Mjadala Wahenga: Kizazi Kipya Watofautisha Maana ya Misemo ya Wahenga
Dar es Salaam – Katika siku za hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii kumeibuka mjadala kuhusu misemo mbalimbali ya wahenga.
Mjadala huo unatokana na namna ambavyo kizazi cha sasa maarufu Gen-Z kinavyotafsiri misemo hiyo ya wahenga kwa maana tofauti na iliyokusudiwa na wazee.
Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la pili, mhenga ni mtu mwenye hekima na busara ambaye aghalabu huwa na umri mkubwa.
Misemo hiyo inajumuisha nahau, methali na semi mbalimbali ambazo zimekuwa zikitumika kuonya, kufundisha, kuhamasisha na kuchochea bidii ya kazi na kutoa mwelekeo kwa jamii kuhusu mambo kadhaa.
Mfano wa misemo hiyo ni mshika mawili moja humponyoka, haba na haba hujaza kibaba, haraka haraka haina Baraka na mtegemea cha ndugu hufa maskini.
Badru Salum (80), mkazi wa jijini Dar es Salaam, anasema misemo hiyo ambayo kizazi cha sasa inaitaja kama ya wahenga imebeba historia, malezi na mafunzo ambayo yameongoza jamii kwa vizazi vingi.
"Kinachofanywa na vijana wa sasa kubadili maana au kuigeuza kuwa utani kunapunguza thamani ya busara iliyokusudiwa," amesema.
Mdau wa Kiswahili, Uswege Hobokela, amesema hiyo inatokana na baadhi ya vijana kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu maana halisi na busara iliyo ndani ya misemo hiyo.
Amesema misemo hiyo awali ilikuwa ikitumiwa na jamii kuelimisha, kuburudisha na kuonya, huku maana halisi pamoja na busara iliyopo katika baadhi ya misemo, nahau au methali ikiwa haipo bayana.
"Kwa mfano wanaposema mchumia juani hulia kivulini, ililenga kumpa moyo mtu anayepambana kutafuta maisha ipo siku atapata mafanikio na siyo kwamba mtu achukue kitu katika mazingira yenye jua kisha alie kivulini kama ambavyo inaelezwa na kizazi cha sasa huko kwenye mitandao ya kijamii," amesema.
Mdau mwingine wa Kiswahili, Dk Ernest Haonga, amesema wanachokifanya kizazi cha sasa ni kuhakiki kazi ya sanaa katika jamii.
"Siyo wanadhihaki bali wanahakiki kile kilichokuwa kimewekwa katika jamii kupata uhalali wake," amesema.
Amesema vijana hao wa sasa wanafanya majaribio ya kile kilichosemwa na wazee wa zamani kama kina uhalisia na wakati uliopo pamoja na matukio wanayokutana nayo katika jamii.
"Lugha ni kwa ajili ya jamii, hivyo inaruhusiwa kuibananga katika namna inayowawezesha kuwasiliana ila inapokuwa katika mfumo rasmi kufanya hivyo ni kosa," amesema na kuongeza:
"Mfano mwalimu anafundisha darasani na kusema akili ni nywele huwezi sema hata wenye vipara wana akili, hapana. Kufanya hivyo siyo sahihi kutokana na muktadha," amesema.
Amos John, mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam anasema ni wazi kuwa baadhi ya nahau, methali na semi za kale haziendani na nyakati zilizopo sasa.
Amesema hiyo ndiyo inasababisha baadhi ya vijana kuhoji uhalisia na uhalali wake kupitia majukwaa mbalimbali ya kijamii.
"Vijana wengi wa sasa hawakubali tu vitu bila ya kuhoji na ndiyo maana hata katika misemo mbalimbali ya Kiswahili wanataka kuona uhalisia wake katika maisha halisi," amesema.
Siwema Ngaya, mkazi wa Magomeni, jijini Dar es Salaam anasema kinachofanywa na vijana ni sehemu ya burudani na siyo kama hawajui maana au umuhimu wa misemo hiyo ya wahenga.
"Ni sehemu tu ya burudani haina maana kuwa tunadharau kile kilichosemwa na wahenga," amesema.