Rais Samia Atahutubia Bunge: Wananchi Wana Matarajio Saba Muhimu
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan kesho Ijumaa Novemba 14, 2025 atalizindua Bunge kwa kulihutubia ambapo pamoja na mambo mengine, wananchi watarajia kusikia masuala saba muhimu.
Masuala hayo ni msimamo wa Serikali kuhusu maandamano yaliyozaa vurugu na vifo wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 na mikakati ya kurejesha hali ya kawaida na kuondoa mgawanyiko, mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya na utekelezaji wa ahadi zake za uchaguzi.
Matarajio mengine ya wananchi katika hotuba hiyo kwa Taifa, ni kusikia namna gani Rais atawafariji wananchi wakiwemo wafiwa na waathirika wa maandamano hayo, msimamo wa Serikali kuhusu kuzuia matukio ya utekaji na kupotea kwa watu, pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ufisadi na rushwa.
Matarajio hayo yameelezwa na wananchi waliohojiwa, siku moja kabla ya Rais Samia kulifungua rasmi Bunge la 13, katika kipindi cha pili cha uongozi wake.
Wakati Rais Samia akizungumza mara tu baada ya kuapishwa Chamwino Dodoma, alisema katika hotuba hiyo kwa Bunge na taifa, atatoa mwelekeo wa Serikali yake, wananchi na wanazuoni kwa upande wao, watarajia pia kusikia sauti ya mamlaka kuhusu suluhisho la yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na namna Serikali itakavyoshughulikia tatizo hilo ili lisijirudie.
Kutatua Matatizo ya Taifa
Katikati ya matarajio mengi, Profesa George Kahangwa, mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema hotuba ya kwanza ya Rais kwa Bunge mara nyingi huchora ramani ya utekelezaji wa mipango aliyoipanga kwa miaka mitano ya uongozi wake.
Amesema kupitia hotuba hiyo, mkuu wa nchi hueleza Serikali yake inakusudia kufanya nini na matarajio yake mbele ya wabunge, ambao kimsingi ndio wawakilishi wa wananchi.
Hata hivyo, kutokana na uhalisia wa mazingira yaliyopo, Profesa Kahangwa anatarajia hotuba hiyo itagusia maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29, mwaka huu na kusababisha vifo, uharibifu wa mali za umma na binafsi na kesi mbalimbali kufunguliwa.
"Ni matarajio kwamba Rais akizungumza, Watanzania watakuwa wanasubiri kwa hamu kuona atasemaje, hasa kufafanua hoja yake ya maridhiano katika falsafa ya 4R, ahadi zake ndani ya siku 100 na lililotajwa na Makamu wake (Dk Emmanuel Nchimbi), alipokuwa kwenye vikao vya SADC," amesema.
Kwa kuwa baadhi ya watu wana maumivu, amesema Watanzania wengi wanasubiri kwa hamu kusikia kauli ya faraja ya mkuu wa nchi na hatua atakazotangaza.
"Atafanya nini kwa kipindi tunachokiendea huenda lisivute hisia za wengi, tofauti na namna gani Serikali yake italishughulikia ili tuishi kwa amani kama ambavyo tumeishi kwa miaka 60 iliyopita," amesema Profesa Kahangwa.
Mbali na hilo, Profesa huyo amesema ni matarajio yake kumsikia Rais Samia akizungumzia mambo mbalimbali yanayolisibu Taifa ukiwemo ufisadi na rushwa na matukio ya kutoweka na kupotea kwa watu.
"Watanzania wangependa kujua hili, maana watu wanakula mpaka wanavimbiwa huku vijana hawana ajira, sababu ni mambo ya rushwa na ufisadi," amesema.
Amesema ni matarajio yake katika hotuba hiyo, Rais atagusia uanzishwaji wa mchakato wa Katiba mpya kama alivyoahidi wakati wa kampeni zake, kwani ni suala muhimu na limeombwa kwa zaidi ya miongo mitatu.
