Nairobi Yapitisha Maazimio 11 ya Kulinda Mazingira Duniani
Nairobi. Maazimio 11, maamzi matatu na tamko moja la mawaziri yanayolenga kuimarisha ustahimilivu wa dunia, yamepitishwa katika mkutano wa mazingira huko Nairobi.
Maazimio hayo ya kikao cha saba cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEA-7) yalihitimishwa Desemba 12, 2025 na mataifa wanachama, wakati Marekani ikipinga ajenda hizo, kwa madai kuwa maamuzi hayo yamepoteza mwelekeo.
Mkutano huo wa siku tano umeshuhudia viongozi wa kimataifa, watunga sera, wanasayansi na wadau wengine wa mazingira zaidi ya 6,000 kutoka kwenye nchi 186 duniani, wakijadili changamoto mbalimbali za kimazingira kwenye mkutano uliokuwa na kaulimbiu ya kutafuta suluhu endelevu kwa ustahimilivu wa dunia.
Maazimio Yaliyopitishwa
Rais wa UNEA-7, Abdullah Bin Ali Al-Amri, amesema hoja zilizopitishwa ni pamoja na usimamizi salama wa kemikali na taka na kuimarisha mwitikio wa kimataifa katika usimamizi wa majanga ya moto.
Nyingine ni kuongeza ufanisi wa rasilimali zilizopo kupitia uratibu na ushirikiano katika mikataba ya kimataifa ya mazingira na utekelezaji wake na kuhakikisha mifumo salama, yenye uwajibikaji na endelevu ya akili mnemba (AI).
"Kuimarisha mwitikio wa kimataifa dhidi ya wimbi kubwa la uongezekaji magugu baharini aina ya sargassum na kuendeleza ushiriki wenye maana wa watoto na vijana katika utawala wa mazingira," alisema.
Hoja nyingine ni usimamizi salama wa mazingira wa madini na metali, pamoja na mwongozo wa mzunguko endelevu wa rasilimali za madini, na usimamizi wa mfuko wa amana na michango iliyotengwa kwa matumizi maalum.
Hoja Zilizoshindwa Kupitishwa
Kwa mujibu wa hati ya hoja 15 zilizojadiliwa, baadhi ya hoja ambazo hazijapitishwa ni pamoja na kuimarisha mwitikio wa kimataifa kukabiliana na uhalifu unaoathiri mazingira, na kuharakisha hatua za kimataifa kuimarisha ustahimilivu wa miamba ya matumbawe dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Hali ya Hewa na Mazingira wa Norway, Andreas Bjelland Eriksen, alitaja sababu za hoja hizo kutopitishwa kuwa ni muda mchache wa kuzijadili na kuzipitisha.
Alisema hoja nyingi zinashindwa kupitishwa kutokana na wadau kutokubaliana tafsiri ya baadhi ya maneno yanayotumika kwenye hoja hizo, kwani jambo moja linaweza kuwa na maana nyingine kwenye maeneo tofauti.
Al-Amri alisema kupinga hoja ni haki ya wanachama na hivyo suala la Marekani kujitoa linaheshimiwa.
"Sio wote tuliokubaliana katika kila hoja, hata zilizopita zilihitaji majadiliano na marekebisho zaidi mpaka zikafanikiwa," alifafanua na kusema hata ambazo hazikupita zilihitaji mjadala zaidi na zimehamishwa kwa wakati mwingine.
Tanzania Yaunga Mkono Maazimio
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Festo Dugange aliunga mkono hoja zote zilizojadiliwa ikitia mkazo kwenye hoja ya kuendeleza ushiriki wenye maana wa watoto na vijana katika utawala wa mazingira.
"Tunashauri wadau kutekeleza maazimio haya kwenye nchi zao, pia ushirikishwaji wa vijana kama nguzo muhimu ya kulinda mazingira," alisema.
Aliongeza kuwa, "kama nchi tunaahidi kutekeleza maazimio haya na tutashirikiana na wadau wote katika hili."
Marekani Yajiondoa Katika Maazimio
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wawakilishi wa Marekani, nchi hiyo imeamua kujiondoa katika mazungumzo ya maazimio yote ya UNEA-7.
"Marekani haiwezi kuunga mkono kazi inayopoteza mwelekeo kutoka katika wajibu wa msingi wa UNEA. Kila mwaka tumekuwa tukisisitiza kuwa idadi ya maazimio ipunguzwe na izingatie tu masuala yaliyo wazi ndani ya uwezo," nchi hiyo imeeleza.
Marekani imesisitiza kuwa vikao vinaendelea kurudia hoja zisizo na masilahi ya mazingira na kuwa maandiko ya UNEA yamejaa marejeo ya zamani, lugha tata, na mapendekezo yanayoongeza majukumu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) bila ufadhili.
Itakumbuka kuwa kuanzia Januari 2026, Marekani itakuwa imejitoa rasmi kwenye mkataba wa Paris ambao ndio mwongozo mkuu kwa dunia kwenye mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.
Januari 20, 2025 Rais wa nchi hiyo, Donald Trump alisema mkataba wa Paris hauitendei haki Marekani na unadhoofisha uchumi.