Rais Samia: JWTZ Lisikubali Kuchafuliwa na Siasa
Dar es Salaam – Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, amelitaka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutokubali kuchafuliwa wala kumuacha au kumlinda mtu yeyote mwenye cheo kikubwa au kidogo kukigeuza chombo hicho kuwa cha mashinikizo ya siasa.
Rais Samia amesema jeshi ni chombo tofauti na siasa, iwe Mwana-CCM, Mwana-Chadema au chama kingine katika Serikali, JWTZ litabaki kwa ajili ya kulinda nchi na wananchi wake.
Alieleza hayo jana Jumatatu, Desemba 15, 2025 akifungua mkutano wa tisa wa Mkuu wa Jeshi (CDF) na makamanda uliofanyika katika Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga (SKUA), mkoani Tanga.
"Kwa hiyo siasa na chombo (jeshi) hiki ni tofauti, ulinzi imara ndio msingi wa maendeleo na amani ya nchi yetu. Kauli mbiu hii, inaakisi ukweli kwamba hakuna maendeleo bila amani," amesema Rais Samia.
"Sasa jeshi la wananchi likiwa chombo muhimu cha ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi, linategemewa kuendeleza usalama na amani ili wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo," ameeleza Rais Samia.
Kutokana na hilo, Mkuu huyo wa nchi, ameitaka JWTZ kuitumia kauli mbiu ya ‘ulinzi imara ndio msingi wa maendeleo na amani ya nchi yetu’ kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
Mchango wa Wanawake Katika Jeshi
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema wanawake wanaendelea kuthibitisha uwezo katika maeneo mbalimbali ya kijeshi, ikiwemo fani za urubani, uhandisi na udaktari.
"Kwa muda mrefu jeshi letu, limeendelea kuwa la mfano katika ukanda wa Afrika na duniani, kutokana na weledi, nidhamu na utii. Ili kuendelea kuwa jeshi imara na mfano, muhimu kuwekeza kwenye mafunzo na mazoezi yanayoendeana na matishio ya kisasa na matumizi ya teknolojia mpya," amesema.
"Sambamba na kuwekeza katika mafunzo ya kisasa na mazoezi, ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ni muhimu katika kudhibiti matisho ya kiusalama yakiwemo ya ugaidi," ameeleza Rais Samia.