Rais Mwinyi Afanya Mabadiliko Makubwa ya Wakuu wa Wizara Zanzibar
Unguja – Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amefanya mabadiliko makubwa ya viongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuteua na kubadilisha makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu katika wizara kadhaa.
Katika uteuzi huo, makatibu wakuu wa wizara nane wamebadilishwa na manaibu katibu wakuu wa wizara tano, wakiwemo wakuu wa mikoa wawili waliokuwa wakihudumu katika nafasi hizo.
Katika wizara tisa, makatibu wake wakuu wameendelea kuwa walewale waliokuwapo awali. Wateule wote wataapishwa Jumamosi Novemba 22, 2025 katika Ikulu ya Zanzibar.
Kulingana na taarifa kwa umma iliyotolewa Novemba 20, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said, Mattar Zahor Masoud aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Salama Mbarouk Khatib aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji.
Dk Rahma Salim Mahfoudh aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango. Saleh Mohamed Juma ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo akitokea kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo.
Ali Said Bakari ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe.
Mabadiliko ya Makatibu Wakuu
Fatma Mabrouk Khamis amehamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu akitokea Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Khamis Suleiman Mwalimu amehamishiwa Wizara ya Kazi na Uwekezaji akitokea Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Dk Habiba Hassan Omar amehamishiwa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Uteuzi wa Manaibu Katibu Wakuu
Mohamed Dhamir Kombo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo na Uhakiki wa Chakula.
Amos John Enock ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Awali, alikuwa Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rashid Ali Salum amehamishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji akitokea nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Makame Machano Haji ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, akitokea Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Khalid Masoud Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji akitokea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.