Naibu Waziri Ole Millya Atangaza Vita Dhidi ya Viongozi Wanaouza Ardhi Simanjiro
Simanjiro – Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, ametangaza kiama kwa viongozi wa vijiji wenye tamaa ya kuuza ardhi.
Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro ameeleza kwamba hawatishi wala kuwaogopesha viongozi wenye tamaa ya kuuza ardhi ya vijiji, ila atahakikisha anapambana na wabadhirifu hao.
Akizungumza kwenye sherehe ya misa ya Diwani wa Kata ya Komolo, Saning’o Somi, ya kumshukuru Mungu na kuomba baraka za uongozi, amesema siku za wauza ardhi Simanjiro zinahesabika.
"Siwatishi ila nitakula sahani moja na wala ardhi Simanjiro ambao baadhi ya viongozi walikuwa wanafiki, kwani midomoni wanapinga uuzaji ila marafiki zao ni wauza ardhi," amesema Ole Millya.
Ameeleza kuwa siku zote za maisha yake atapinga uuzaji wa ardhi holela, akiwa mbunge au asiwe mbunge, kwani ni kilio kikubwa kwa watu wanyonge ambao wanategemea ardhi kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.
Naibu Waziri amesema baadhi ya wenye tamaa ya kuuza ardhi huwa wanaopatiwa maeneo ikiwemo ekari 10, anauza kisha anaenda kupewa eneo jingine na kuuza tena.
Viongozi Wamtakia Kila la Heri Diwani Mpya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, amesema kwa mara ya kwanza Wilaya ya Simanjiro imepata kiongozi wa serikali katika ngazi ya Naibu Waziri, hivyo wanashukuru.
Padri Edwin Kiromo wa Kanisa Katoliki Misheni ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Terrat amemtakia kila la heri Somi kwa kupeleka furaha kwa watu wa Kata ya Komolo.
"Tusiwe na hila wala upendeleo kwani hata Mfalme Suleiman hakuomba mali wala ng’ombe, aliomba hekima akapewa na mali juu. Hivyo tembea na Mungu katika uongozi wako," amesema Padri Kiromo.
Mchungaji Agustino Laizer amemweleza Somi kuwa kiti alichokalia siyo cha starehe wala cha raha, ni kiti cha kutatua matatizo na changamoto za watu wa Kata ya Komolo.