaka: Okoa Maisha na Mazingira
Kaulimbiu ya mwaka huu ya "Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira" inalenga kusisitiza kuwa matumizi ya nishati hiyo si suala la kiteknolojia pekee, bali ni njia ya kuokoa maisha, kulinda afya na kuhifadhi mazingira.
Zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania bado hutegemea kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, hali inayosababisha madhara makubwa ya kiafya, kuongeza uharibifu wa mazingira na kudhoofisha uchumi.
"Hata hivyo, mabadiliko chanya yameanza kuonekana kupitia jitihada za pamoja kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo," imeelezwa kwenye kongamano hilo.
Serikali Yaelekeza Lengo la Mwaka 2034
Mhandisi Mramba amesema ni lazima elimu iendelee kutolewa kwa jamii na nguvu ya pamoja inahitajika ili watu waendelee kuhama kutoka kutumia nishati isiyosafi kuanza kutumia nishati safi.
Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
"Tanzania takriban asilimia 80 ya kaya zetu bado zinategemea nishati za jadi za kuni na mkaa na wote tutakubaliana idadi hiyo ni kubwa na kwa pamoja tunahitaji kufanya kitu kurekebisha hali hiyo," amesema Mramba.
"Hali hii inawaweka watu katika hatari ya kiafya kuchochea ukataji miti hovyo na mzigo mkubwa wa kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto."
Matumizi ya Nishati Isiyosafi Yanapungua
Matumizi ya nishati isiyosafi yanaenda yanapungua nchini huku nishati kama kuni na mkaa ikianza kuwa vigumu kupatikana ikilinganishwa na zamani.
Katibu Mkuu amesema upatikanaji wa kuni na mkaa kwa sasa ni changamoto kubwa ikilinganishwa na zamani, jambo linalofanya suala la kuhama kutoka kwenye nishati chafu kwenda safi kuwa muhimu zaidi.
"Kwa upande wa mijini hali inazidi kuwa ngumu zaidi, gharama ya kuni na mkaa inazidi kupaa, bei zinazidi kupanda na kuna sehemu bei hazihimiliki. Kwa vijijini wananchi wanatumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa na wanapoteza muda wao wa uzalishaji," amebainisha.
Vikwazo vya Matumizi ya Nishati Safi
Imeelezwa kuwa mahitaji ya gesi ya kupikia nchini Tanzania kwa mwezi ni futi za ujazo 30,000 huku uwezo wa Bandari katika kupokea gesi kwa sasa ni mdogo.
Mratibu wa Kitaifa wa Wanawake kwenye LPG, Winner Lukumay ameomba Serikali kuhakikisha inaendelea kuboresha bandari nchini ili kurahisisha uingizaji wa gesi ya kupikia jambo linaloweza kuchangia kushusha gharama za nishati hiyo.
Amesema hadi sasa bandari inaweza kupokea meli ya gesi yenye futi za ujazo 5,000 pekee kwa wakati mmoja wakati.
"Hii inamaanisha kuwa meli sita zinapaswa kuingia kwa mwezi ili kukidhi mahitaji kama nchi. Tukiboresha bandari hata gharama za usafirishaji ambazo zinaongeza gharama ya gesi kwa mlaji wa mwisho zitapungua," amesema.
Winners amesema changamoto nyingine ambayo bado inafifisha jitihada za matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kukosekana kwa elimu ya fedha.
"Huyu mamantilie yuko radhi anununue mkaa wa Sh3,000 kila siku, lakini je tuna mpango maalumu ambao utamuwezesha huyu mama kununua gesi kidogo kidogo," amesema.
Zanzibar Yaanza Kutoa Elimu Shuleni
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanza kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kuanzia shule za msingi ikiwa ni mkakati wa kuziba pengo la ukosefu ya elimu sahihi.
Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini, Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Said Mdungi amesema hatua hii itasaidia kujenga kizazi bora cha baadaye.
"Unapompa mtoto ujuzi atakwenda kushawishi nyumbani siku mzee wake akipata uwezo itakuwa ni rahisi kupata nishati safi ya kupikia. Mtoto huyu akikua na kuanza kujitegemea si rahisi kuchagua nishati za jadi bali ataendelea kutumia nishati safi ya kupikia," amesema.
Changamoto kwa Vijana
Uelewa, ushirikishwaji na gharama ya nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa vikwazo vinavyotajwa kuchangia vijana kutokutumia nishati safi ya kupikia.
Mtaalamu wa masuala ya jinsia kutoka TANGSEN, Gaudensia Malongo amesema: "Kuna vikwazo mbalimbali ambavo wanapata wanawake au vijana wadogo katika nishati safi ya kupikia. Moja ni suala la ushirikishwaji katika mipango ya kuhakikisha nishati safi inawafikia."
Amesema ili kuondokana na kikwazo hicho suala la ushirikishwaji linapaswa kupewa kipaumbele zaidi ili kupata mawazo yao kuhusu mkakati mzima.
"Suala la gharama nalo ni changamoto kwa vijana, wanahitaji kutumia nishati hiyo ila kwa uwezo wao wa kifedha ni ngumu kidogo. Hata uelewa bado ni mdogo jambo linawafanya wengi kuogopa kutumia nishati safi," ameongeza.
