Mafyatu na Tatizo la Ukosefu wa Ubunifu
Kuna mafyatu wenye ugonjwa wa ukosefu wa ubunifu kiasi cha kugeuzwa wadudu. Wadudu hawa wana silaha moja tena ya hovyo. Nayo ni kujikomba, kusifia hata ujinga, kujigongagonga, kutabiri upuuzi, kuimba pambio na mashairi tena wamuimbiaye akiwa kipofu na taahira. Je, hapa tatizo ni nini? Ni wale wasifuo au wale wasifiwao au wote? Kwani, nani asiyejua? Kizuri huwa chajiuza na kibaya chajitembeza?
Sijui kwanini maneno haya yanajitokeza, lakini yanabeba ukweli mkubwa. TNC inakubaliana na hoja kwamba, asiyejua hili ajue. Anayejua akupuuzia ajue. Anajipuuzia mwenyewe. Onyo, si kila wakusifuo wanakusifu. Wengi wanakuramba kichogo na kukugeuza bunga wakutumie na wakishafanikiwa, unatupwa kama diaper achia mbali ganda la muwa.
Sifa za Uongo ni Hatari
Wanakuponda wakikudanganya wanakupenda wakati ukweli mchungu ni kwamba wanakuchukia. Kahaba huwa hapendi wateja wake bali mifuko yao fedha. Zikiisha, nawe unaisha. Uliyedhani anakupenda, anaweza kukulinganisha hata na kaburi. Ukimpenda mtu vilivyo na kimakweli ni kumwambia ukweli hata kama unauma, siyo kuuma na kupuliza.
Kitimoto ni kiti fire hata apakwe blusher. Juhaa ni juhaa hata aitwe mjuvi. Kiti fire ni mchafu tu hata apakwe mafuta na kufukizwa ubani na utuli. Fisi ni fisi hata avishwe ngozi ya kondoo. Cha hovyo ni cha hovyo hata kisifiwe vipi bado kibaki kuwa hovyo.
Ubaya ni ubaya hata uitwe uzuri hauishi ubaya wake. Urongo ni urongo hata uitwe ukweli na kuaminika bado ni uongo. Hakuna uongo mbaya kama kuwadanganya wengine halafu nawe ukajidanganya. Isitoshe, hakuna uongo wa kudumu bali ukweli.
Utumwa wa Hiari
Ni mpumbavu apangaye kupaka rangi upepo. Mtumwa awe wa kujituma au kulazimishwa ni mtumwa. Tofauti ni kwamba mtumwa wa kulazimishwa anaweza kujikomboa ilhali yule wa hiari anachukia na kuogopa ukombozi. Huyu, hana tofauti na kuku atagaye mayai na kulishwa nafaka kavu ilhali mayai yake yenye virutubisho yakiliwa na wengine. Mbwa hulinda mali lakini yu maskini daima. Sindano hushona nguo ila siku zote i uchi.
Mashindano ya Hovyo
Hakuna mashindano mabaya na ya hovyo kama mtu kushindana mwenyewe. Unapowaua au kuwazuia wapinzani wako kuingia uwanjani mshindane ukashindana na ombwe, kweli unashindana au unajidanganya? Huwezi kuniandikia haki halafu ukaziua na kunifanya nizipate zikawa haki. Hii si haki bali dhihaka.
Woga ni ugonjwa mbaya ambaye humfanya mwoga kujifanya shujaa wakati ni mwoga. Kuna wakati mafyatu wasiofyatuka wakafyatua wanaogopa hata vivuli.
Matokeo ya Uovu
Asiyejua wala kuchelea kesho hana tofauti na maiti. Unawezaje kutenda mabaya ukategemea mema? Unawezaje kuumiza wenzako nawe usiumizwe hata kama si leo wala kesho. Watenda maovu wanajua uovu wao. Hata hivyo, japo wanajua matokeo ya uovu huu, wengi hujifanya hamnazo na kujitoa akili wakidhani siku yao haitafika.
Wenye akili sawa sawa huwapenda wanaowakosoa na kuchukia wanaowasifia ujinga na uongo. Heri akulaumuye kwa haki kuliko akusifuye kwa hila. Kwani, hawapo? Jana, walimsifu fulani. Leo wanambagaza. Walijifanya wanampenda. Leo, wanamchuuza tena kwa sababu ya sifa na udohoudoho.
Ogopeni Sifa za Uongo
Ndugu zanguni ogopeni sifa. Sifa za uongo ni mbaya kuliko hata upupu kwani, waweza kuoga ukakutoka. Sifa za wenye hila ni kaburi la wamsifiaye. Kwani, humpotosha na kumdanganya akapotoka, akadanganya na kujidanganya.
Waweza kudhani mko pamoja kumbe kila mtu ana safari yake. Wapo wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa ili unogewe wakupige visu. Tumeyaona au tunajisahaulisha?
Ukiona mchugaji anamsifu ng’ombe unono, ujue ana mpango wa ima kumuua au kumuuza. Kuku hata alale kwenye kitanda, bado ni kuku. Atayarunda humo. Nani awezaye kumfuga swila asimng’ate. Heri swila swila kuliko swila mdudu.
Busara ni Nini?
Kunyamaza si ujinga na kusema sana si busara. Kuna wakati mtu anapaswa kukubali kujisuta kabla ya kusutwa. Heri ajisutaye kuliko asutwaye japo kote ni kusuta. Ni kiziwi pekee asiyesikia wala kufaidi muziki. Ni kipofu pekee asiyehitaji mwanga.
Nondo ni mdudu wa ajabu. Huona moto na kujitupa mwenyewe akidhani anaota moto.
Onyo, usione wamenyamaa ukadhani hawajui chafu yako hata kukuzushia.