Wakuu wa Mikoa Wahakikishia Usalama wa Wananchi Katika Uchaguzi Mkuu
Dar/Mikoani – Wakati Watanzania wakihesabu saa kwenda kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani, wakuu wa mikoa nchini wamewahakikishia usalama wananchi kwenye maeneo yao.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 29, 2025 ambapo Watanzania wenye sifa kote nchini watapiga kura kuchagua viongozi.
Mkoa wa Dar es Salaam Upo Tayari
Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila amesema kuna maneno yaliyopo mtaani kwamba uchaguzi utavurugika, amewataka wananchi kuyapuuza.
Amesema maandalizi ya uchaguzi katika Mkoa wa Dar es Salaam, wenye wapigakura takribani milioni nne, yamekamilika, hivyo amewataka wote wajitokeze kutumia haki hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
Amesema mkoa huo upo salama huku akibainisha kuwa maandalizi katika vituo vyote vya kupigia kura yamekamilika ikiwamo kubandikwa kwa majina ya wapigakura katika vituo.
"Nitoe rai kwa wote waliojiandikisha kwenda kuhakiki majina katika vituo mama walivyojiandikishia na kwenye vituo cha kupigia kura. Kituo ulichojiandikisha kinaweza kisiwe ndicho kituo cha kupigia kura, kama utakuwa umebadilishiwa, basi itakuwa ni karibu na kituo ulichotumia kujiandikishia awali," amesema.
Ameongeza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeongeza wigo wa vituo vya kupigia kura kwa sababu kujiandikisha kulikuwa siku nyingi zaidi, lakini kupiga kura ni siku moja ambao mchakato wake utaanza saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni.
Usalama Umeimarishwa
Amesema vyombo vya dola vimeapa kulinda usalama wa raia na mali zao, hivyo siku hiyo katika Jiji la Dar es Salaam hatakuwepo mtu atakayemtishia mwingine atakayekwenda kupiga kura na akaachwa afanye hivyo.
"Vyombo vya dola havijajipanga kutisha watu, bali vimejipanga kuhakikisha wewe Mtanzania na mwana Dar es Salaam unakwenda kupiga kura salama na unaondoka ukiwa salama," amesema Chalamila.
Ametoa maelekezo kwa wenyeviti wa Serikali ya mtaa kwa kusaidiana na uongozi wa mitaa yao na kushirikiana na sungusungu katika kulinda miundombinu yote ikiwamo ya Dawasa, Tanesco na miundombinu mingine katika maeneo yao.
Pia, ameelekeza barabara zote za mwendokasi zisitumiwe na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakizitumia kinyume cha utaratibu.
Shinyanga: Mazingira Rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro amesema watu wenye ulemavu wamewekewa mazingira rafiki ambayo hayatakuwa na changamoto kwao na kuhakikisha upigaji kura unakwenda vizuri.
Akizungumza katika ofisi yake iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, leo Oktoba 27, 2025, Mtatiro ameeleza kuwa hakutakuwa na changamoto yoyote kwa sababu tume ya uchaguzi imeandaa mazingira rafiki kwa wote.
"Watu wenye ulemavu kama wenye uoni hafifu, karatasi za nukta nundu zimeandaliwa na hawatahitaji kuingia na mtu kwenye chumba cha kupigia kura. Pia, wasiosikia wakalimani wa lugha za alama watakuwepo, hali ni shwari na usalama wa wananchi na mali zao ni wa hali ya juu," amesema Mtatiro.
Morogoro: Polisi Waonya Dhidi ya Uchochezi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya uchochezi, uharibifu wa miundombinu ya uchaguzi, maandamano yasiyoruhusiwa au matukio ya ghasia yatakayolenga kuvuruga uchaguzi.
Kamanda Mkama amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari akisema wanaendelea na majukumu yao kwa kufuata miongozo ya kisheria ikiwemo kufanya doria maalumu kwa ajili ya kuandaa mazingira salama kuelekea uchaguzi mkuu.
"Tunawaonya wale wote watakaotaka kufanya maandamano au kuzuia wananchi wema wasishiriki upigaji kura tutachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria," amesema Kamanda Mkama.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi wema hawapaswi kuogopa mwonekano wa vyombo vya ulinzi na usalama vinavyoendelea na doria huko mtaani vikiwa na askari, bali wavione kama fursa ya kutimiza jambo lao la kikatiba la kupiga kura kwa amani na utulivu.
Kilosa: Kamati ya Amani Iahimiza Ushiriki
Katika hatua nyingine, kamati ya amani Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imewataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki kupiga kura.
Kamati imesisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.
Katibu wa Kamati hiyo, Abdallah Mazingira amesema: "Kupiga kura ni wajibu wa kila raia na ni njia halali ya kushiriki katika ujenzi wa Taifa letu, kila kura ina thamani kubwa katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu, familia zetu na vizazi vijavyo."
Arusha: Vituo 1,051 Vimeandaliwa
Huko Arusha, Mkuu wa Wilaya hiyo, Joseph Mkude amewahakikishia wananchi wenye sifa za kupiga kura kuwa Serikali imejiandaa kikamilifu kuwawezesha kutimiza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Oktoba 27, 2025 amesema walifanya maandalizi katika maeneo matatu ambayo ni kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na kwamba hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuwa nzuri.
"Wilaya ya Arusha imejiandaa vizuri kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanashiriki kikamilifu kupiga kura siku ya uchaguzi ambayo ni Jumatano na imetangazwa itakua ni siku ya mapumziko nchi nzima," amesema Mkude.
Amesema katika kipindi chote cha kampeni Wilaya ya Arusha imeshuhudia utulivu kwa wagombea wa ngazi zote na hakujatokea matukio ya uvunjifu wa amani wakati vyama mbalimbali vikikaribia kufunga kampeni zao.
Kuhusu siku ya uchaguzi amesema kwenye mitaa 154 ya Jiji la Arusha vipo vituo 1,051 ambavyo vimewekwa kimkakati ili kuwawezesha wananchi kutembea umbali mfupi kwenda kupiga kura na kuendelea na majukumu mengine.
"Ukiangalia idadi ya vituo 1,051 ni vingi lakini lengo ni mwananchi asitembee umbali wa zaidi ya kilometa tatu kufuata kituo kilipo, pia ulinzi umeimarishwa kikamilifu maandamano pekee yanayoruhusiwa ni ya kwenda kupiga kura kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan na sio vinginevyo," amesema Mkude.