HABARI KUBWA: Vijana 13 wa Tanzania Watengeneza Ndege ya Kwanza ya Taifa
Vijana 13 wa Kitanzania, wote wasomi wa fani za uhandisi na anga, wamefanikisha mradi wa kihistoria kwa kutengeneza ndege za kwanza zilizozalishwa nchini. Hivi sasa, Tanzania imeingia rekodi kama nchi ya kwanza Afrika yenye uwezo wa kutengeneza ndege zake mwenyewe.
Kampuni ya Airplanes Africa Limited (AAL) imezalisha ndege za aina ya Skyleader 500 na 600, ambazo zina uwezo wa kubeba abiria wawili na kusafiri kwa muda wa saa saba mfululizo. Ndege hizi zinatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, utalii, utafiti, ulinzi na usalama.
Mradi huu wa kibunifu unaonesha uwezo mkubwa wa vijana wa Tanzania katika sekta ya teknolojia na uhandisi. Hadi sasa, AAL imeshazalisha ndege tisa, ambazo tano zipo tayari kazini na nne zinaendelea kukabidhiwa.
Msimamizi wa ubora wa ndege, amesema kuwa malighafi zote za utengenezaji zilinunuliwa kutoka maeneo yaliyoidhinishwa kwa vifaa vya ndege kimataifa. Lengo kuu ni kuendeleza uzalishaji wa ndege zaidi ili kuimarisha uwezo wa sekta ya anga nchini.
Hatua hii ni ishara ya nguvu na ubunifu wa vijana wa Tanzania, na inatoa tumaini kubwa kwa taifa letu. Mradi huu unadhihirisha kwamba Tanzania ina uwezo wa kutengeneza teknolojia ya hali ya juu na kuimarisha uchumi wake.
Viongozi na wananchi wanakuhamasisha kushirikiana na kuendeleza ubunifu huu, ili kuwa na Tanzania yenye uchumi imara na taaluma za kisayansi.