KCMC Yapanga Kuanzisha Benki ya Vinasaba kwa Ajili ya Utafiti wa Afya
Moshi – Chuo Kikuu cha KCMC mkoani Kilimanjaro kimepanga kuanzisha benki ya vinasaba mbalimbali katika juhudi za kuimarisha utafiti na ubunifu katika kada za afya nchini, ili kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Lughano Kusiluka, ametoa taarifa hii wakati wa mahafali ya kwanza tangu taasisi hiyo itangazwe kuwa chuo kikuu rasmi. Mahafali hayo yamefanyika katika viwanja vya chuo hicho na jumla ya wahitimu 559 wamehitimu fani mbalimbali za afya.
"Tunakusudia, kama chuo kikuu, kuboresha kiwango cha utafiti, kuongeza ubunifu na kuimarisha huduma za ushauri elekezi pamoja na huduma za jamii katika maeneo tunayobobea. Lakini pia tunataka kuanzisha benki ya vinasaba mbalimbali ambayo tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo mbalimbali duniani," amesema Profesa Kusiluka.
Amesisitiza kuwa chuo hicho kitaendelea kuhakikisha elimu inayotolewa inaheshimika ndani na nje ya Tanzania.
"Tutaendelea kuhakikisha wahitimu wetu ni bora, wanaouzika na wanaojitangaza kwa ujuzi wao, si kwa vyeti. Vyeti vije baadaye lakini kwanza tuone ujuzi na namna wanavyotengeneza taaluma yao," amesema.
Katika hotuba yake kwa wahitimu, Profesa Kusiluka amewataka kuzingatia maadili ya taaluma zao na kuonyesha umahiri katika kutoa huduma za afya kwa Watanzania.
"Tunawapongeza sana wahitimu wote, najua safari haikuwa ndogo, mmefika hapa mkiwa na akili timamu kabisa. Kaipeperusheni bendera ya KCMC, zingatieni maadili ya taaluma zenu, thibitisheni umahiri wenu ili watu wengi wapone na kuwa na afya njema, ndio furaha yetu," amesema Profesa Kusiluka.
Profesa Kusiluka pia amewakumbusha wahitimu kuwa Taifa limewekeza kwao na hivyo linawategemea kwa kiwango kikubwa katika kutoa huduma bora za afya.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Ephata Kaaya, amesema katika mahafali hayo wahitimu kutoka fani 22 za afya zenye jumla ya wahitimu 559 wamehitimu.
"Kati ya hao, stashahada ni 14, shahada ya kwanza 402, shahada za uzamili 135 na shahada za uzamivu 8," amesema Profesa Kaaya.
Ameeleza kuwa katika mwaka huu wa masomo, wahitimu wa kiume ni 246 (asilimia 44) na wa kike 300 (asilimia 56), ikilinganishwa na mwaka jana ambapo wahitimu wa kike walikuwa asilimia 52 na wa kiume asilimia 48.
Aidha, amesema kwa mwaka wa masomo 2024/2025 chuo hicho kimefanikiwa kuchapisha machapisho saba katika majarida yenye hadhi kubwa duniani, hatua ambayo inadhihirisha maendeleo makubwa ya kitaaluma.