Waziri Ulega Atoa Ruhusa Daladala Zitumie Barabara ya BRT Gongo la Mboto
Dar es Salaam – Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa ruhusa kwa magari ya kawaida ya abiria kuitumia barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu ya Gongo la Mboto, ili kupunguza msongamano katika Barabara ya Nyerere.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza msongamano wa magari kwa watumiaji wa njia hiyo, unaosababishwa na ufinyu wa barabara na wingi wa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara hiyo.
Waziri ametoa ruhusa hiyo katika kipindi ambacho tayari utekelezaji wa awamu ya tatu ya miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka umefikia asilimia 96, huku ujenzi wa barabara za zege ukikamilika kwa asilimia 100.
Hata hivyo, Serikali inaendelea na mchakato wa kumpata mtoa huduma kwa ajili ya kuleta mabasi yaendayo haraka na hatimaye barabara hiyo ianze kutumika, ndio maana ameruhusu kwa kipindi hiki itumike na daladala.
Maelekezo ya Rais Samia
Ulega ametoa maelekezo hayo Jumanne Novemba 25, 2025 alipozungumza na wananchi wa Gongo la Mboto, wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu na barabara mbalimbali, Dar es Salaam.
"Hayo ndio maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, amenituma nije kutoa ruhusa kwamba kipindi hiki ambacho mabasi hayajawa tayari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ijipangie utaratibu wa kuruhusu magari mengine yaendelee kutumia barabara," amesema Waziri.
Amesema haiwezekani barabara zimejengwa na wananchi wenyewe na inakuwa vigumu kuitumia huku watu wakiendelea kukwama katika msongamano.
Waziri amesisitiza anafanya hivyo ili kuhakikisha msongamano wa magari katika njia hiyo unapungua na wananchi wanapata nafasi ya kufika katika shughuli zao na huduma kwa haraka zaidi.
Ombi la Mkuu wa Mkoa
Maelekezo hayo ya Ulega yametokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyesema angalau Serikali iruhusu barabara za mabasi yaendayo haraka zitumike na magari mengine yanayobeba abiria katika kipindi ambacho bado mabasi yaendayo haraka hayajafika.
Chalamila ameeleza ni muhimu ifanyike hivyo ili kupunguza kiwango cha msongamano kinachowakabili watumiaji wa barabara hiyo ya Nyerere.
"Mabasi yakifika magari yatatoka na barabara zitaendelea kufanya kazi yake. Yakifika nitakuja kuzungumza na wananchi na kuwaambia watoe magari yao ili mabasi yaendayo haraka yaendelee na huduma," amesema Mkuu wa Mkoa.
Maendeleo ya Mradi
Akitoa taarifa kuhusu mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu kuanzia katikati ya Dar es Salaam hadi Gongo la Mboto, mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mongo Malima amesema mkandarasi ni Sino Hydro kutoka China na gharama za ujenzi ni Sh231.66 bilioni zilizotokana na mchango wa Serikali na Benki ya Dunia.
Mradi huo umefanyika kwa miezi 41 na kazi zinapaswa kukamilika Desemba 31, mwaka huu na hadi sasa utekelezaji ni asilimia 96 ambayo ni zaidi ya mpango wa mkandarasi.
Kazi zilizokamilika ni ujenzi wa miundombinu ya maji ya mvua, barabara za zege asilimia 96, ujenzi wa barabara za lami kwa ajili ya magari ya kawaida asilimia 97 na vituo vya mabasi imekamilika.
Kazi zinazoendelea sasa ni umaliziaji na kwamba kuna marekebisho ya miundombinu iliyoathiriwa. Kazi zote za barabara zimekamilika na barabara inaweza kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Malalamiko ya Wananchi
Katika ziara hiyo, wananchi walipewa nafasi ya kuzungumza, Abdul Malisa ameomba kuondolewa kwa askari wa usalama barabarani anayewasumbua wafanyabiashara katika eneo hilo kwa kumwaga biashara zao.
"Anatusumbua akikukuta anakuchapa fimbo na anamwaga biashara yako, kwa jina siwezi kumtaja lakini anatusumbua sana, naomba utusaidie. Hatuna cha kumfanya tunaomba tusaidie," amesema Malisa anayefanya biashara ya maji.
Hatua hiyo imesababisha Ulega kuagiza ufuatiliaji wa taarifa za askari huyo na mamlaka zinazohusika, huku akimzawadia Sh100,000 Malisa ikiwa ni kuongezea mtaji wake wa biashara ya maji.
Eneo la Biashara Buguruni
Akiwa Buguruni katika ziara hiyo pia, Waziri amemwelekeza Chalamila kuangalia uwezekano wa kuwezesha upatikanaji wa eneo la biashara kwa wafanyabiashara wa eneo hilo kunakojengwa barabara.
Maelekezo yake hayo yametokana na maombi ya wananchi aliowapa fursa ya kumweleza changamoto zao na wakasema ujenzi wa barabara unaoendelea utawanyima nafasi ya kufanya biashara.
"Mkuu wa Mkoa utaangalia kujua kwa eneo la nani na mtafanya utaratibu wa kuona kama inawezekana wafanyabiashara wapewe waendelee na shughuli zao," amesema Ulega.
Katika maelezo yake, Chalamila amesema atawasiliana na mamlaka mbalimbali kujua anayehusika na kwamba wananchi wavumilie wakati Serikali ikifanya utaratibu.