Vijana Wahimizwa Kuenzi Mapambano ya Uhuru wa Tanzania
Wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 64 ya uhuru wa Tanganyika (baadaye Tanzania), Desemba 9, mwaka huu, vijana wametakiwa kuenzi harakati za mapambano ya uhuru na kutovuruga maendeleo yaliyopiganiwa na waasisi wa taifa hili.
Wamehimizwa kufikiria na kuchukua hatua za kuendeleza yale yaliyojengwa na waasisi wa taifa hili, kuhakikisha nchi inafikia hatua mpya za maendeleo na ustawi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
TNC imefanya mahojiano maalumu na mwalimu mstaafu, Jotham Chagwa (82), mkazi wa Lugulu, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, akisimulia mapito ambayo vijana wa zamani walipitia katika mapambano ya uhuru.
Hali ya Utawala wa Kikoloni
Mwalimu Chagwa anasema wakati taifa hili likiwa mikononi mwa wakoloni, wananchi hawakupenda kuongozwa kwa amri, badala yake walitaka kufanya uamuzi wao wenyewe badala ya kufanyiwa na wageni.
"Japo wakoloni walifanya mambo mengi mazuri, watu hawakuridhika na kutawaliwa, kufanyiwa kila kitu kwa amri ya wazungu, badala ya kujifanyia wenyewe. Hata maofisa wote waliokuwa serikalini walikuwa wazungu," anasema.
Anasema wakati huo, akipatikana Mtanganyika aliyesoma, ilikuwa ni lazima apewe cheo cha chini. Kulikuwa na namna ya kudharauliwa na wakoloni, wananchi hawakupenda kutawaliwa na wazungu, badala yake walitaka uhuru ili wapange mambo yao wenyewe.
Furaha Baada ya Uhuru
"Baada ya kupata uhuru, watu walifurahia sana, waliwapenda viongozi wao. Nakumbuka Mwalimu Julius Nyerere pamoja na viongozi wengine walipendwa kutokana na kutuletea uhuru wa Tanganyika, hivyo waliwapenda, kuwaheshimu na walifanya nao kazi bega kwa bega kuliko walivyokuwepo wakoloni," anasema Mwalimu Chagwa.
Anaongeza kuwa baada ya uhuru hakukuwa na wataalamu wengi, hivyo Nyerere alitumia busara kubaki na wazungu wachache na kuwashirikisha kwenye uongozi wake. Baada ya kusomesha wataalamu nje ya nchi na kupata maarifa, baadaye waliwaondoa wazungu.
"Mwalimu Nyerere alijitahidi kusomesha vijana wengi ili wapatikane wenye uwezo na aliwapeleka nje za nchi kusoma. Walipopatikana wenye uwezo na wasomi, akapunguza wale wazungu na kuwaweka wazawa wasomi kwenye nafasi zao," anasema Mwalimu Chagwa.
Anasema enzi hizo vijana wengi walipelekwa nje za nchi kusoma, mpaka wakapatikana vijana wengi walioweza kusaidia shughuli za Serikali na kuingia kwenye mfumo rasmi wa utumishi wa umma.
Maendeleo Baada ya Uhuru
"Wananchi wengi hawakuridhika na maendeleo yaliyokuwepo, japo wazungu walikuwa wamejitahidi kwa kiwango chao, lakini hawakufikia kiwango cha kuwaridhisha wananchi kufurahia maendeleo yao. Kipindi kile hata barabara hazikuwepo, shule zilikuwa chache," anasema.
Baada ya uhuru, anasema Mwalimu Nyerere alijitahidi kuongeza shule sehemu mbalimbali nchini pamoja na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Mwalimu Chagwa anasisitiza kuwa taifa hili limejengwa kwa jasho la watu wengi, hivyo ni muhimu vijana wakaenzi juhudi za waasisi badala ya kurudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana kwa gharama kubwa.
"Vijana, tuyaenzi kwa heshima yale yaliyopatikana kwa jasho la waasisi wetu. Kujaribu kuvuruga maendeleo ni kurudisha nyuma kile kilichopatikana kwa miaka mingi," anasema Mwalimu Chagwa.
Anaongeza kuwa: "Hatuwezi kuvuruga maendeleo haya; bali tuna jukumu la kuyajenga zaidi."
"Vijana mnatakiwa mjue huko tulikotoka hali ilikuwa mbaya sana. Viongozi na wazazi wetu walijitahidi kutufikisha tulikofika kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo tunayoyaona leo, hivyo tusifanye kitu chochote kinachoweza kuharibu yale maendeleo yaliyopambaniwa na wazee wetu baada ya kumwondoa mkoloni," anasema.
