Jeshi la Zimamoto Mbeya Lipokea Magari Tisa ya Kisasa
Mbeya – Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya limepokea magari tisa ya kisasa yatakayosaidia kukabiliana na majanga ya moto na ajali mkoani humo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo mkoani humo, Gervas Fungamali, amesema upatikanaji wa magari haya unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya majanga na ajali za moto zilizokuwa zimeshamiri katika mkoa huo.
Akizungumza leo Oktoba 27, 2025 wakati wa kupokea magari hayo, Fungamali amesema awali walikuwa wakipata changamoto kukabiliana na matukio hayo kutokana na upungufu wa vifaa.
Ameeleza kuwa Jeshi hilo lilikuwa na magari mawili tu, hivyo upatikanaji wa magari tisa ya kisasa yanaenda kusaidia ufanisi wao katika kukabiliana na majanga ya moto na ajali za barabarani.
"Niwahakikishie wananchi mkoani Mbeya kwamba usalama wao na mali zao viko salama, tutatumia vyema vifaa hivi kutimiza wajibu wetu na tutavitunza vizuri tuweze kufikia malengo, zaidi tunaishukuru Serikali," amesema Fungamali.
Kamanda huyo ameongeza kuwa kwa wiki hupokea matukio matatu ya ajali za moto huku akiwaomba wananchi kutochoma hovyo moto haswa kipindi hiki cha kiangazi akiahidi jeshi hilo kuendelea kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu.
Akizindua magari hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameliomba jeshi hilo kutunza magari hayo na kuwafikia wananchi kwa elimu namna ya kujikinga na majanga ya moto.
"Hakuna sababu kujua gharama ya magari haya, kwa sababu hata kwa macho unagundua ni fedha nyingi sana, sasa niwaombe msikae ofisini, nendeni kwa wananchi muwape elimu na tunzeni vyema magari haya," amesema Malisa.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia mapokezi ya magari hayo, Benson Muya, amesema vifaa hivyo huenda ikawa sehemu ya kuwafikia wananchi wengi wanaokumbwa na majanga ya moto.