Masoko Nchini Yashuhudia Msongamano wa Wanunuzi, Bei za Vyakula Zinapanda
Dar es Salaam. Masoko kadhaa nchini yameanza kushuhudia msongamano wa wanunuzi wa vyakula na bidhaa muhimu kufuatia hofu ya uwezekano wa kutangazwa marufuku ya kutembea kwa muda fulani kuelekea Desemba 9 mwaka huu.
Mbali na ongezeko la ununuzi wa mahitaji ya msingi kama vyakula, TNC imeshuhudia kupanda kwa bei za bidhaa za chakula katika baadhi ya maeneo nchini.
Kwa mara ya kwanza, Oktoba 29 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitangaza marufuku ya kutembea kuanzia saa 12:00 jioni baada ya kujitokeza ghasia, maandamano na uharibifu wa mali katika maeneo kadhaa nchini.
Marufuku hiyo iliyodumu kwa siku sita katika miji kadhaa nchini, ilisababisha bei za bidhaa muhimu kupanda huku ikiwa na matokeo hasi kwa kaya nyingi hasa zile zisizo hifadhi vyakula ndani, uhaba wa bidhaa, kupanda kwa bei ya vyakula, mafuta na bidhaa muhimu.
Mfano, kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, kilo moja ya nyama ilipanda bei kutoka kati ya Sh10,000 hadi Sh11,000 hadi kati ya Sh19,000 na Sh20,000.
Kufuatia hilo katika miji kadhaa wananchi mbalimbali wameonekana katika masoko na maduka ya bidhaa za jumla wakinunua kwa wingi vyakula vya nafaka na vile visivyoharibika ikiwamo mchele, unga, tambi na nyinginezo.
Mchambuzi wa Uchumi Atoa Maoni
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa uchumi, Profesa Haji Semboja amesema kawaida Desemba ni mwezi ambao wengi huwa mapumziko, lakini kwa sasa inachangia na hali iliyojitokeza hivi karibuni.
"Kile kipindi cha Oktoba 29 hata uwe na fedha vitu hakuna na palipokuwa na vitu walinunua kwa bei ya juu, kuna soko ambalo mahitaji yanaongezeka kwa haraka na makubwa kwahiyo ni kawaida duniani kote kwenye soko kuongeza bei," amesema.
Profesa Semboja amesema hali hiyo imesababishwa na Serikali, mpaka sasa kutoweka bayana mikakati ili kuwahakikishia watu wote kwamba, wale waleta vurugu na wanaohamasisha mitandaoni hawatafanya kama ilivyokuwa awali.
"Watanzania ni watu wa amani, si watu wa fujo. Hiki kinachoonekana wananchi wanaonesha hisia zao kwamba wahalifu watafanya tena, kinachotokea sasa ni mwitikio wa uhitaji na ndiyo maana bei inapanda," amesema.
Hali Mwanza
Wakazi wa Mwanza wanaendelea kununua kwa wingi mahitaji ya chakula, huku bei zikipanda.
Kwa sasa, kilo moja ya mchele inauzwa kati ya Sh2,500 na Sh3,200, ikilinganishwa na Sh2,200 hadi Sh2,500 hapo awali.
Mahindi nayo yameongezeka kutoka Sh20,000 hadi Sh25,000 kwa debe, huku maharagwe yakiuzwa Sh2,200 kutoka Sh1,800 kwa kilo.
"Juzi nilipita hapa dukani kununua mchele ‘super’ kilo moja Sh3,000 lakini leo nimeukuta Sh3,200 bila shaka kesho utakuwa juu zaidi," amesema Hellena Julius mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza.
Muuzaji wa vyakula, Nursin Ayoub amesema wanalazimika kupandisha bei kwa kuwa maduka ya jumla wanauziwa bei ya juu.
"Mbaya zaidi wateja wanaenda kuhemea kwenye maduka ya jumla. Kwa hiyo wauzaji wanapandisha bei hadi kwetu," amesema.
Jiji la Arusha
Kwa upande wa Jiji la Arusha, baadhi ya wananchi wameanza kununua bidhaa za nyumbani ikiwamo vyakula ili kujihadhari.
Mmoja wa wafanyabiashara wa duka la jumla, Aminata Kessy alisema kuanzia mwanzoni mwa wiki hii ameshuhudia ongezeko la wateja, tofauti na hali ya awali, watu wengi wamejitokeza kununua vyakula na bidhaa muhimu za nyumbani.
"Kiukweli nikikumbuka Oktoba 29, 2025 tulivyoteseka nimejihami na familia yangu nimeshanunua vyakula na bidhaa zote muhimu ili kukitokea chochote tuwe na chakula ndani," amesema Joshua Abdiel mkazi wa Arusha.
Neema Amos amesema licha ya uchumi wake kuwa mdogo, amenunua mahitaji muhimu ikiwamo vyakula na kuhifadhi ndani.
Dar es Salaam
Mkoani Dar es Salaam, katika masoko ya Buguruni, Mahakama ya Ndizi na Mbezi, wakazi walionekana kwa wingi wakiwa katika ununuzi tofauti na hali ya kawaida.
