Madiwani wa Mufindi Watakajiwa Kuwashirikisha Wananchi Katika Maamuzi
Mufindi – Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, wametakiwa kusikiliza zaidi wananchi ni kitu gani wanahitaji kwenye maeneo yao, kuliko kuwaamulia bila kuwashirikisha.
Hayo yameelezwa Jumatano Desemba 3, 2025 na mwenyekiti wa muda wa uchaguzi, ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo, wakati madiwani wakila kiapo na kutoa ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.
Madiwani hao walifanya uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake katika mkutano wa baraza la kwanza la madiwani lililokutana kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo.
Chongolo amesema viongozi hao wanapaswa kubadilisha namna ya utendaji kazi wao kwa kuwasikiliza na kujadiliana na wananchi ili kujua mahitaji yao ya msingi.
"Sote tunafahamu tulipita katika mtikisiko kidogo kwa wale ambao tupo karibu na mji mtakuwa mnaelewa. Twendeni kwa wananchi tukawasikilize na kujua mahitaji yao, kwa kufanya hivyo tutajua kitu gani wanahitaji kwa wakati huo," amesema.
Ameeleza kila kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha huduma bora zinatolewa ambazo zinaonyesha matokeo chanya na tija kwa wananchi, ikiwamo kusimamia fedha, kupanga mipango na utekelezaji wa mifumo mbalimbali kwenye miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Chongolo amewasisitiza madiwani kuhakikisha miradi ambayo haikukamilika kipindi kilichopita inakamilika kabla ya kuanzisha mipya ili ufanisi uonekane.
Kiongozi Ni Kioo Kwa Jamii
Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Linda Salekwa, aliwataka madiwani kutumia vizuri nafasi zao kwa kuwatumikia wananchi, badala ya kusababisha migogoro kwenye maeneo yao.
"Kiongozi ni kioo kwa jamii anayoiongoza kwa sababu huwezi kuwa kiongozi halafu unakuwa chanzo cha migogoro katika eneo lako. Hivyo, niwaombe madiwani mnapaswa kuzingatia maadili ya viapo vyenu mnapokuwa kwenye maeneo yenu ya kazi," amesema.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mashaka Mfaule amesema amepokea maelekezo yaliyotolewa na viongozi hao, hivyo atahakikisha wanakwenda kuyafanyia kazi ili wananchi wapate huduma bora na stahiki kwenye maeneo yao.
Akizungumza baada ya kuapishwa, diwani wa Ihalimba, Different Lufyagile amesema amepokea maelekezo, hivyo atahakikisha anashirikiana na wananchi kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye kata hiyo ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
"Nitakuwa mtu wa kuwasikiliza zaidi wananchi kwa kujadiliana kwa pamoja ili tuweze kupata majibu katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yetu," amesema.
Katika mkutano huo, madiwani wameunda na kuchagua viongozi wa kamati za kudumu kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri hiyo.