Vijana wa Kiwira Wakemea Uvunjifu wa Amani, Wamsihi Polisi Kumwachia Huru Diwani Mstaafu
Mbeya – Vijana wa Kata ya Kiwira wilayani Rungwe wamekemea vitendo vya uvunjifu wa amani, huku wakiliomba Jeshi la Polisi kumuachia huru aliyekuwa diwani wa Kata hiyo, Simon Kiraiti na kumpa heshima maalumu ya mtumishi mstaafu.
Wakizungumza leo Desemba 7, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya udereva kwa waendesha pikipiki ‘bodaboda’ wamemshukuru Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge kwa kutekeleza ahadi hiyo kwa bodaboda na kuwaunganisha kuwa pamoja.
Msemaji wa vijana wa kata hiyo, Furaha Mwakyusa, amesema wanakemea na kulaani matukio yote ya uvunjifu wa amani, akifafanua kuwa umoja wa vijana katika kata hiyo umeazimia kulinda na kutetea amani katika eneo hilo, bila kuendeshwa kwa itikadi za kisiasa.
Amesema kuwa pamoja na maazimio hayo, wanaliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kumuachia huru diwani mstaafu, Simon, ambaye anadaiwa kuchukuliwa siku tatu zilizopita, na wanataka apewe heshima ya mtumishi mstaafu, huku wakisisitiza kuwa hawajui kilichomkumba.
"Hatukubaliani na uvunjifu wa amani, hata yanayoendelea mitandaoni kuhusu Desemba 9, sisi vijana wa Kiwira tumeazimia kulinda maeneo yetu kuhakikisha hakutokei maandamano, tunajua kuandamana ni haki kikatiba ila kuna taratibu na sheria zake, tukitaka kufanya hivyo tutaomba kibali Jeshi la Polisi," amesema Mwakyusa.
"Tunashukuru kwa kututhamini, tunaomba diwani wetu mstaafu aliyeshikiliwa na Polisi kwa kuwa vijana wa hapa wana uthibitisho umuachie huru kwa sababu hatujui ameshikwa kwa sababu gani zaidi ya tetesi tu," ameongeza.
Kamanda wa Polisi Aahidi Kuchunguza
Akijibu sakata hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga amesema hakuwa na taarifa hizo mapema akiomba kufuatilia kuanzia ngazi za wilaya na mkoa akiahidi majibu kutolewa mapema, akibainisha kuwa jukumu la Jeshi la Polisi ni kukamata, kuchunguza na kupeleleza kubaini ukweli.
Amewataka vijana hao kutumia mafunzo hayo kwa faida yao ili kujiletea kipato akifafanua kuwa vurugu haziwezi kuleta maendeleo, akiwaomba kudumisha amani kwa kuwa Serikali imeanza kutekeleza ahadi zake kuhakikisha vijana wanajiinua kiuchumi.
"Naomba nisiwe msemaji kwenye hili kwa kuwa sikupata taarifa mapema, nitalifanyia kazi, Jeshi la Polisi jukumu letu ni kukamata, kuchunguza na kupeleleza kama ni kweli, lakini tumieni mafunzo haya kwa faida yenu ili kuondokana na changamoto za barabarani," amesema Kuzaga.
Mafunzo ya Bodaboda Yafunguliwa
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, Notker Kilewa, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kundi hilo ili kuongeza ufanisi wa kazi yao na kuzuia changamoto zinazoweza kutokea wanaposhughulika na mamlaka barabarani.
"Serikali imeweka mazingira mazuri, kumbukeni awali gharama za leseni kwa pikipiki na bajaji ilikuwa Sh70,000, lakini sasa ni Sh30,000, hivyo mnaweza kunufaika na mabadiliko haya, pia hii ni fursa ya kuomba mikopo," amesema Kilewa.
Naye Mratibu wa Mafunzo ya Muda Mfupi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), Rajabu Ghuliku, amesema mafunzo hayo yanaweza kuwahusisha pia madereva wa vyombo vingine vya moto, akifafanua kuwa wameamua kuhamia rasmi Kiwira kutoa elimu kwa kundi hilo.
Serikali Inatekeleza Ahadi
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Mbeya Mjini na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, diwani wa kata hiyo, Christopher Mwangomango, amesema kuwa Serikali tayari imeanza kutekeleza ahadi zake kupitia ilani ya CCM.
Amesema kuwa mafunzo hayo yametokana na ahadi iliyotolewa na Mwalunenge alipokutana na kundi hilo, ambapo aliahidi mambo mbalimbali ikiwemo mfuko wa fedha kwa makundi tofauti, yakiwemo mama lishe, wajasiriamali, bodaboda na machinga.
Mwangomango ameweka wazi kuwa lengo kuu ni kuwawekea mazingira mazuri Bodaboda na makundi mengine kufanya kazi zao kikamilifu na kwa usahihi.
"Aliahidi pikipiki tano na Sh3 milioni, ambazo tayari tumekabidhi. Sasa tunaomba vijana muwe watulivu, kwani Serikali inaendelea kutekeleza mahitaji yenu. Tuweke mkono pamoja ili kufanikisha malengo ya pamoja, na tumieni mafunzo haya kujiendeleza kiuchumi," amesema Mwangomango.