Mfanyabiashara Niffer Asalia Rumande Huku Wengine Wakifutiwa Mashtaka ya Uhaini
Dar es Salaam/Mikoani. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) ameendelea kuwafutia mashtaka washtakiwa wa kesi za uhaini, lakini mfanyabiashara wa vipodozi, Jenifer Jovin (26), maarufu Niffer, anaendelea kusalia rumande kwa kuwa mashtaka dhidi yake hayajafutwa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Niffer, mwandishi wa habari wa Kituo cha Ayo TV na wafuasi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamefutiwa mashtaka na kuachiwa huru leo Novemba 25, 2025.
Akilihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma, Novemba 14, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza msamaha kwa vijana waliofikishwa mahakamani kwa kesi za uhaini kwa kufuata mkumbo wa kushiriki kwenye vurugu.
Alivielekeza vyombo vya sheria na hasa ofisi ya DPP kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana hao na kwa ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wafutiwe makosa yao.
Jana Novemba 24, 2025 washtakiwa 210 waliachiwa huru mkoani Arusha wakiwa 24, Mwanza (139) na Dar es Salaam (47).
Niffer na Mshtakiwa Mwingine Wasalia Rumande
Washtakiwa 20 kati ya 22 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na Niffer, wamefutiwa mashtaka na kuachiwa huru.
Niffer na wenzake 21 walifunguliwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiwa miongoni mwa washtakiwa 310 waliofunguliwa mashtaka hayo mahakamani hapo wakiwa katika makundi sita.
Wanadaiwa kujihusisha na makosa hayo yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati wa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.
Mbali ya hao, washtakiwa 217 wamefikishwa mahakamani hapo leo Novemba 25, 2025.
Niffer na wenzake walisomewa mashtaka mawili ya kula njama kutenda kosa la uhaini, kosa lililodaiwa kutendwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili mosi na Oktoba 29, 2025.
DPP Atumia Mamlaka Kufuta Mashtaka
Washtakiwa 20 wameachiwa huru baada ya DPP kuwafutia mashtaka kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Titus Aron ameieleza Mahakama kuwa, kesi iliitwa kwa ajili ya uamuzi kuhusu dosari kwenye hati ya mashtaka.
Hata hivyo, amesema DPP hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa 20, isipokuwa kwa mshtakiwa wa kwanza Niffer na wa 17, Mika Chavala (32), ambao watasalia katika kesi hiyo.
"Shauri hili lilipangwa leo kwa ajili ya uamuzi lakini leo Novemba 25, 2025, tumewasilisha hati inayoitwa Nolle Prosequi (taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendela na mashtaka) kwa mujibu wa kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai marejeo ya mwaka 2023," amesema.
"Kwa mujibu wa kifungu hiki, Mkurugenzi wa Mashtaka hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa kwanza (Niffer) na wa 17 (Chavala)."
Baada ya kupokea taarifa hiyo ya upande wa mashtaka, Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya amesema kesi hiyo inaondolewa rasmi dhidi ya washtakiwa 20 iaipokuwa hao wawili, Niffer na Chavala.
"Kwa sababu upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea na mashtaka isipokuwa kwa mshtakiwa wa kwanza na wa 17, kwa washtakiwa wengine shauri hili linaondolewa mahakamani," amesema.
Kesi ya Niffer Yaahirishwa
Hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 3, 2025 kwa ajili ya kitajwa kwa shauri dhidi ya Niffer na Chavala.
Awali, katika kesi ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26388 ya mwaka 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Lyamuya Niffer na wenzake walisomewa mashtaka matatu.
Niffer na wenzake 21 walikabiliwa na shtaka la kula njama kutenda kosa la uhaini na lingine la uhaini lilllomuhusu yeye peke yake.
Wenzake kwa pamoja walikabiliwa na shtaka la uhaini.
Katika shtaka la kwanza, walidaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, Chavala anadaiwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025.
Wanadaiwa walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Shtaka la tatu ambalo ni la uhaini linamkabili Niffer pekee ambaye pamoja na mambo mengine anadaiwa kuwahamasisha watu kununua dukani kwake vifaa vya kujikinga na mabomu ya machozi.
Mwandishi wa Habari Ayo TV Aachwa Huru Arusha
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini washtakiwa wanne, akiwamo mwandishi wa Habari wa Ayo TV, Godfrey Ng’omba.
Wengine walioachiwa ni watoto watatu wa kiume wenye umri wa miaka 13, 16 na 17 (waliokuwa mahabusu ya watoto) ambao kwa pamoja walishtakiwa kwa makosa ya uhaini.
Uamuzi huo umefikiwa leo Jumanne Novemba 25, 2025 na Hakimu Mkazi Regina Oyier, baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kuwa DPP, hana nia ya kuendelea kuwashtaki.
Jamhuri iliieleza Mahakama kuwa mashauri mawili yalipangwa kutajwa lakini DPP kwa niaba ya Jamhuri hana nia ya kuendelea kuwashtaki chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Washtakiwa hao wanne ni miongoni mwa wenzao 59 wanaowakilishwa na jopo la mawakili likiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Arusha, Khamisi Mkindi.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa mawili ya kula njama ya kutenda kosa kinyume cha kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ikidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Oktoba mosi hadi 29, 2025 walifanya njama za kutenda kosa la uhaini.
Kosa la pili ni la uhaini kinyume cha kifungu cha 39 (2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Hakimu Oyier aliwaachia huru washtakiwa hao pasipo masharti yoyote.
Washtakiwa 24 wa kesi za uhaini walioachiwa huru na Mahakama hiyo jana Novemba 24 watakuwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja na kutakiwa kuripoti mara moja kila mwezi kituo cha polisi.
Wafuasi Sita wa Chadema Waachwa Huru Mbeya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imewaachia huru washtakiwa sita, ambao ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliokabiliwa na makosa mawili ya kula njama za kufanya kosa na uhaini.
Uamuzi wa kufuta shauri la uchunguzi (P.I 26722/2025) umetolewa leo Novemba 25 na hakimu Mtengeti Sangiwa, baada DPP, kupitia Wakili wa Serikali, Dominick Mushi, kuieleza Mahakama hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Mushi ameeleza kwa mamlaka aliyonayo DPP chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, haoni haja ya kuendelea na mashtaka hayo.
Baada ya maelezo hayo, Sangiwa ametoa uamuzi wa kuwaachia huru washtakiwa wote sita.
Mmoja wa walioachiwa huru, Andrew Kasesela, amesema wamepitia magumu lakini wanamshukuru Mungu na wananchi waliowasaidia.
"Haikuwa kazi rahisi, tumepitia mazito sana," amesema.
Wengine walioachiwa huru ni Adam Melele, Lusekelo Lugani, Daud Sent, Philemon Sanga na Paul Mwangama.
Wote watapaswa kuripoti kituo cha polisi licha ya kuachiwa.
Baada ya uamuzi wa Mahakama, Askofu Kais Mwambona wa Kanisa la T.A.G alifanya ibada maalumu kuwaombea, tukio lililohudhuriwa na wananchi na wafuasi wa Chadema.
Mwenyekiti wa Bavicha Mbeya Mjini, Hassan Mwamwembe, amesema licha ya kuachiwa kwa makada hao, bado wako vijana wanaoweza kukamatwa hivyo mapambano yanaendelea.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Joseph Kasambala, amesema mapambano ya kudai haki hayajaisha.