Serikali ya Niger, Nigeria Yaahidi Ulinzi wa Watoto Dhidi ya Utekaji wa Nyara
Nigeria. Serikali ya Jimbo la Niger nchini Nigeria imeahidi kuwalinda watoto dhidi ya matukio ya utekaji katika kipindi hiki kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na Mwaka Mpya.
Ahadi hii imetolewa Jumatatu Desemba 22, 2025 wakati serikali ya jimbo hilo ikiwapokea watoto na walimu 130 waliotekwa nyara na kuachiliwa huru baada ya kuwa mateka kwa muda wa mwezi mmoja.
Utekaji wao kutoka shule ya bweni ya Kikatoliki katika jamii ya Papiri, Jimbo la Niger, ni miongoni mwa matukio makubwa ya utekaji katika historia ya Nigeria.
Hakuna mtu au kundi lililodai kuhusika na tukio hilo hadi sasa, lakini wakazi wa eneo hilo wanayalaumu makundi yenye silaha yanayotafuta fidia.
Ongezeko la Matukio ya Utekaji Shuleni
Utekaji nyara shuleni umekuwa ishara ya ukosefu wa usalama katika nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. Sasa mamlaka zinasema zinaimarisha hatua za kiusalama.
Mratibu wa kitaifa katika Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Nigeria, Adamu Laka amesema wanatekeleza hatua za muda mfupi za ulinzi katika maeneo hatarishi dhidi ya watoto na jamii kwa ujumla.
Amesema wanakishirikiana na serikali za majimbo, viongozi wa kimila na wa kidini, ili kupata suluhisho la kudumu kwa ajili ya usalama.
"Elimu haipaswi kuathiriwa na vurugu. Tutaendelea kufuata sera na operesheni zitakazorejesha imani, kufungua tena shule kwa usalama na kuhakikisha kuwa haki ya kila mtoto wa Nigeria ya kupata elimu katika mazingira salama inalindwa," amesema.
Swali la Fidia Linabaki Bila Jibu
Hata hivyo, maafisa wa serikali hawajaweka wazi iwapo walilipa fedha zilizoombwa na watekaji au la ili kuachiwa watoto hao.
"Sidhani kama ni haki sana kwa mfumo au kwa serikali kuulizwa kama pesa zilitumika au la. Jambo la muhimu zaidi ni kwamba tumewarejesha watu hawa bila madhara," alisema Gavana wa Jimbo la Niger, Mohammed Umar Bago.
"Mambo mengine ni yetu sisi, si yenu. Kwa hiyo jambo la muhimu zaidi ni kwamba tumewapata watoto waliopotea, na namna tulivyofanya hivyo, sisi tunaijua."
Shule hiyo ilisema watoto wengi waliotekwa nyara walikuwa na umri kati ya miaka 10 na 17. Watoto hao sasa wataungana na familia zao kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.