Ujitolevu wa Wananchi
Chagwa anasema baada ya kupata uhuru, Mwalimu Nyerere aliwashawishi watu wafanye shughuli zao wenyewe na walifanya kwa moyo mweupe, hivyo maendeleo yalipatikana kwa haraka.
Anasema shule za msingi na sekondari zilijengwa, hususani katika Mkoa wa Tanga ambako kulikuwa na sekondari moja tu ya wakoloni (Tanga School), shule za msingi na sekondari ziliendelea kuongezeka tofauti na zile zilizokuwepo kabla ya uhuru.
"Watu walijiamulia mambo yao wenyewe, kukawa na serikali za vijiji, hivyo walijitahidi kufanya mambo yao wenyewe na kujitolea pale ambapo Serikali haijaleta fedha za kutosha, walikuwa na moyo wa kujitoa.
"Kwa hiyo, shule na barabara nyingi zilichimbwa kwa mikono ya wananchi, maana Nyerere aliwahimiza wapende nchi yao na wafanye maendeleo yao wenyewe bila kutegemea misaada ya nje kwa asilimia 100," anasema Mwalimu Chagwa.
Anasema baada ya kupata uhuru, watu walichakarika kufanya shughuli zao kwa bidii, kujenga shule na hospitali. Wananchi walijitahidi kufanya hivyo kwa mikono yao wenyewe, ndiyo maana maendeleo yalipatikana kwa haraka, maana Serikali isingeweza kupata fedha za kuleta maendeleo kujenga shule nchi nzima.
Matunda ya Uhuru
Mzee Chagwa anasema maendeleo yanaonekana kwa sasa kwenye uboreshaji wa miundo ya barabara, shule, vituo vya afya, maboresho kwenye sekta ya maji—yote haya ni matunda ya uhuru.
"Kila unachokiona sasa ni matunda ya uhuru. Sasa hivi kuna majumba makubwa yamejengwa na maeneo mengi zamani yalikuwa mapori, nyumba watu walikuwa wakiezeka kwa majani na makuti na nchi nzima ilikuwa ni hivyo. Kuona mtu amejenga nyumba ya bati kipindi kile ilikuwa nadra sana," anasema Mwalimu Chagwa.
"Hivyo, baada ya uhuru, mambo yalibadilika sana. Watu waliendelea kuwa na maendeleo mbalimbali ya kiuchumi, walijenga nyumba nzuri za kisasa pamoja na maendeleo mengine makubwa. Miaka 64 ya uhuru, tumepiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
"Wazee wetu leo hii wangeamka wakaona maendeleo ya sasa hivi, wangeshangaa sana kukuta kila mahali majumba mazuri ya ghorofa, barabara za lami, vitu vingi vimefanyika ni kwa vile tu wengi hawajui huko nyuma kulikuwaje," anasema.
"Hata kama tuna maendeleo makubwa, watu bado wanahitaji zaidi na zaidi. Maendeleo ni makubwa, sasa hivi ukienda vijijini unakuta kuna shule nyingi, vituo vya afya, barabara. Enzi hizo kabla ya uhuru hapakuwa navyo. Hivyo Nyerere alijitahidi kujenga shule za msingi na sekondari," anasema.
Ujumbe kwa Vijana
Mwalimu Chagwa anawataka vijana kuenzi, kuheshimu, kutunza na kutovuruga maendeleo yaliyopambaniwa na taifa hili kwa jasho kubwa.
"Vijana, tuyaenzi kwa kuwaheshimu na tusikubali kuvuruga haya maendeleo tuliyonayo. Zaidi, tunaweza kuongeza zaidi maendeleo, tusivuruge yale yaliyotengenezwa na wazazi wetu. Hatupaswi kurudisha nyuma maendeleo tuliyosotea kwa miaka mingi," anasema Mwalimu Chagwa.
Anasema inatakiwa vijana wajue kwamba taifa lilikotoka hali ilikuwa mbaya na wazazi wetu walijitahidi kulifikisha lilikofika kwa kufanya mambo mengi ya maendeleo yanayoonekana leo. Hivyo, anawasihi vijana wasifanye kitu chochote kinachoweza kuharibu maendeleo.
Nasaha kwa Viongozi
Kwa upande wa viongozi, anasema: "Viongozi wanapaswa kujua wananchi wanahitaji nini, ili waweze kuwasaidia. Lakini kuweka mshikamano mzuri kati ya viongozi na wananchi, kusiwe na matengano kati ya viongozi na wananchi.
"Vijana pia tusiwatenge, maana ndio waleta maendeleo ya kesho. Tujaribu kwenda nao kujua wanataka nini. Serikali ibuni vitu ambavyo vitasaidia vijana wapate kazi za kujitegemea, hata kama si za kuajiriwa. Tusiwatenge vijana katika shughuli yoyote, maana ndio taifa la kesho."