Mazungumzo ya Kina Kuhusu Mbegu Bora za Miti Yapigwa Banjul, Gambia
Banjul, Gambia. Mazungumzo ya kina kati ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo na Dk Anders Pedersen, mtaalamu maarufu wa jenetiki ya miti na mmoja wa waanzilishi wa Tanzania Tree Seed Agency (TTSA), yamekuwa miongoni mwa matukio muhimu katika siku ya tatu ya kikao cha 25 cha African Forestry and Wildlife Commission (AFWC25), kilichoendelea Desemba 3, 2025, jijini Banjul.
Wawili hao wamekutana kando ya kikao na kujadili mustakabali wa upatikanaji wa mbegu bora za miti ikiwa ni nyenzo muhimu katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha misitu ya kibiashara na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwanda.
Akizungumzia safari ya taasisi hiyo, Profesa Silayo amesema TTSA iliyoasisiwa miaka ya 1990 ikijengwa juu ya tafiti na ushauri wa wataalamu, kwa sasa imeimarishwa zaidi kupitia Kitengo cha Uzalishaji Mbegu za Miti TFS, ambacho kinahakikisha upatikanaji wa mbegu zilizothibitishwa kisayansi kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.
"Mbegu bora ndiyo msingi wa misitu imara. Bila chanzo cha kuaminika, hatuwezi kuwa na misitu inayostahimili tabianchi na magonjwa. Misitu ya kesho inaanza na mbegu nzuri leo, na mbegu hizo zinapatikana TFS," amesema Profesa Silayo akiwahimiza wadau na wawekezaji kununua mbegu bora kutoka kwa wakala huo.
Dk Anders, ambaye amekuwa mshauri wa muda mrefu katika sekta ya mbegu Tanzania na Afrika Mashariki, amesema Afrika iko kwenye nafasi adhimu ya kuongoza dunia katika mageuzi ya misitu endapo itawekeza kikamilifu kwenye ubunifu wa kielimu na vyanzo vya mbegu vilivyoboreshwa.
"Tulipoanzisha TTSA tuliona pengo kubwa la upatikanaji wa mbegu bora. Leo mahitaji yameongezeka zaidi, lakini uwezo wa kuzalisha suluhisho upo, hasa kupitia taasisi kama TFS," amesema.
Mazungumzo hayo yameibua tena umuhimu wa kuwekeza kwenye sayansi ya mbegu bora, jambo ambalo linatajwa kuwa uti wa mgongo wa misitu inayohitajika kukabiliana na changamoto za ardhi, viwanda vya mazao ya misitu na mahitaji mapya ya kimataifa.