Mauaji ya Wanawake Yaendelea Kuwa Tishio Duniani
Dar es Salaam – Mauaji ya wanawake duniani yameendelea kuwa tishio kwa usalama wa kundi hilo, huku takwimu zikionesha idadi ya wanauoawa kwa mwaka iko juu.
Takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa (UN) zikionesha kuwa, mwaka 2024 pekee, wanawake na wasichana 50,000 waliuawa na wenza wao wa karibu au wanafamilia, sawa na wastani wa wanawake 137 wanaopoteza maisha kila siku.
Pamoja na kwamba jamii nyingi zinaona mauaji hayo kama matukio ya kawaida kwenye ngazi ya familia, wataalamu wanatahadharisha kuwa, mauaji dhidi ya wanawake ni tatizo zaidi ya mauaji ya kawaida.
Hatua hiyo inatajwa kuwa ni matokeo ya mifumo kandamizi ya kijinsia, ukatili wa kimfumo na ukosefu wa uwajibikaji unaozidi kuota mizizi.
Afrika Yaongoza Takwimu za Mauaji
Kwa mujibu wa ripoti ya UN, takribani asilimia 60 ya mauaji ya wanawake hufanywa na waume, wapenzi au wanafamilia wa karibu. Kwa maneno mengine, nyumba ambayo ingepaswa kuwa mahali salamu imekuwa uwanja wa mauaji.
Hali hiyo inaonekana kuwa mbaya zaidi Afrika. Mwaka 2024, bara hilo limeongoza kwa idadi ya wanawake waliouawa na wenza au wanafamilia, ikifikia 22,600.
Matukio ya aina hiyo yamekuwa yakiripotiwa pia hapa nchini huku wivu wa kimapenzi ukitajwa kuwa chanzo cha mauaji dhidi ya wanawake yanayofanywa na wenza wao.
Ripoti ya UN inaeleza kuwa, mfumo dume uliokithiri, umaskini sugu, migogoro ya kijamii na mifumo dhaifu ya usalama vinachangia kuifanya Afrika kuwa kitovu cha tatizo hilo.
Wanawake Katika Nafasi za Umma Wako Hatarini
Mbali na hilo, ripoti inaonesha kuwa wanawake katika nafasi za umma – wanasiasa, wanahabari, watetezi wa haki, na watetezi wa mazingira – ndiyo waathirika wakubwa wa mashambulizi yanayoweza kuzalisha mauaji.
Vitisho wanavyotokea nje na mtandaoni vinatokana na mchanganyiko wa chuki ya kijinsia, uonevu wa kisiasa na mazingira duni ya ulinzi.
Wataalamu Watoa Maoni
Mtaalamu wa masuala ya jinsia na familia, Angela Laiser amesema chanzo kikuu cha mauaji hayo ni imani potofu inayowapa wanaume umiliki wa maisha ya wanawake.
Amesema mabadiliko ya kijamii yenye kuwapa wanawake fursa zaidi kielimu, kiuchumi na kisiasa yanahitaji kuambatana na elimu ya kujenga uhusiano wenye heshima na si mgongano unaozalisha ukatili.
"Kwa baadhi ya wanaume, kupoteza udhibiti wa mwanamke ni sawa na kupoteza mamlaka. Wanapoona hawana tena nguvu hizo, hulipiza kwa ukatili," amesema Laiser.
Mtetezi wa haki za wanawake, Kelvin Masebo amesema tatizo si tu mauaji bali kutokuwepo kwa hatua madhubuti dhidi ya wahusika.
Amesema mifumo ya ulinzi kwa wanawake inahitaji kuimarishwa mara moja ili kuzuia matokeo mabaya zaidi.
"Kesi nyingi za ukatili huishia kwa maridhiano, rushwa au kuahirishwa bila uchunguzi. Ukiona mhalifu anaweza kupiga, kumjeruhi au hata kutishia mwanamke mara kwa mara pasipo hatua, basi mauaji sio mbali," amesema Masebo.
Vitisho vya Mtandaoni
Mwanaharakati anayepigania usalama wa wanawake mtandaoni, Maria Nchimbi amesema licha ya matishio ya mitandaoni kutochukuliwa kwa uzito lakini yanakatisha maisha ya watu.
"Wengi huanza kudharauliwa mtandaoni, kuingiliwa faragha, kisha vitendo hivyo vinahamia katika maisha halisi. Mara nyingi hatuchukulii vitisho vya mtandaoni kwa uzito, lakini vinakatiza maisha ya watu," amesema Maria.
Suluhisho Linalopendekezwa
Katika kukabiliana na hilo, Laiser anashauri kuanzishwa kwa programu za elimu kwa wanaume na vijana ili kuvunja mizizi ya fikra hatarishi.
Sambamba na hilo anashauri kuongeza huduma za tiba na ushauri na kusimamiwa kikamilifu kwa sheria kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kupata hatua stahiki.
"Tukiacha hili liendelee, tutafika kwenye Taifa linalowazika wanawake kuliko kuwalea, maana mauaji haya hayapo tu kimataifa hata hapa nchini tumekuwa tukisikia matukio ya aina hii mara kadhaa," amesema Laiser.