Rais Mwinyi Afanya Uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Manaibu Katibu Wakuu
Unguja – Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amefanya teuzi tano muhimu za viongozi wa serikali, zikiwemo wakuu wa mikoa watatu na manaibu katibu wakuu wawili.
Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Zena Ahmed Said, ametangaza kwamba wateule wote wataapishwa Jumatano Desemba 17, 2025, saa 8:00 mchana, Ikulu Zanzibar.
Wakuu Wapya wa Mikoa
Moh’d Ali Abdallah ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini. Moh’d anachukua nafasi ya Idrisa Kitwana ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi Maalumu vya SMZ.
Cassian Gallos Nyimbo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja. Gallos anachukua nafasi ya Mattar Zahor Mattar ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar.
Mgeni Khatib Yahya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Pemba. Mgeni amechukua nafasi ya Salama Mabrouk Khatib ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji.
Manaibu Katibu Wakuu
Hawwah Ibrahim Mbaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Ubunifu. Kabla ya uteuzi huo, Hawwah alikuwa Naibu Katibu Mkuu iliyokuwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar.
Dk Said Seif Mzee ameteuliwa tena kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.