Amesisitiza matarajio ya wengi ni kujua mikakati ya Serikali kiuchumi, utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 hasa katika mambo ya maendeleo ya watu na uchumi.
Suala la yaliyotokea Oktoba 29 na siku kadhaa zilizofuata, limezungumziwa pia na Dk Conrad Masabo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Yeye amesema namna nzuri ya kuliweka sawa, ni Rais Samia kukiri hadharani kwamba mzizi wa kilichotokea ni hali ya kutosikilizana iliyokuwepo kabla ya matukio hayo.
"Njia pekee na nzuri ya kueleza masuala hayo ni kukubali kwamba yaliyotokea yamesababishwa na sisi kutosikilizana, hasa upande wa Serikali kukubali kwamba haikusikiliza," amesema.
Mhadhiri huyo anatarajia hotuba hiyo, itaweka wazi kwamba Serikali imetambua wananchi wake wamebadilika, wanaposema kitu kinahitaji kushughulikiwa, basi kishughulikiwe na ahadi ya kutatua changamoto zilizopo itolewe.
"Natarajia hotuba hiyo ieleze yaliyokuwepo kabla ya tukio na kuiweka Serikali kwenye nafasi kwamba kweli hatukufanya vya kutosha kushughulika na matatizo yaliyotokea, na ndiyo maana yakatokea yote na kisha iahidi kuyafanyia kazi," amesema.
Maridhiano na Mchakato wa Katiba
Miongoni mwa njia zinazotazamwa katika kushughulikia mpasuko uliopo ni maridhiano, njia ambayo, Mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia, Thomas Kibwana amesema inapaswa ijitokeze kwenye hotuba ya Rais ya kufungua Bunge, na kutoa dira yake kwa miaka mitano ijayo na kwa vizazi vijavyo pia.
Amesema anatarajia kusikia kuhusu ahadi ya kuunda tume ya maridhiano na kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya, kwa kuwa mambo hayo yatatoa dira ya Tanzania kwa miaka mingi ijayo.
Vilevile, amesema Rais kupitia hotuba hiyo, ataeleza vipaumbele vya Serikali yake na aina ya uongozi anaotarajia, hasa zile ahadi alizoahidi ndani ya siku 100 za kwanza.
Mbali na wanazuoni, hata taasisi za kiraia zimeelekeza masikio yake kwa Rais Samia, kama anavyoeleza Manga Msalaba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Safer World Organisation la jijini Mwanza, kuwa anatarajia kusikia Rais Samia akitoa pole kwa waathirika wa maandamano na kuwafariji.
"Natarajia atatoa pole kwa waathirika wa maandamano kwa kuwa yeye ndio mfariji namba moja na hasa ukizingatia waliouawa si wote walikuwa waandamanaji. Pia, kwenye hotuba yake agusie namna ambavyo Taifa litatoka hapa tulipo twende mbele tukiwa wamoja na kuimarisha utawala sheria," amesema.
Kuhusu maridhiano, Msalaba amesema ni suala lingine analotarajia liguswe katika hotuba hiyo na Rais Samia aweke wazi, yatafanyika kuanzia lini, kwa kuwa kukosekana kwa hayo ndiko kulikosababisha vurugu hizo.
Ajibu Maswali ya Wananchi
Kiu ya wananchi haiachani sana na maoni ya wanazuoni na asasi za kiraia, ni kusikia kauli ya mkuu wa nchi kuhusu vurugu za Oktoba 29 na uamuzi atakaotangaza kuuchukua ikijibu maswali kadhaa waliyonayo, kama anavyoeleza James Dawson, mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha.
"Tunatamani kujua mwelekeo wa Serikali yake, pili tunatamani atenge dakika kugusia kuhusu suala la maandamano na kile kilichotokea kwenye vurugu zilizozaa vifo na majeruhi, hatua za Serikali kutatua changamoto zinazolalamikiwa, pia natamani kusikia kuhusu ahadi zake," amesema.
