Historia ya Libya: Somo kwa Tanzania
Oktoba 20, 2011, saa 2:30 asubuhi kwa saa za Ulaya Mashariki, saa 4:30 asubuhi Tanzania, aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, akiongozana na vikosi vya jeshi la Libya, walikuwa wakikatiza barabarani kwenye mji wa Sirte.
Uelekeo wa Gaddafi ulikuwa kwenye eneo Jarref Valley, mji aliozaliwa. Inaamimika kuwa Gaddafi alikuwa na uhakika wa kupata maficho Jarref Valley, kisha baadaye angetoroka nchi kwa kupitia Bahari ya Mediterranean.
Hata hivyo, msafara wa Gaddafi ulishambuliwa kwa mabomu ya angani kutoka kwenye ndege za kivita za Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato). Msafara wa Gaddafi ukatawanyika. Mahali Gaddafi alipokimbilia, akajikuta mikononi mwa wanamgambo waasi wa Misrata.
Wanamgambo hao wa Misrata, walimkamata Gaddafi, wakampiga, wakamtesa na kumdhalilisha huku wakimchukua picha za video kupitia simu. Mwisho, walimuua. Mwili wa Gaddafi ulimiminiwa risasi nyingi tumboni, nyingine kifuani na maeneo mengine. Huo ukawa mwisho wa Gaddafi.
Miaka 14 Baada ya Gaddafi
Ni miaka 14 imepita tangu Gaddafi alipouawa. Na imetimia miaka 14 na miezi minane kutoka Machi 19, 2011, siku ambayo utawala wa Gaddafi ulipinduliwa rasmi Tripoli. Kipindi hiki Tanzania kuna hamasa ya ghasia mitandaoni, ni vizuri kusoma kwa wenzetu, ili kutambua matokeo ya kile kinachochokonolewa.
Kuelekea kumwondoa Gaddafi, Marekani na mataifa mengine makubwa washirika, walifadhili vikundi vingi vya uasi ili kufanikisha lengo lao. Vikundi hivyo walivipa silaha na kuvilinda vilipokuwa vinachanja mbuga kushikilia miji mbalimbali mpaka vilipofika mji mkuu na makao makuu ya nchi, Tripoli.
Nato ilikuwa imara kuyakabili majeshi ya Serikali, kila yalipotaka kuwakabili waasi. Kutokana na hali hiyo, waasi waliua watu hususan walioonekana kuwa wafuasi wa Gaddafi. Majeshi ya Serikali yalipotaka kujibu yalikutana na Nato pamoja na mkwara wa Marekani, Ufaransa, Italia, Uingereza na nchi nyingine.
Machafuko Baada ya Mapinduzi
Baada ya Gaddafi kupinduliwa na kuuawa, vikundi hivyo havikutii wito wa kuweka silaha chini na kuunda Serikali moja. Matokeo yake Libya ikawa "na majeshi mengi", kila kikundi chenye silaha kilichohusika wakati wa vita ya kumpindua Gaddafi kinajiona ni jeshi kamili. Hiyo ndiyo sababu ya utulivu kukosekana Libya. Upo wakati Libya ilikuwa na vikundi vya kijeshi zaidi ya 30,000.
Oktoba 23, 2011 (siku mbili baada ya Gaddafi kuuawa), Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC) liliitangaza Libya kuwa imekombolewa. Kiongozi wa NTC, Mahmoud Jibril alisema mashauriano ya ujenzi mpya wa Libya yalikuwa yameanza. Baadaye Jibril alijiuzulu na NTC ilimchagua Abdurrahim el-Keib kuwa Waziri Mkuu wa Libya. Aprili 26, 2012 el-Keib aliondolewa madarakani na wajumbe wa NTC.
Julai 2012 uchaguzi ulifanyika kwenye maeneo machache, ikachaguliwa Serikali ya Baraza Kuu la Taifa la Congress (GNC) na Novemba mwaka huo, Ali Zeidan alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu. Machi 2014 GNC walimtoa Zeidan madarakani na kusabisha machafuko.
