Mapinduzi ya Zanzibar: Historia ya Miaka 62 ya Mgawanyiko
Wito mkuu ulioongoza Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea Januari 12, 1964, ulikuwa ni kuwaondoa Waarabu kwenye utawala, nyuma ya matamshi yaliyonadiwa ndani ya kampeni ya kumfukuza Sultan. Lengo lilikuwa ni kuwa Waarabu waachie madaraka ili Wazanzibari asilia wajitawale.
Changamoto kubwa ambayo imebaki kuwa urithi wa Mapinduzi ni tafsiri tofauti za historia hiyo. Wazanzibari wenye asili ya Pemba, tafsiri yao ya kiimani ni kuwa Unguja iliipindua Pemba. Wazanzibari wanaoifia zaidi Unguja, huamini Mapinduzi siyo tu yalilenga kumwondoa Sultan, bali pia kuikomboa Pemba kwenye makucha ya Waarabu.
Wazanzibari ambao uhafidhina wao unafungamana zaidi na Pemba, hutafsiri kwamba Mapinduzi yalikuwa mkakati wa Tanganyika kuitwaa Zanzibar, na kilele chake ni Aprili 26, 1964, ilipoundwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kabla ya kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mgawanyiko Unaoendelea
Changamoto hiyo ya kuwa na tafsiri tofauti ya Mapinduzi kutoka Unguja hadi Pemba, ndiyo zao la nongwa ya miaka 62, hisia za ubaguzi na kinachoonekana ni shuruti ya uzalendo na utii wa Mapinduzi tangu siku yalipofanyika. Mpaka leo, bado kuna makundi mawili ya Wazanzibari; wanaotamka ‘Mapinduzi Daima’ na wasiotamka. Halafu, kuna wanaotamka kinafiki.
Unguja, ndiyo hujinasibu kuwa wenye Mapinduzi na hutamka kwa sauti kubwa; ‘Mapinduzi Daima’. Pemba, wenaoitikia ‘daima’ kila linapotajwa neno ‘Mapinduzi’, huonekana wasaliti au wasio wazalendo kwa kisiwa chao. Wanamapinduzi daima, huwaona wasiotamka kuwa si Wazanzibari. Halafu, wale ambao ndimi zao ni muhali kusema ‘Mapinduzi Daima’, huwatafsiri Wanamapinduzi Daima kama walioiuza Zanzibar yao kwa Tanganyika.
Changamoto za Viongozi wa Awali
Ufahari wa Mapinduzi kwa upande mmoja wa Wazanzibari na ukakasi uliopo kwa wengine, chanzo chake ni waasisi wa Mapinduzi. Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, hakufanya ipasavyo kuwafanya Wazanzibari wote waelewe dhana nzima, sababu na msukumo wa kufanya Mapinduzi.
Sheikh Karume, baada ya kufanikisha maandamano, alijielekeza zaidi katika kujenga vitu kwa usawa baina ya Pemba na Unguja, ili kudhihirisha kuwa visiwa hivyo ni pacha. Bahati mbaya, hakuwekeza kwenye utoaji elimu kwa umma, vilevile kujenga uenezi wa makundi au kutoka mtu mmoja hadi mwingine kuhusu Mapinduzi, umuhimu na ulazima wake.
Jitihada za Usawa
Dhamira ya Karume ilikuwa njema, kuvifanya visiwa vyote viwili kupiga hatua za kimaendeleo kwa namna ya saresare. Hiyo ndiyo sababu ukifika Unguja utakutana na maghorofa marefu ya Michenzani, kisha ukiwa Pemba, utayaona majengo ya Mapinduzi, Kengeja, Madungu, Machomane, Wete, Micheweni na Konde.
Karume alipokuwa anajenga usawa Zanzibar, alitaka kila chenye kufanyika Unguja, kifanyike pia Pemba, kwa ukubwa na ubora sawa. Kipindi akiwa madarakani, aliwapangia naibu mawaziri wote waishi Pemba, kusudi kila kilichokuwa kinaamuliwa na Baraza la Mapinduzi, kitekelezwe ipasavyo Pemba chini ya usimamizi wa naibu mawaziri.
Mgawanyo wa ajira, Karume alitaka usawa, isipungue asilimia 60 kwa 40. Ikiwa ajira ni 100, basi Pemba waajiriwe kuanzia 40 kupanda juu.
