Mahakama Kuu Yatoa Maelekezo Kuhusu Shauri la Tume ya Rais
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeipa Serikali na wajumbe wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025, wanakabiliwa na shauri mahakamani kuwasilisha utetezi wao.
Pia, mahakama hiyo imewataka waombaji katika shauri hilo la maombi ya kibali cha kupinga uteuzi wa tume hiyo, kuwapatia wajibu maombi, wajumbe wa tume hiyo, nyaraka za shauri hilo ndani ya siku mbili.
Maelekezo hayo yametolewa Jumanne, Desemba 2, 2025 na Jaji Hussein Mtembwa anayesikiliza shauri hilo, wakati lilipotajwa kwa mara ya kwanza.
Tume hiyo inayoongozwa Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mohamed Chande ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 20, 2025 kuchunguza matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wakati shauri hilo lilipotajwa, waombaji hao wamewakilishwa na mawakili, Mpale Mpoki (kiongozi) na Hekima Mwasipu, huku Serikali imewakilishwa na mawakili wake Mark Mulwambo, Stanley Kalokola na TLS ikiwakilishwa na Ferdnand Makore.
Hata hivyo, japo shauri hilo limetajwa kwa njia ya mtandao, mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo ya Rais hawakutokea.
Wakili Mpoki ameieleza mahakama kuwa walikuwa hawajawapatia nyaraka zinazohusiana na shauri hilo wala taarifa ya mahakama ya kuwepo kwa kesi hiyo.
Kwa upande wake Wakili Mulwambo ameiomba mahakama iwape siku 10 kuwasilisha kiapo kinzani kujibu madai hayo.
Hata hivyo, Jaji Mtembwa amewaelekeza waombaji kuwapatia nyaraka na hati ya taarifa ya kesi hiyo wajibu maombi wa pili mpaka wa tisa (mwenyekiti na wajumbe wa tume) na mahakama hiyo imeipa siku saba Serikali na wajibu maombi wengine wote kuwasilisha viapo kinzani.
Hivyo, Jaji Mtembwa amepanga shauri hilo litajwe Desemba 10, 2025, siku ambayo wadaiwa wote watatakiwa kufika mahakamani, kwa ajili ya kuangalia kama maelekezo hayo yametekelezwa kabla ya kutoa amri nyingine.
Katika shauri hilo lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, waombaji hao wanaomba kibali kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama kuomba amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.
Wanahoji uhalali wa uteuzi huo, wakidai ulifanywa kwa nia ovu, kinyume cha kanuni hiyo ya haki asili.