Zaidi ya hilo, wanataka hotuba ya Rais iwe na ujumbe wa umoja, amani na kujenga upya imani kati ya wananchi na Serikali.
"Tangu yatokee mauaji, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali za wafanyabiashara, wajasiriamali na umma, hatujamsikia Rais akieleza kwa kina. Ukimya umetawala, tunatarajia neno kutoka kwake, ili kurudisha imani ya Watanzania kwa Serikali iliyopo madarakani," amesema Festo Mwilo mkazi wa Kimara, Dar es Salaam.
Kama ilivyo kwa wengi, Victor Mwakipesile anayeishi Mbeya anatarajia kusikia kauli na msimamo wa Serikali kuhusu vurugu za siku ya uchaguzi na namna tatizo litakavyomalizwa.
"Ushauri ni mwingi sana, lakini kubwa tuone mwelekeo mpya wa Taifa kumaliza migogoro ndani na nje ya siasa na hakikisho la vurugu zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu zisitokee tena," amesema.
Kwa upande wake Ephraim Mwanjojele, mkazi wa Mbeya, anatarajia hotuba hiyo itangaze kuwaachia huru viongozi wa kisiasa waliopo mahamakani na kuunda tume ya maridhiano.
"Kuna viongozi hasa wa vyama vya upinzani wapo mahamakani muda mrefu, kuna waliokamatwa wakati na baada ya uchaguzi mkuu, waachiwe huru na kuwepo uhuru wa vyombo vya Habari," amesema.
Abraham Saiguran anayeishi Olorien jijini Arusha, amesema anatarajia kumsikia Rais Samia akizungumzia namna ya kuufufua mchakato wa Katiba mpya, kwani ni suala muhimu kwa mustakabali wa taifa.
"Suala hili limekuwa likizungumzwa kila mara kuanzia kipindi cha kabla ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, hili limekuwa likipigiwa kelele na makundi mbalimbali ya jamii, hivyo linaonekana ni hitaji muhimu kwa wananchi," amesema.
Kwa upande wa Julius Mollel, ni matamanio yake katika hotuba ya Rais pamoja na masuala mengine, azungumzie kujenga upya Taifa hasa katika kipindi ambacho kumemalizika uchaguzi mkuu.
Amesema maridhiano yatasaidia kuondoa changamoto inayoendelea katika makundi mbalimbali ya jamii hasa kutokana na vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu.
"Tunatamani Rais azungumzie suala la maridhiano na lifanyike kwa vitendo ili kuhakikisha umoja wa taifa letu unarejea," amesema.
Hata hivyo, Mkazi wa Mwanza, Masele Justine amesema hatarajii zaidi ya kile alichokizungumza Rais Samia wakati anakabidhiwa cheti cha ushindi wa nafasi ya urais.
"Nilitarajia atatoa pole kwa familia zilizopoteza vijana wao ambao wengine hawakuwa kwenye fujo wala maandamano, bali risasi ziliwafata wakiwa kwenye biashara zao au nyumbani kwao. Lakini alisema nini? Alisema ni vijana kutoka nje wamekuja kufanya vurugu," amesema.
Kwa upande wake Dhahili Juma, amesema anatarajia mkuu wa nchi azungumze jambo litakalowapa faraja wazazi waliopoteza watoto wao kati ya Oktoba 29 hadi Novemba 6, 2025 kwa kuwaagiza wasaidizi wake wakabidhi miili kwa wafiwa bila masharti.
Ametaka suala la amani linalozungumzwa liambatanishwe na haki kwa kuwa ni vitu vinavyoenda sambamba.
"Hakuna mtu asiyependa amani, lakini hakuna mtu anayeweza kuvumilia siku zote kunyimwa haki yake. Hivyo natarajia kumsikia anavyoongelea jinsi ambavyo ataimarisha utoaji haki kwa wananchi hasa wa hali ya chini," amesema.