Yalikuwa maono kuwa usawa wa huduma, miundombinu na vitu vingine vyenye kuonekana, ungeweza kuwafanya Wazanzibari kujiona ni kitu kimoja. Inasikitisha kuwa hilo halikufanikiwa. Bahati mbaya zaidi, imebaki kuwa hivyo kwa miaka yote 62.
Kesi ya Dk Salim Ahmed Salim
Miaka 62 imetimia, bado kukiwa na kumbukumbu kuwa moja ya zawadi bora zaidi kuwahi kuwa nayo kama Watanzania, Dk Salim Ahmed Salim, hakupewa fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu ya historia ya Mapinduzi. Kumbukumbu mbaya za Salim na urais wa Tanzania ni Uchaguzi Mkuu 1985 na 2005.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa anakaribia kukabidhi kijiti cha uongozi wa nchi mwaka 1985, alikusudia kumkabidhi Salim. Simulizi hii inathibitishwa na Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Spika wa Nne, Pius Msekwa.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi walimgomea Nyerere kumsimamisha Salim kuwa mgombea urais, wakati alikuwa Waziri Mkuu, huku Mwinyi, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, ndiye alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Mwinyi ameandika kuwa historia ya Mapinduzi ndiyo kikwazo kwa Salim. Hoja iliyopenyezwa ni kuwa Salim huwa hasemi ‘Mapinduzi Daima’. Zaidi, waliompinga wakadai Salim alihusika na mauaji ya Sheikh Karume, aliyeuawa Aprili 7, 1972.
Uzalendo wa Shuruti
Kwa nini Salim alinyimwa fursa kwa sababu eti hatamki ‘Mapinduzi Daima’, wakati kipindi ambacho NEC inasimama imara kumgomea Mwalimu Nyerere na mpango wake, ilikuwa imeshakatika miaka 21 tangu Mapinduzi yatokee? Inajenga uthibitisho ni kiasi gani Mapinduzi yametengeneza nongwa ya kihistoria.
Salim ni kielelezo kuwa Mapinduzi yamejenga ubaguzi wa kihistoria Zanzibar. Asili yake ni Mpemba, na kwa vile propaganda ilijengwa kumzunguka kwamba hasemi ‘Mapinduzi Daima’, kwa hiyo Wazanzibari wenye kutamka ‘Mapinduzi Daima’, kwa sauti kubwa, wakaona Salim siyo Mzanzibari kamili, hivyo hana uzalendo.
Hata Uchaguzi Mkuu Tanzania mwaka 2005, Salim alishughulikiwa kwa sababu ya Mapinduzi. Aliitwa Hizbu, kwa maana ya Mwarabu, ambaye ndiye hasa upande wa waliopinduliwa. Salim ni kielelezo cha wengi ambao wamejeruhiwa kwa sababu ya ubaguzi uliozaliwa na Mapinduzi.
Njia ya Mbele
Uzalendo haupaswi kuwa wa shuruti, bali utashi binafsi na kwa mahaba ya dhati. Wazanzibari wanatakiwa kuyapenda na kuyaenzi Mapinduzi kwa moyo wote, siyo kwa kushurutishwa au kutamka ‘Mapinduzi Daima’ kwa unafiki ili kutojizibia fursa. Itawezekana kama elimu itatolewa kikamilifu, kizazi kimoja baada ya kingine.
Muhimu, kufanya uwekezaji mkubwa katika kufuta mbegu ya ubaguzi ambayo huambukiza kizazi kimoja hadi kingine. Hata sura ya kisiasa Zanzibar, Pemba kuonekana kuwa ngome ya upinzani, wakati Unguja, CCM ikitamalaki, sababu ni historia ya Mapinduzi. Mbegu ya ubaguzi haikufutwa. Nongwa ikaachwa ishamiri.
Sheikh Karume alijitahidi kwa kuwekeza vitu, maono yake hayakusaidia. Marais sita waliofuata baada yake, hawajafanikiwa kuyafanya Mapinduzi kuwa fahari ya Wazanzibari wote. Pengine wa sasa, Dk Hussein Mwinyi, au mwingine baada yake atafanikiwa kuleta umoja kamili.