Serikali Yaahirisha Sherehe za Uhuru, Fedha Zielekezwe Kurekebisha Miundombinu
Dar es Salaam – Serikali imetangaza mwaka huu hakutakuwa na sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9, huku fedha zilizopangwa kwa shughuli hiyo zikielekewa kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na vurugu za Oktoba 29.
Uamuzi huu unakuja wiki mbili kabla ya kufikia siku ya sherehe za maadhimisho ya Uhuru, ambapo Tanzania Bara inatimiza miaka 64 tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Uingereza tarehe Desemba 9, 1961.
Kwa kawaida, maadhimisho hayo yanahusisha sherehe katika viwanja mbalimbali, zinazoambatana na maonesho ya vifaa vya kijeshi na hatua zilizopigwa tangu uhuru, huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakialikwa kuhudhuria.
Miundombinu inayohitaji kurekebishwa kwa fedha hizo ni pamoja na vituo vya mabasi yaendayo haraka, barabara, vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa na maeneo mengine ya umma yaliyochomwa moto katika vurugu za Oktoba 29.
Katika vurugu hizo, ukiacha miundombinu ya umma iliyochomwa moto, watu binafsi waliharibiwa biashara zao, wapo waliopoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Taarifa ya kutokuwepo kwa sherehe hizo imetolewa jijini Dar es Salaam Novemba 24, 2025 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alipozungumza katika mkutano wa hadhara baada ya ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29.
"Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Desemba 9 hakutakuwa na sherehe za kuadhimisha na gharama ya fedha ambazo zilikuwa zitumike kwenye sherehe ameelekeza ziende kutengeneza miundombinu hii iliyoharibika," amesema Dk Nchemba.
Waziri Mkuu ameagiza kuanzia sasa, sekta zinazohusika zikae na kuanza kuratibu fedha zote zilizopangwa kwa ajili ya sherehe, zipelekwe haraka kurekebisha miundombinu iliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe amefafanua kuwa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka pekee, ukarabati wake hadi huduma kurejea unahitaji Sh12.5 bilioni.
Profesa Shemdoe amesema kutoka Kariakoo hadi Kimara kuna vituo 20 vya mabasi hayo na vyote vimeharibiwa katika vurugu hizo, maeneo yaliyoathirika zaidi ni mifumo ya umeme, kukusanyia nauli na vioo.
Huduma Zirejee Ndani ya Siku 10
Dk Nchemba katika hotuba yake ameagiza Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na wadau wote wanaohusika wakae na kutengeneza utaratibu wa mpito ili kurejesha huduma za usafiri huo ndani ya siku 10 Barabara ya Morogoro.
Ametaka mageti yaliyokuwepo na hayakuwa yanatumika yawekwe na kuanza kurejeshwa masuala ya mawasiliano, umeme na maeneo ya kukusanya mapato na ndani ya siku 10 shughuli zirejee kama kawaida.
"Kaeni kuanzia leo husisheni wadau wote, makandarasi, mabenki wadau wote kwenye kila eneo, mnaona kuna mmoja wapo anahusika tupate suluhisho la mpito wakati tunaandaa kurejesha katika utaratibu wake wa kawaida," amesema.
Waziri Mkuu ametaka miundombinu itakaporejea wananchi wote wawe walinzi kwa kuwa ni mali yao.