Unguja. Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif amesema wizara hiyo haitomvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi za ujenzi chini ya kiwango kisichoheshimu mkataba wa makubaliano yao.
Nadir ameyasema hayo Alhamisi Desemba 4, 2025 akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa vituo vya kupokea na kupozea nishati ya umeme vilivyopo kisiwani Unguja.
Amesema, wananchi wana matumaini makubwa na wizara hiyo hivyo haitakuwa tayari kuwaacha makandarasi kujenga miradi chini ya kiwango na ikawafanya wananchi kupoteza imani kwao.
Vilevile, amesema ujenzi wa vituo hivyo unalenga kutatua kero za wananchi kuhusu changamoto ya nishati ya umeme hivyo ujenzi huo utaifungua Zanzibar kupata umeme wa uhakika.
Ameeleza, Serikali imedhamiria kuwa na nishati ya umeme wa uhakika ili kuongeza idadi ya wawekezaji visiwani humo na wafanyabiashara waendelee kuzalisha.
Amesema, kituo cha umeme kilichopo Welezo kitakuwa kituo kikuu cha kupokea umeme utakaotoka Fumba na baadaye kusambazwa katika kituo cha Makunduchi na Matemwe ili kufika kwa wakati bila ya changamoto.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Seif Kombo Pandu amesema mradi huo ni wa kimkakati hivyo kuna kila sababu ya wataalamu wa ujenzi kujenga kwa kiwango kinachoridhisha kwa maendeleo ya wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Joseph Kilangi amesema mradi huo unajengwa kwa kutumia fedha za mkopo wa Benki ya Dunia na unalenga kuwanufaisha wananchi.
Amesema, kuwepo kwa kituo cha kupozea nishati ya umeme na kupokelea hapa Zanzibar kitaondosha upotevu wa nishati hiyo wakati wa kusafirishwa.
Mshauri wa mradi huo amesema ujenzi umeshafikia asilimia 55 na utakamilika kwa muda uliopangwa.