Miradi ya Afya kwa Wanawake na Watoto Afrika Yaendelea Kusaidia Ustawi wa Watoto Tanzania
Dar es Salaam. Miradi ya afya kwa wanawake na watoto barani Afrika iliyoasisiwa na Profesa Peng Liyuan, ambaye ni mke wa Rais Xi Jinping wa China, imeendeleza ustawi wa afya za watoto na kufikia ndoto zao nchini.
Miradi hiyo ilizinduliwa na Profesa Peng mwaka 2023, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Wanawake Viongozi wa Afrika, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani, inayoadhimishwa Juni Mosi kila mwaka.
Akizungumza wakati wa sherehe ya kuadhimisha mwaka wa pili wa mpango wa afya kwa watoto unaofanyika kwa siku mbili Desemba 13 na 14 jijini Dar es Salaam, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesisitiza umuhimu wa msaada wa China katika sekta ya afya na ustawi wa watoto nchini Tanzania.
Msaada wa Afya kwa Watoto Wanyonge
Amesema Profesa Peng amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza miradi ya afya kwa wanawake na watoto barani Afrika.
Balozi Chen amesema watoto si tu mustakabali wa taifa, bali pia ni daraja hai linalokuza urafiki na ushirikiano wa karibu kati ya China na Tanzania.
Mpango huu unalenga kutoa huduma za afya kwa watoto wanyonge, kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kutokana na ukosefu wa huduma za matibabu.
"Miaka miwili iliyopita tulikusanyika hapa kuanzisha mpango huu. Leo tunafurahi kuona watoto hawa wakiendelea kukua wakiwa na afya njema, nguvu, na matumaini," amesema Balozi Chen.
Jitihada za Kulea Watoto Yatima
Balozi Chen pia amepongeza juhudi za Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Zaida, Zaida Hassan na wafanyakazi wake kwa kujitolea kwenye kituo chao kusaidia ustawi wa watoto kufikia ndoto zao.
Kwa mujibu wa Balozi Chen, Tanzania imekuwa mshiriki muhimu katika mpango huu, ikipokea msaada wa chakula, dawa, na vifaa vya kielimu, huku ikinufaika na huduma za madaktari wa China walioko hapa.
"Kuwaona watoto hawa wakiendelea kukua wakiwa na kujiamini kunanifanya nijisikie furaha kubwa. Watoto hawa pia ni ishara ya urafiki wa kudumu kati ya China na Tanzania," amesema Balozi Chen.
Huduma za Madaktari na Dawa
Ameongeza kuwa China imetuma dawa, chakula, na timu ya madaktari, wakiwemo wataalamu wa pediatrics, macho, moyo, na ngozi, wamefanya vipimo vya kina na kutoa mwongozo kwa wafanyakazi kuhusu kinga na ustawi wa watoto.
Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na China amesema timu ya kwanza ya madaktari ilifika Zanzibar mwaka 1964, na Tanzania Bara kuanzia 1968. Hadi sasa, timu 35 zimehudumia Zanzibar na 27 Bara, zikitibu wagonjwa takribani milioni mbili.
Lengo la Kituo cha Kulea Watoto
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo, Zaida Hassan amesema kujitolea kwao ni huruma katika kuwahudumia watoto wa Kitanzania katika kutimiza ndoto zao.
Amesema lengo lao ni kuhakikisha watoto hao wanapata fursa ya kustawi kimaisha, kisaikolojia na kiafya, hali inayowasaidia kufuata ndoto zao bila vizuizi vya ukosefu wa rasilimali au changamoto za maisha.
Hassan amesema wanatambua kuwa kila jitihada ya kuwahudumia watoto, kwa malezi, elimu, lishe na huduma za afya, inachangia katika kujenga mustakabali thabiti kwa kila mtoto.
Dhamira ya Timu ya Madaktari
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya madaktari hao, Dk Bao Zengtao, amesema mpango huu ni alama ya urafiki na uwajibikaji wa pamoja kati ya nchi hizo mbili.
"Dhamira yetu ni kutibu magonjwa, kulinda maisha, na kusaidia ukuaji wa kiafya. Watoto ni mustakabali wa familia, jamii, na taifa," amesema.
Mshauri wa ubalozi wa China nchini, Chu Kun, ambaye alitembelea kituo cha Ashura Orphanage Foundation kilichopo Vingunguti, Dar es Salaam, amesisitiza yatima ni sehemu muhimu ya mustakabali wa jamii.
"Kusaidia afya, elimu, na ustawi wa watoto hawa ni jukumu letu sote. Kupitia chakula, dawa, na vifaa vya kielimu, tunaleta faraja, furaha, na fursa," amesema.