Serikali Yapiga Marufuku Matumizi ya Maji ya Mto Ruvu kwa Shughuli Zisizo za Kibinadamu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amepiga marufuku matumizi ya maji yanayotoka Mto Ruvu kwa shughuli nyingine zisizo za kibinadamu, akisisitiza kuwa kwa sasa maji hayo yatatumika kwa matumizi ya binadamu pekee hadi hali ya upatikanaji itakapokuwa sawa baada ya mvua kunyesha.
Aidha, ameiagiza mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kuhakikisha maji yanayopatikana yanagawiwa kwa usawa bila upendeleo wowote.
Aweso ametoa maagizo hayo leo Jumapili, Desemba 7, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na mtambo wa uzalishaji maji Ruvu chini, wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani. Ziara hiyo imefanyika kufuatia upungufu wa maji unaoendelea kushuhudiwa kutokana na kupungua kwa kiwango cha maji katika Mto Ruvu, hali inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa joto na kuchelewa kwa mvua.
Marufuku Kwa Shughuli za Kibiashara
Katika maelekezo yake, Waziri Aweso amesema ni marufuku kuendelea na shughuli nyingine zinazotumia maji ya Ruvu ikiwemo shughuli za kibiashara na matumizi makubwa yasiyo ya lazima, huku akisisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza ni matumizi ya binadamu. Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni ya muda ili kuwalinda wananchi dhidi ya athari kubwa zaidi za uhaba wa maji.
Amesema pamoja na kupungua kwa uzalishaji wa maji, bado kuna maeneo yanaendelea kupata huduma, akitolea mifano ya maeneo ya Kimara, Ubungo, Mabwepande hadi Mbweni. Hata hivyo, amewataka wananchi kutumia maji kwa uangalifu mkubwa na kuyahifadhi pale yanapopatikana.
"Hiki ni kipindi cha mpito, hali itarejea kuwa nzuri, lakini kwa sasa nchi nzima tuna wajibu wa kulinda matumizi ya maji kwa binadamu," amesema Aweso.
Visima Kuunganishwa Katika Mfumo wa Dawasa
Aweso pia ameagiza visima vyote vilivyochimbwa na Serikali kuunganishwa katika mfumo wa Dawasa ili kuongeza upatikanaji wa maji. Amehimiza ushirikiano kati ya taasisi binafsi na mashirika ya dini yanayomiliki visima ili kusaidiana katika kuhakikisha wananchi hawakosi maji, huku akitahadharisha dhidi ya matumizi holela ya rasilimali hiyo adimu.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema ofisi yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa marufuku hiyo na kuhakikisha maji yanayopatikana yanamfikia kila mwananchi kwa usawa. Ameonya kuwa hawataruhusu watoa huduma binafsi kutumia changamoto ya maji kama fursa ya ulanguzi au kuuza maji kwa bei kubwa.
Dawasa Iko Tayari Kutekeleza Maagizo
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Dawasa, Romanus Mwang’ingo, amesema mamlaka imepokea maelekezo ya waziri na iko tayari kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maji yaliyopo yanatumika ipasavyo kwa matumizi ya binadamu, huku marufuku ya matumizi mengine ikizingatiwa kikamilifu.