Madiwani wa Bariadi Waapishwa, Waonywa Kuhusu Uadilifu na Matumizi Mabaya ya Madaraka
Bariadi – Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wameapishwa rasmi wakati wakinolewa kuhusu umuhimu wa uadilifu, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuepuka mgongano wa masilahi na matumizi mabaya ya madaraka.
Amasha Bura, Ofisa Maadili kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ametoa onyo hilo wakati wa kuapisha madiwani hao Jumatano Desemba 10, 2025.
Amesema madiwani wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na viapo vyao ili kuwaletea wananchi maendeleo wanaostahili.
Onyo Kali Kuhusu Zabuni na Kandarasi
Bura ameeleza kuwa wapo baadhi ya madiwani wamekuwa wakifanya biashara na halmashauri kwa kuchukua zabuni na kandarasi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
"Madiwani msijihusishe na zabuni au kandarasi ndani ya halmashauri. Ukipata mradi na ukaufanya chini ya kiwango, tutafanyaje utambuzi wa uwajibikaji wenu? Lazima tuwe mfano katika uadilifu," amesisitiza.
Ofisa huyo amesema viongozi wa ngazi hiyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika matumizi sahihi ya rasilimali za umma, uwazi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kupunguza uaminifu wa wananchi.
Wito wa Ushirikiano na Ufuatiliaji wa Miradi
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amewataka madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano, kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, kufuatilia na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo kupitia kamati zao.
"Tunawahitaji kuwa daraba kati ya halmashauri na wananchi. Simamieni miradi ikamilike kwa ubora na kwa wakati, kwa sababu wananchi wanawaamini," amesema Simalenga.
Uchaguzi wa Viongozi Wapya
Sambamba na hayo, Nkenyenge Charles amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo baada ya kupata kura 14 za Ndiyo, huku Zawadi Mkilila akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kura 14 za Ndiyo.
Matarajio ya Wananchi
Neema Magesa, mkazi wa Nyakabindi, amesema ni vizuri madiwani wakajikita katika kusimamia miradi ya afya na maji ambayo inawagusa kila siku kwenye maisha yao.
"Tunataka madiwani wapya waangalie afya na maji. Miradi mingi imeahirishwa bila maelezo, tunahitaji kuona mabadiliko sasa," ameeleza Magesa.
Kwa upande wake, John Malosha, mfanyabiashara katika Soko la Bariadi, ameonyesha matumaini ya kuona mazingira bora ya biashara.
"Kero za ushuru na tozo zisizoeleweka ziangaliwe. Tukipata viongozi wakuongea na wananchi, mambo yatakwenda vizuri," amesema Malosha.
Baraza hilo jipya linatarajiwa kuleta msukumo mpya katika ustawi wa mji wa Bariadi, huku wananchi wakisubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa ahadi za viongozi wao katika kipindi kijacho.