Viongozi wa Dini Pemba Wamemkumbusha Dk Hussein Mwinyi Kutekeleza Ahadi za Uchaguzi
Pemba. Viongozi wa dini Kisiwani Pemba wamemkumbusha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi kutekeleza ahadi alizotoa mwaka 2020 ambazo baadhi bado hazijakamilika, huku wakimweleza kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani bila umwagaji damu.
Katika mkutano wa Jumapili, Oktoba 5, 2025 mjini Utaani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dk Mwinyi amesisitiza kuwa ajenda kuu ya CCM ni kudumisha amani, mshikamano na umoja, jambo linalochangia maendeleo kuonekana kila kona ya Zanzibar.
“Pemba hii wakati wa uchaguzi uliopita hali haikuwa hivi. Hii ni neema kutoka kwa Mola wetu, tuendelee kuidumisha,” amesema Dk Mwinyi.
Akizungungumza kuhusu maendeleo, Mwinyi alisema kuwa miaka iliyopita Zanzibar ilikumbwa na ubaguzi mkubwa, lakini sasa umepungua kwa kiwango kikubwa. “Kwa sasa watu wanachaguana kwa kuzingatia utendaji kazi na siyo asili wala dini yao,” alisema.
Viongozi wa dini walipongeza hatua zilizofikiwa wakati wa uongozi wake, lakini wakasisitiza kuwa changamoto ziko bado. Sheikh Khamis Omar wa Micheweni alisema, “Mambo mengi umeyatekeleza lakini yapo ambayo hayajafanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa ikiwamo suala la ubaguzi, rushwa na unyang’anyi.”
Imamu Omar Ali Faki alishauri kuwa Wazanzibari wanahitaji amani wakati wa uchaguzi, akisema kuna maisha baada ya uchaguzi. “Hatutaki kuona watu wakipoteza maisha au kuumizwa kipindi hiki cha uchaguzi,” alisema.
Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisisitiza kuwa amani ni jukumu la kila mmoja. “Tusikiingize katika siasa. Tutangulize amani na tuwe mstari wa mbele kuihifadhi,” alisema.
Mkutano huu unaonyesha matarajio makubwa ya kudumisha amani na umoja katika Zanzibar, huku viongozi wa dini wakiwa na matumaini ya mabadiliko chanya.