Tanzania Kuanza Kuandaa Tuzo za Afrika kwa Sekta ya Ujenzi
Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuanza kuandaa Tuzo za Afrika zinazolenga kuzitambua kampuni zinazofanya vizuri katika sekta ya ujenzi na nyingine zinazohudumu katika mnyororo wa thamani.
Tuzo hizo zitakazoanza kutolewa mwakani, ni mbadala wa tuzo za Afrika Mashariki za Sekta ya Ujenzi na Miundombinu (EABC) ambazo zilikuwa zikitolewa nchini kwa miaka mitano mfululizo.
Walengwa katika tuzo hizi ni watoa huduma wa chakula katika maeneo ya ujenzi, rangi, vifaa vya ujenzi, malazi na wengine ikiwemo sekta za fedha.
TNC imebaini kuwa juhudi hizi zinalenga kuhamia Afrika ili kutanua wigo wa kuwatambua watoa huduma katika sekta hii na kazi wanazofanya.
Mwenyekiti wa Chemba ya Ujenzi, Pamela Shoo amesema sekta ya ujenzi na miundombinu ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huku akiiomba Serikali kuongeza ushirikiano na wadau ili kuiwezesha sekta hiyo kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani.
Mmoja wa walipokea tuzo kama watoa huduma bora wa chakula, Meneja Masoko wa Gwambina Group, Gerald Tronche amesema juhudi zao kupitia utoaji huduma ya chakula katika sekta ya madini, ujenzi na kampuni mbalimbali ndiyo sababu iliyowafanya washinde tuzo hiyo.
Amesema wamepata tuzo hiyo kwa mara ya pili kupitia jukwaa la EABC jambo ambalo linawahamasisha kuendelea kutoa huduma bora.
Amesema wamekuwa wakitoa huduma ya chakula katika miradi ya Serikali na binafsi ya ujenzi jambo ambalo limefanya watu kuona juhudi zao.
"Tunajivunia katika huduma bora na tunawahi sana kufanyia kazi changamoto zinapotolewa ndani ya saa 24. Pia tunajivunia kuwa na watoa huduma wabobevu katika tasnia hii ambao baadhi wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30," amesema.
Meneja uendeshaji wa Gwambina Group, James Mongella amesema hiyo ni tuzo ya tano wanapata ndani ya mwaka huu, huku akisema ukuaji wao wa kasi na kuamini kuwa mwakani itakuwa kampuni ya kwanza kuchaguliwa na wadau kushinda tuzo hiyo.