Hofu Yaenea Kariakoo Baada ya Ubomoaji wa Kuta na Barabara
Dar es Salaam – Wakazi na wafanyabiashara wa mitaa ya Swahili na Donge, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, wanaishi kwa hofu kutokana na ubomoaji wa kuta za nyumba na sehemu ya barabara uliofanyika usiku wa kuamkia Desemba 6, 2024, bila makubaliano wala kibali cha mamlaka husika.
Tukio hilo, lililofanywa na mmoja wa majirani, limesababisha uharibifu wa miundombinu ya majitaka, nyufa katika majengo jirani, hasara za kibiashara na kuibua hofu ya kuhatarisha maisha ya wananchi, hususan katika eneo lenye msongamano wa watu.
Hofu imeanza miongoni mwa wananchi wa mtaa huo, huku wakiwa na kumbukumbu ya tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika mtaa wa Mchikichi, Novemba 16, 2024, lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na majeruhi zaidi ya 80.
Ubomoaji Ulifanyika Bila Taarifa Rasmi
Shekha Viamungu, mtoto wa mmiliki wa jengo la ghorofa tano lililoathirika, amesema ubomoaji huo ulifanyika bila taarifa rasmi, licha ya familia yao kusisitiza umuhimu wa makubaliano na kuzingatia usalama.
"Tulikuwa tayari kukaa chini na kufikia muafaka, lakini bila makubaliano, fensi ilivunjwa usiku, jambo lililosababisha nyufa kwenye jengo na kutulazimu kuhama kwa hofu ya usalama," amesema.
Amesema juhudi za kupata zuio la polisi hazikufanikiwa, huku Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikitoa amri ya kusitisha ujenzi Desemba 11, 2024, ambayo anadai haikuheshimiwa.
Makubaliano Yagonga Mwamba
Kwa mujibu wa Shekha, awali walipendekeza kukaa chini na mpangaji pamoja na wahusika wote ili kupata suluhu ya pamoja, ikiwemo kumpa mpangaji fremu ili aendelee na maisha bila kuathiriwa.
"Tulifika hatua ya kusema kama kuna hatari kutokana na ubomoaji kwa mmoja wa wapangaji wetu, atafutiwe fremu ili aendelee na biashara zake, kuliko kumtoa hapo halafu wasijue anakwenda wapi, lakini walikataa," amesema.
Amesema mjenzi wa eneo hilo amedai mpangaji alitaka pesa nyingi ambazo yeye hawezi kutimiza, hali iliyozidisha mvutano na kufanya pande hizo kushindwa kufikia muafaka, huku ikiibuka hoja ya kuzidisha mpaka wa eneo.
Kutokana na utata huo familia hiyo ilipendekeza kufufua mipaka rasmi kwa kuwaita wataalamu wa upimaji ardhi ili kuthibitisha kama kweli wamezidi eneo.
"Tulisema kama tumekosea au tumezidi hata kidogo, tuko tayari kuachia. Eneo linalodaiwa ni dogo na halina faida ya kuleta mgogoro mkubwa namna hiyo," amesema.
Wafanyabiashara Wapata Hasara
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Khalfan Masoud, amesema amepata hasara na anaishi kwa hofu baada ya ukuta wa eneo analofanyia biashara kubomolewa, tukio lililosababisha bidhaa zake kubaki wazi nje bila ulinzi.
"Wakati wanabomoa sikuwapo, nimesikia watu wamekuja kubomoa na kuacha stoo ikiwa wazi, mizigo iko nje, na hatua hiyo inaweka mazingira ya kuibiwa, huku jengo lenyewe likiwa katika mazingira yanayoweza kusababisha ajali," amesema Masoud.
Barabara na Majitaka Yameathirika
Athari nyingine za ubomoaji wa fensi na ujenzi huo ni kuathiriwa kwa mfumo wa majitaka pamoja na barabara ya mtaa wa Donge, ambayo imepasuka na kusababisha kuwekwa bati kuzuia madhara zaidi.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Ilala, John Magori, amesema watakagua ujenzi huo na endapo kutabainika uharibifu wowote, watachukua hatua za kisheria.
"Sina taarifa kuhusu uharibifu wa barabara ya mtaa wa Donge na Swahili, lakini kwa kuwa umeniuliza hapa, nitaomba nifuatilie kesho asubuhi, nikaangalie uharibifu uliofanyika, kisha tutachukua hatua na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria," amesema Magori.
DAWASA Inatoa Ufafanuzi
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa ufafanuzi kuhusu tukio la kuporomoka kwa chemba ya taka katika eneo la Kariakoo, ikieleza kuwa chanzo chake ni shughuli za uchimbaji wa msingi wa jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa karibu na miundombinu hiyo.
Msimamizi wa DAWASA eneo la Kariakoo, Joseph Tillya, amesema chemba zilizopo eneo hilo ni fupi na baadhi yake hupitisha maji taka kutoka maeneo mbalimbali.
"Chemba zetu hapa ni fupi, kuna iliyopo pembeni ambayo hupitisha majitaka kutoka Hoteli ya Cate na nyumba nyingine. Wakati wa kuchimba kwenda chini kwa ajili ya ujenzi, waligusa miundombinu yetu na kusababisha chemba ishuke," amesema Tillya.
Serikali ya Mtaa Haikushirikishwa
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnanzi Mmoja, Baraghashi Azimio, amesema ofisi yake haikushirikishwa kikamilifu katika hatua za awali za ujenzi wa jengo lililosababisha mgogoro wa ubomoaji wa ukuta na uharibifu wa miundombinu ya majitaka na barabara katika eneo hilo.
"Hatupingi maendeleo, tunachotaka ni taratibu zifuatwe na wananchi walindwe. Serikali ya mtaa iko tayari kushirikiana na kila upande," amesema Azimio.
Sheria Zinakataza Ujenzi Bila Kibali
Kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, Kifungu cha 31, kinakataza mtu yeyote kufanya ujenzi, ubomoaji au mabadiliko ya miundombinu bila kibali cha mamlaka husika.
Kwa upande wa usalama, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2004 inamtaka mwajiri au mkandarasi kuhakikisha mazingira ya kazi ni salama kwa wafanyakazi na jamii inayozunguka eneo la kazi.
Mkandarasi Atarekebisha Uharibifu
Mkandarasi wa jengo hilo, Khamis Mkude, amesema hitilafu zilizojitokeza wanazifanyia kazi kwa kujenga upya ukuta wa zege, na wameanza maandalizi ya kurejesha eneo lililoathirika, ikiwemo chemba ya maji taka na kipande cha barabara.
"Tumerekebisha sehemu iliyoharibika kwenye mfumo wa majitaka kwa kurejesha mabomba. Hatua inayofuata ni kujenga tena retaining wall ili kuimarisha eneo lote lililoharibika," amesema Mkude.
Jiji Linafanya Uchunguzi
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Jiji la Dar es Salaam, Maduhu Ilanga, amesema ofisi yake ilichukua hatua baada ya kupokea taarifa za awali kuhusu tukio hilo, kwa kuelekeza wahandisi kufanya tathmini ya kitaalamu.
Ameeleza kuwa ujenzi wa aina hiyo katika eneo lenye msongamano mkubwa wa watu na majengo kama Kariakoo hauwezi kuchukuliwa kirahisi, kwani unaweza kuhatarisha usalama wa majengo jirani pamoja na maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wake, jiji linaendelea kufanya uhakiki ili kubaini kama taratibu zote za kisheria zilifuatwa, ikiwemo suala la vibali vya ujenzi, huku nyaraka husika zikiendelea kufanyiwa uchunguzi.