Serikali Mbili za Libya
Agosti 4, 2014, uchaguzi mwingine ulifanyika na Baraza la Manaibu (CoD) ambalo hutambulika zaidi kama Baraza la Wawakilishi (HoR), lilichaguliwa kuunda Serikali, lakini GNC wakamtangaza Omar al-Hasi kuwa Waziri Mkuu.
Kutokana na mvutano huo, Libya ikawa na Serikali kuu mbili, moja ni ya GNC ambayo makao yake makuu yapo mji mkuu wa Tripoli na ile ya CoD au HoR inayoendesha Serikali kutokea Jiji la Tobruk ambalo ndilo wanalitangaza kuwa mji mkuu mpya wa Libya.
Vipo vikundi vingine vikubwa vinavyotambulika kuwa na silaha pamoja na wapiganaji wengi, vikiwa vimeshikilia maeneo yao ya kiutawala. Kuna Baraza la Shura ya Uislamu ya Wanamapinduzi wa Benghazi, linaoongozwa na Ansar al-Sharia, hili limetapakaa maeneo yote ya Libya.
Lipo kundi la Dola ya Kiislam ya Iraq na Levant (ISIL’s), hili lipo baadhi ya majimbo, vilevile kuna wapiganaji wa Ghat, Tuerag, wanaodhibiti maeneo ya jangwa Kusini-Magharibi. Vipo vikundi vingine ambavyo hata majina havitambuliki, vipo Misrata na vinadhibiti miji ya Bani, Walid na Tawergha.
Pamoja na vyote hivyo, kuna wanajeshi wengi ambao hufanya matukio kisha kuhama kutoka mji mmoja hadi mwingine. Hao ni wengi na madhara yake ni makubwa. Katika hali hiyo, Libya inakuwa haina udhibiti wa pamoja kama Taifa.
Juni 2018, HoR walifanya kile kilichotafsiriwa kuwa ni kuikomoa Marekani na jumuiya za kimataifa kwa kumtoa jela mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam ambaye alikuwa akiandaliwa na baba yake kuwa mrithi wake. Hivi sasa Saif anatajwa kuwa mmoja wa viongozi wa HoR.
Somo kwa Tanzania
Hivyo ndivyo Libya imekuwa. Taifa ambalo lilikuwa na utulivu chini ya Gaddafi, leo limekuwa maskani ya vikundi vya uasi. Kila kikundi chenye bunduki 10, kinajitangaza kuwa jeshi. Libya inakutana na matokeo ya kudharau methali: "Zimwi likujualo halikuli likakwisha." Hamasa ya kutaka zimwi jipya, sasa zimwi jipya linawala Walibya, linawamaliza.
Libya imegeuka maskani ya biashara ya utumwa. Binadamu wanauzwa kama bidhaa. Hayo ni matokeo ya Libya chini ya zimwi jipya. Na hutakiwi kuangalia Libya peke yake, Iraq, Syria, Sudan, Tunia, Misri na nchi nyingi zilizochagua ghasia dhidi ya Serikali zao.
Inawezekana kuundoa utawala madarakani, halafu Jeshi likachukua nchi, kisha ukawadia udikteta wa kijeshi, na mapinduzi ya kijeshi kama Nigeria ilivyokuwa kwa miaka 33, 1966 – 1999. Inaweza kutokea mgawanyiko wa kijeshi, vikosi mbalimbali vikajitangazia utawala. Yote ni hatari.
Mitandaoni kuna hamasa ya kuingia barabarani Desemba 9, wengine Desemba 25 (Siku ya Krismasi). Huwezi kudharau, maana Oktoba 29, ilitokea. Ni vizuri kipindi hiki, watu watafakari, changamoto zilizopo na fursa za kuendelea kujenga nchi moja, dhidi ya machafuko, vifo na kumwelekea zimwi tusilolijua.