Baadhi ya wananchi waliokutwa sokoni walisema wanafanya ununuzi huo kwa lengo la kuwa na akiba ya chakula na mahitaji muhimu ya nyumbani kabla ya Desemba 9, kutokana na hofu ya matokeo yanayoweza kutokea.
"Leo nimekuja Mahakama ya Ndizi kwa mara ya pili. Nilikuja juzi kununua unga, mchele na nafaka zingine na leo nitanunua viungo mbalimbali ili niwe na akiba ya wiki mbili au mwezi mmoja mbele, tulivyofungiwa nilipata tabu sana nina fedha mfukoni lakini sioni chakula cha kununua," amesema Nurat Ibrahim mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam.
Wiseman Mhando, mteja katika Soko la Mbezi Louis wilayani Ubungo amesema: "Kwa hali ilivyo na tunayoyasikia, nimeona leo nianze kununua mahitaji madogo madogo maana nimeshajifunza nilipitia kipindi kigumu sana baada ya Oktoba 29, sipo tayari kuishi yale maisha."
Mhando amesema bei nayo imeongezeka japo siyo sana, "mfano karoti na hoho hii sio bei niliyoizoea leo kuna mabadiliko kwa kweli, lakini sina budi maana hapo mbele hatujui itakuaje bora nichukue tahadhari mapema."
Mteja soko la Mbezi, Maimuna Ridhiwani amesema jirani yake amemsisitiza kuweka vitu ndani, hivyo ameona asipuuze, japo hana fedha ameanza kununua kidogo kidogo anaamini ikifika tarehe husika atakuwa na akiba nzuri.
Mteja mwingine Christopher Temba amesema, "nimekuja kuchukua mahitaji ya nyumbani, ameniagiza mke wangu amesema tujiandae kabisa, maana taarifa ni nyingi na siwezi kuzipuuza kwa sababu bado nina kumbukumbu na maisha tuliyoishi baada ya Oktoba 29, sasa nimekuja kujipanga kimahitaji najua bei zitapanda zaidi bora nianze na hivi vichache."
Kwa sasa ni neema kwa wafanyabiashara kama anavyoeleza mfanyabiashara wa Soko la Mbezi Louis, Athuman Ngopo.
"Hali ya biashara kwa sasa kiukweli imechangamka tofauti na hapo awali, watu wananunua kwa ‘package’ mfano huyu mama sijamzoea hivi ila naona leo amefungasha mzigo mkubwa, lakini hata sisi tukienda sokoni tunachukua mzigo mwingi na Alhamdulillah unaisha kwa sasa."
"Bei bado haijapanda sana, tupo pale pale tu ila siku mbili mbele nadhani itapanda maana magari yatakuwa yanaingia machache sana kuleta mzigo, hivyo tutanunua kwa bei ya juu."
Mfanyabiashara wa samaki wakavu, Shamte Likoko amesema tangu juzi anaona watu wanafungasha mizigo, "changamoto ni bei ninayonunulia imeongezeka inanilazimu niongeze na mimi ili nipate faida sasa wateja hawaelewi wanadhani tumepandisha makusudi."
Mfanyabiashara wa Soko la Mahakama ya Ndizi, Ismal Mgeja amesema kuna ongezeko la wateja tangu wiki hii imeanza na wanafika kununua mahitaji kwa wingi tofauti na ilivyozoeleka.
Mbeya
Wakazi wa Mbeya wamejitokeza kwa wingi kufanya ununuzi, huku bei za bidhaa katika baadhi ya masoko ikipaa kwa kiwango kikubwa jambo linalowafanya wananchi wa kipato cha chini kushindwa kumudu.
Mfanyabiashara wa mchele Soko la Sido, Tausi Azory amesema mchele umepanda kutoka Sh40,000 kwa debe moja mpaka Sh65,000 kulingana na ubora.
"Sababu kubwa za kupaa kwa bei ni kutokana na ugumu wa upatikanaji mazao kwa sababu wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakienda kwa wakulima shambani," amesema.
Mfanyabiashara wa dagaa, Kadara Ndomba alisema bei imepaa kutoka Sh11,000 hadi 14,000 kulingana na aina dagaa kwa ujazo wa lita nne.
Mfanyabiashara wa viazi mviringo Soko la Mabatini, Jane Joel amesema bei imepanda kwa plastiki la kilo 20 kutoka Sh12,000 hadi Sh15,000.
Mkazi wa Nonde jijini Mbeya, Rehema Mwanjonde amesema kimsingi hali ni mbaya kwa wananchi wa kipato cha chini na kuomba Serikali kuingilia kati kudhibiti wafanyabiashara kutumia maandamano kama sehemu ya kuumiza wananchi wa kipato cha chini.
Dodoma
Katika Mkoa Dodoma kwenye wilaya za Mpwapwa, Chamwino na Jiji la Dodoma ni unga pekee ndiyo umepanda huku vyakula vingine bei ipo chini ukilinganisha na msimu kama huu mwaka jana.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mazao ya nafaka, Abushir Yahaya amesema mchele umepungua kwa Sh200 kwa kilo ukilinganisha na bei ya mwaka jana katika msimu kama huu.
Kwenye bei hizi unga na maharagwe vimetajwa kupanda, maharagwe yameongezeka Sh100 kwa kilo wakati mfuko wa kilo 25 wa unga umepanda kwa Sh20,000.