Mjaribu wa Ndoa: Hadithi ya Jozi Iliyojuta Kuachana
Canada. Kisa cha jozi moja kinaweza kuwa funzo kwa ndoa nyingi. Mke na mume walikuwa na ugomvi usiokwisha hadi kila mmoja akifikiria kuachana na mwenziwe kutokana na kuchoshwa na ugomvi.
Katika harakati za kutaka kuokoa ndoa yao, wahusika walituamini na kututembelea ili tuwape ushauri. Walikuwa wakweli kwetu katika kuelezea kadhia yao. Mume alikuwa na tabia ya kumfokea mkewe. Mkewe naye hakukubali. Alikuwa akijibu mapigo. Kwa ufupi, wote walikuwa wanafokeana kutegemea nani alianzisha ugomvi. Katika kuwasikiliza kwa umakini, tuligundua kuwa walikuwa wakitafuta mchawi wa ndoa yao bila kujua kuwa wao ndiyo walikuwa wachawi.
Kwa mfano, tuliwauliza kama hawawezi kuamua kwa makusudi kubadili tabia kwa kuacha kufokeana tena mbele ya watoto. Katika kujitetea, kila mmoja alisema kuwa anadhani wamechokana. Baada ya kusema hivyo, tuliwapa usemi maarufu usemao kuwa wakati unasema huyu ni wa nini, wapo wanaosema huyu nitampata lini. Tuliwaasa kuwa kila mtu ana thamani pamoja na upungufu wake. Tumeonya mara nyingi kuwa hakuna malaika duniani. Kila binadamu ana ubora na udhaifu wake. Huu ndiyo ubinadamu ambao wote tunao; tuwe tumefanikiwa au kutofanikiwa vipi katika ndoa au maisha.
Uamuzi wa Kuachana
Tuligundua kitu kimoja. Wanapokuja wanandoa wakiwa wameshaamua kuachana, mjue, walishaachana muda mrefu. Kinachokuwa kimebakia ni kumalizia kwa kutengana au kupeana talaka.
Na hii ndiyo maana wanandoa wengi wanapoombwa ushauri juu ya uamuzi wa kuachana kwa wenzao huwa wanasita kusema "si muachane tu" kwa vile wanajua wanapotamka hivyo, ujue washaaamua. Hivyo, wanaoombwa ushauri huogopa kulaumiwa kwa kitu ambacho wahusika wameshaamua. Kama walivyokuwa wamedhamiria, walikuja kwetu kumalizia kuvunja ndoa yao. Walipeana talaka na kila mmoja akashika hamsini zake wasijue kuwa binadamu tunajua tutokako siyo tuendako. Baada ya kuvunja ndoa, kila mmoja alijiaminisha kuwa angempata mwenye kumfaa, wasijue kuwa usichojua ni usiku wa kiza! Ngoma ilikuja kunoga baada ya kila mmoja kumpata aliyedhani angemfaa. Kimsingi, walitumia uadui, ugomvi, na hasira zao kufanya uamuzi ambao baadaye wangeujutia maisha.
Wahenga walituasa kuwa hasira ni hasara. Hivyo, ushauri wetu wa kwanza ni kwamba usifanye uamuzi ukiwa na hasira au chuki. Wahusika walikaa kitambo wakisaka watakaowafaa bila kujichunguza kama wao wanafaa na hilo ndilo jibu sahihi. Kuokoa muda na nafasi, mume alimpata mke ambaye walianza kwa mapenzi motomoto kila mmoja akitajitahidi kuonyesha kuwa angeziba pengo la mwenzake. Hata hivyo, baada ya muda, tabia mbaya zao ambazo ni kama ugonjwa zilianza kujitokeza. Mume alianza kujutia moyoni kwa vile alimpata mtu mwenye balaa!
Majuto ni Mjukuu
Wahenga wanaasa kuwa majuto ni mjukuu. Jamaa alianza kujuta na kujiona kama alikuwa amemuogopa mjusi na kuishia kifuani mwa chatu au mamba. Maji yakishamwagika hayazoleki. Ameshaingia mkenge. Kwa upande wa mke, alimpata mume mwenye kiburi, katili, na mpigaji. Mume mpya hakuwa na muda wa kufoka zaidi ya kutembeza vipigo kila mara. Mama alianza kujuta na kujilaumu kwa nini alikuwa ametoka kwenye kufokewa na kuishia kwenye vipigo. Wahenga walionya. Waweza kuruka mkojo ukaishia kuyakanyaga mavi.
Hapa, funzo ni kwamba kila binadamu ana ubora na kasoro. Hali hii ni ngumu na hatarishi kuliko ya mwanzo kwa wote. Walifikia kwenye hatua ngumu sana. Kwenda mbele au kurudi nyuma, havikuwa jibu tena. Je, katika hali kama hii, kama ungekuwa wewe, ungefanya nini? Wahenga wanatuasa kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Tiba waliyotafuta wahusika iligeuka gonjwa tena donda.
Ushauri kwa Wanandoa
Kwa kuzingatia kisa hiki ambacho kinaakisi ndoa nyingi, tunashauri wanandoa wajenge mazingira na tabia vya kuheshimiana na kuishi kwa amani. Maana, duniani tunaishi mara moja hata kama mtu anaweza kuoa au kuolewa tena. Je, hili ndilo jibu sahihi? Kwa wale ambao hayajawakuta haya, hata kama mna ugomvi, jifunze kitu. Kwanza, mjue. Ndoa ni kama bahari. Huwa haiishi wala kukosa mawimbi.
Pili, mjue kuwa unaweza kumkimbia mjusi ukaishia kifuani mwa chatu au mamba. Tatu, wanandoa waepuke kuchukiana, kudharauliana, kufokeana, kutukana na mengine kama hayo. Nne, wajue kuwa binadamu wote ni sawa. Hivyo, unayedhani ni bora anao udhaifu wake na unayemuona dhaifu, anao ubora wake. Tano, kwenye ndoa, ni wanandoa kutegemeana na si kupanga kuwa huru au kuachana. Si jibu, kwani, wakati mwingine, unalodhani ni jibu, laweza kuwa tatizo.
Mwisho, tunashauri wanandoa wakae wajidurusu na kudurusu matatizo yao na siyo kukurupuka kufanya uamuzi wa kuachana wasijue wanaweza kujikuta wamewakimbia mijusi wakaishia vifuani mwa mamba. Hakuna mja mkamilifu na mwanzo wa unachodhani ni suluhisho kinaweza kuwa mwanzo wa matatizo makubwa kupita yale uliyoyatafutia suluhu ya haraka na kukurupuka. Heri kuendelea kuishi na mjusi uliyemzoea kuliko mamba ambaye si rahisi kuzoeleka kwa vile hatakupa muda wa kuishi na kumzoea.