Umuhimu wa Kumruhusu Mtoto Kuuliza na Kujibu Maswali
Dar es Salaam – Moja ya zawadi kubwa ambayo mzazi anaweza kumpa mtoto si fedha, si shule za gharama, bali mazingira ya kuuliza na kujibu maswali bila hofu.
Katika familia nyingi, watoto hukuzwa kwenye mifumo inayozuia kuuliza, kuhoji, au hata kujaribu kuelewa kwa kina. Mara nyingi swali la mtoto hujibiwa kwa haraka, kupuuzwa, au kuonekana kama usumbufu.
Lakini tafiti na uzoefu vinaonesha mtoto anayelekezwa kuuliza na kujibu maswali hujengeka zaidi kiakili, kijamii na hata kimaadili.
Kumruhusu mtoto kuuliza maswali humsaidia kukuza fikra pevu. Swali la mtoto mara nyingi si tu kutaka majibu, bali ni ishara ya ubongo wake kuanza kufanya kazi za uchambuzi. Watoto wanaouliza sana hujifunza kuchanganua mazingira yao, kuelewa sababu na athari, na hatimaye kujenga uwezo wa kutatua matatizo.
Kwa mfano, mtoto anapouliza "Kwa nini anga ni la bluu?" au "Kwa nini tunapaswa kusoma?", si tu ana utata, bali anaanza kusuka fikra za kimantiki. Kila swali linalojibiwa kwa utulivu linajenga tabaka moja la maarifa na tabia ya kutafuta ukweli.
Kujenga Ujasiri na Uwezo wa Kujieleza
Wazazi tunapaswa kuelewa kuwa kumshirikisha mtoto katika kujibu maswali huongeza kujiamini na uwezo wa kujieleza. Watoto wengi hukosa ujasiri wa kuzungumza hadharani kwa sababu hawakujengewa utamaduni wa kutoa mawazo yao wakiwa nyumbani.
Anapoulizwa swali na mzazi wake, mtoto hupata nafasi ya kuweka mawazo yake mahali na kuyatamka kwa uhuru. Hilo humsaidia baadaye anapokutana na mazingira yanayohitaji kuwasiliana kwa ufasaha shuleni, kazini, au hata kwenye maisha ya kawaida.
Mzazi anapomuuliza mtoto, "Wewe unafikiri tufanyeje hapa?" anampa ujumbe wa moja kwa moja kuwa fikra zake zina thamani.
Kuwajibika kwa Fikra
Zaidi ya hapo, kujibu maswali humfundisha mtoto uwajibikaji wa fikra. Watoto wanapozoea kuulizwa, wanapata nafasi ya kufikiria kabla ya kujibu, kutafuta mantiki, na kuwajibika kwa kile wanachosema.
Hii humjenga kijana anayejua kufikiria kwa kujitegemea badala ya kuiga au kufuata mkumbo. Katika dunia ya leo iliyojaa taarifa potofu na mitazamo mingi kinzani, uwezo wa mtoto kufikiri kwa uhuru ni hazina.
Lakini pia kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea watoto utamaduni wa kuuliza. Watoto wanaouliza hujifunza kusema "Sielewi, naomba ufafanuzi" – kauli ambayo watu wazima wengi wanashindwa kuitamka kwa sababu waliogopa kuuliza wakiwa wadogo.
Utamaduni wa kuuliza huondoa hofu ya kushindwa na huamsha tabia ya utafutaji maarifa. Mtoto anayezoea kuuliza anakuwa mtu mzima anayejifunza kila siku, anayeweza kubadilika, na anayeweza kushindana katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi.
Ufanisi Elimuni
Katika mazingira ya elimu, watoto wanaouliza maswali ndiyo wanaofanya vizuri zaidi. Maswali huongoza kwenye ufahamu wa kina, sio kukariri.
Mwalimu akitoa mada, mwanafunzi aliyezoea kuuliza atapenda kujua inamaanisha nini, inatumika vipi na ina faida gani. Haya yote humsaidia kutengeneza uelewa uliojikita kwenye mantiki badala ya kukariri tu.
Kiuhusiano, swali ni daraja. Wazazi wanapowapa watoto nafasi ya kuuliza na kujibu, wanaijenga familia inayosikilizana. Mtoto anayeuliza maswali mengi leo ni kijana atakayewafungukia wazazi wake baadaye kuhusu changamoto na maamuzi magumu.
Kusikiliza swali lake leo, hata kama linahusu mbona mbu hawalali, kunajenga mahusiano ya kuaminiana.
Hitimisho
Swali ni chombo cha ukuaji. Mzazi anayejenga mazingira ya kuuliza na kujibu anajenga misingi ya mtoto kuwa mjengaji wa hoja, mwenye fikra pana, aliyejasiri, na aliye tayari kwa maisha ya ushindani.
Kuwazuia watoto kuuliza ni kama kuzima mwanga wa taa kabla ya kuangalia kilichopo mbele.
Ni wajibu wetu wazazi kuwasha taa hiyo kwa kusikiliza, kwa kuhimiza, na kwa kuruhusu ulimwengu wa mtoto kuongozwa na swali moja baada ya jingine.