Dar es Salaam. Mashahidi 60 wanatarajiwa kuitwa na Jamhuri katika kesi ya uhujumu wa kiuchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Jatu Public Limited Company (PLC), Peter Gesaya na wenzake, inayohusiana na ubadhirifu na utakatishaji wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.
Mbali na idadi hiyo ya mashahidi, Jamhuri inatarajia kuwasilisha jumla ya vielelezo 136, ambapo 104 ni nyaraka na 32 ni vitu halisi.
Idadi hiyo ya mashahidi pamoja na vielelezo imebainishwa na waendesha mashtaka Ijumaa, Novemba 21, 2025, wakati wa mwenendo wa kabidhi (committal proceedings).
Katika hatua hiyo, waendesha mashtaka wamewasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi hao pamoja na vielelezo hivyo.
Washtakiwa wamesomewa maelezo hayo na jopo la waendesha mashtaka watatu lililoongozwa na Wakili wa Serikali Roida Mwakamele mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Geoffrey Mhini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.
Mbali na Gesaya, washtakiwa wengine katika kesi namba 491356 ya mwaka 2023 ni Nicholaus Fuime, Esther Kiya, Habiba Magero, Mariam Mrutu, Mariam Kusaja, Lucy Izengo na Jatu PLC.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 37, mashtaka matano yakiwahusu washtakiwa wote na mashtaka 32 yakiwahusu mshtakiwa wa kwanza Gesaya na wa nane Jatu PLC peke yao.
Mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni pamoja na kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia hasara mamlaka, huku mashtaka 33 yakiwa ya utakatishaji wa fedha.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari 1, 2019 hadi Desemba 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.
Mashtaka Makuu
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kuandaa genge la kihalifu kwa nia ya kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi 3,149,172,167 mali ya Jatu Savings and Credit Cooperative Society Limited.
Katika shtaka la pili, washtakiwa wa kwanza Gesaya na wa pili Fuime wanadaiwa kuwa Februari 28, 2019 Dar es Salaam, wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao kama Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Jatu Saccos na Jatu PLC, walitumia vibaya nafasi zao kwa kusaini makubaliano kati ya Jatu PLC na Jatu Saccos.
Wanadaiwa kusaini mkataba huo kinyume na Kanuni za Vyama vya Ushirika za mwaka 2015 na Vyama vya Akiba na Mikopo za mwaka 2019, na kusababisha Jatu PLC kupata faida isiyostahili yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.1.
Shtaka la tatu linawahusu washtakiwa sita, wa pili hadi wa saba, ambao wanadaiwa kuwa kati ya Januari 1, 2019 na Desemba 31, 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watia saini wa akaunti ya benki ya NMB ya Jatu Saccos, walitumia kwa maslahi yao binafsi zaidi ya shilingi milioni 63 mali waliyoaminiwa.
Shtaka la nne linawakabili washtakiwa wote kwa kusababisha Jatu Saccos hasara ya kifedha kwa kujihusisha moja kwa moja katika miamala ya zaidi ya shilingi bilioni 3.1, wakijua kuwa fedha hizo ni matokeo ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali.
Shtaka la tano ambalo ni la utakatishaji wa fedha linawahusu washtakiwa wote. Wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Januari 1, 2019 na Desemba 31, 2021, walijihusisha moja kwa moja katika miamala ya kifedha inayohusisha zaidi ya shilingi bilioni 3.1, wakijua kuwa ni mazao ya kosa la ubadhirifu.
Mali Iliyonunuliwa
Mashtaka 32 ya utakatishaji wa fedha kuanzia shtaka la 6 mpaka la 37 yanamkabili mshtakiwa wa kwanza Gesaya na wa nane Jatu PLC, wakidaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Julai 1, 2017 hadi Februari 25, 2025.
Wanadaiwa kununua mali mbalimbali zikiwemo magari, pikipiki, trekta na shamba.
Magari yanayohusika ni aina za Toyota IST, Nissan X-Trail, Suzuki Carry, Toyota Rav 4, Toyota Alphard, Toyota Mark II, Toyota Noah, Toyota Land Cruiser Prado, Toyota Succeed, Toyota Townace Noah na Toyota Fancargo.
Pia matrekta aina ya New Holland Model TT65 4WD, New Holland Model TT55-2WD, New Holland Model TD Straddle 80 4WD, New Holland Model AGR Tractor, mashine ya kuvunia aina ya Field King Combiner Harvester, malori mawili aina ya Mitsubishi Canter na Toyota Toyoace.
Vilevile pikipiki sita, moja aina ya Sanlag Model SL125-5 na nyingine tano aina ya Fekon, pamoja na shamba lenye hati namba 288 LO Na. 184971 lenye ukubwa wa ekari 500 lililopo Matui, Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia mali hizo kwa fedha zilizotokana na kosa la ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali.
Mashahidi na Ushahidi
Katika mashahidi wamo maofisa sheria kutoka Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA) na mamlaka za usajili wa vyama vya ushirika na taasisi za akiba na mikopo, pamoja na kitengo cha usajili wa vyombo vya moto cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia wamo wanachama wa Jatu kutoka fani mbalimbali wakiwemo wastaafu kutoka taasisi za kifedha na askari polisi.
Katika maelezo yao, mashahidi wameelezea usajili wa kampuni ya Jatu PLC inayojihusisha na uwekezaji katika kilimo cha mazao mbalimbali na Jatu Saccos, taratibu za uendeshaji na jinsi wanachama walivyojiunga.
Wameeleza ahadi na mikakati waliyopewa, uwekezaji walioufanya, faida waliyonufaika awali kabla ya baadaye kukwama kwa kutokulipwa pesa zao ambazo wanadai mpaka sasa.
Vilevile wameeleza uhamishaji wa fedha kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos kwenda kampuni ya Jatu PLC, wakibainisha taratibu zilizopaswa kuzingatiwa pamoja na kuwepo kwa mkataba wa makubaliano ya mkopo ambao hawajawahi kuuona.
Hadi sasa maelezo ya mashahidi 40 tu yamesomwa kati ya 60, na Hakimu Mhini ameahirisha kesi hadi Jumatatu Novemba 24, 2025, kuendelea kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi waliosalia pamoja na vielelezo vyenye kurasa zaidi ya 4,000.