Watanzania Waadhimisha Uhuru Majumbani Kutokana na Usalama
DAR ES SALAAM – Watanzania mwaka huu wamesherehekea maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika wakiwa majumbani pamoja na familia zao, hali ambayo ni tofauti na desturi ya wengi kutumia siku hiyo kupumzika kwenye maeneo ya burudani au kushiriki matukio ya hadharani.
Mabadiliko hayo yalichochewa na taarifa za uwezekano wa maandamano yasiyo na ukomo tarehe hiyo, baada ya maandamano ya Oktoba 29 wakati wa uchaguzi yaliyosababisha vurugu, ambapo watu walipoteza maisha, wengine kujeruhiwa na mali za umma na binafsi kuharibiwa.
Serikali ilitoa agizo la kuwataka wananchi wote wasio na dharura kusalia nyumbani ili kuhakikisha usalama wa umma. Salamu za heri kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, zilizowasilishwa na Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, ziliwahimiza Watanzania kutumia siku ya Uhuru kwa kukaa nyumbani na familia zao.
Tangazo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwamba watu wanaolazimika kutoka nje wabebe vitambulisho na wawe tayari kuulizwa maswali ya uthibitisho, liliongeza umakini na kuwafanya wengi wachague kubaki majumbani. Uwepo wa askari polisi na wanajeshi katika baadhi ya mitaa uliongeza hisia za tahadhari.
Changamoto za Usafiri
Hata hivyo, kwa wale waliolazimika kusafiri kutokana na dharura, hali haikuwa rahisi. Usafiri wa umma ulipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na watoa huduma wengi kutii agizo la Serikali, jambo lililowaadhiri watu waliolazimika kwenda hospitali, kazini au kwenye shughuli muhimu.
Upungufu huo ulisababisha baadhi ya madereva wa bajaji na bodaboda kupandisha nauli mara dufu, jambo lililoleta malalamiko kutoka kwa wananchi waliokuwa na dharura.
Hali Nchini
Dar es Salaam: Eneo la Kariakoo makutano ya Barabara ya Lumumba na Mtaa wa Mkunguni kuelekea Barabara ya Bibititi kukiwa hakuna wafanyabiashara wala watu wanaopita asubuhi ya Jumanne Desemba 9, 2025. Mlimani City ambalo limezoeleka kuwa na pilikapilika za magari na watembea kwa miguu liliwa kimya kabisa.
Moshi: Hali ya utulivu imetawala Manispaa ya Moshi, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa katika eneo la Soko la Mbuyuni. Kwa kawaida mji wa Moshi huwa na pilikapilika nyingi, lakini mitaa iliyozoeleka kuwa na shughuli za kibiashara imeonekana kuwa katika ukimya.
Kibaha: Mtaa wa Loliondo Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani maduka mengi hayakufunguliwa tangu saa kumi na mbili asubuhi hadi saa nne, eneo ambalo kwa kawaida wananchi hufurika kupata mahitaji muhimu.
Mbeya: Hali ya utulivu imetanda katika maeneo ya Soweto, ambapo saa 5:00 asubuhi baadhi ya maduka yamefungwa. Jana Desemba 8, soko hilo lilishuhudia umati wa wananchi wakifanya ununuzi. Huduma ya usafiri ukiwamo bajaji na daladala imekuwa changamoto, huku bodaboda wakionekana kwa nadra.
Mfanyabiashara Suleiman Hashim amesema wananchi walinunua mahitaji siku nyingi kabla ya tarehe 9, hivyo ameamua kufunga biashara. Barabara ya Sam Nujoma pia imeshuhudia utulivu mkubwa.
Segerea: Wafanyabiashara na wasafirishaji wamefunga maduka na kusimamisha huduma za usafiri. Kituo cha Mabasi cha Segerea Mwisho hakikuonekana na mfanyabiashara wala gari la usafiri.
Tandale na Magomeni: Maeneo haya ambayo kwa kawaida yana hekaheka nyingi yamekuwa tulivu. Kuanzia Magomeni Usalama, Kota hadi Tanesco, hakuna maduka wala huduma nyingine zilizofunguliwa. Ukimya umetawala kiasi cha kufananisha mazingira na siku ya msiba.
Abdulrahman Maulid amesema wananchi wametii maelekezo ya Serikali, na wengi walikuwa wamejiandaa mapema kwa kununua mahitaji muhimu. "Safari hii sijaona mtu anayeangaika kutafuta mahitaji, kwa sababu maandalizi yalishafanyika. Kingine mtandao upo, tofauti na Oktoba 29," alisema.
Hata hivyo, baadhi ya maduka yamefunguliwa kwa muda mfupi kutoa huduma kisha kufungwa, huku watu wachache wakionekana mitaani.